JUMATANO
WIKI YA 13 YA MWAKA-B
30/6/2015
30/6/2015
Somo: Mwa 21:5,8-20
Zab:
33:7, 8-9, 10-11, 12-13
Injili: Mt 8:28-34
Nukuu
“Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na
mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka,” Mwa 21:10
“Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni
pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara,
sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa,” Mwa 21:12
“Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye
ni uzao wako,” Mwa 21:13
“Na tazama, wakapiga
kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya
muhula wetu?” Mt 8:29
“Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na
kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini,”
Mt 8:32
“Na tazama, mji wote ukatoka kwenda
kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao,” Mt 8:34
TAFAKARI: “Damu
nzito kuliko maji.”
Wapendwa wana Mungu, usemi huu “damu nzito kuliko
maji,” unajidhihirisha katika tafakari ya masomo yetu ya leo. Kwa maana
nyingine chako ni chako tu hata kama kinadharaulika au kudharauliwa. Mama mzazi
aliyepata uchungu wa kuzaa, na baadaye mtoto yule akawa na tabia mbaya, mfano:
wizi wa kupindukia, mama huyu kwa vile ni mwanaye hawezi kamwe kumkana. Ni
afadhali afe na mwanaye akiwa anachomwa moto kuliko kumkana. Katika somo la
kwanza tunaona hali hiyo ikimtokea Ibrahimu baada ya kauli ya Sara mkewe
kutomtaka mtoto wa Hajiri, Ishamaeli. Maneno ya Sara ni
mazito sana na yasiyokuwa na chembe ya uzazi, na upendo ndani yake. Sara
anamwambia Ibrahimu, “Mfukuze
mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu,
Isaka,” Mwa 21:10. Tuelewe kwamba mwana huyu wa mjakazi, Ishmaeli halikuwa
kusudi la Ibrahimu kuwa na mtoto nje ya ndoa yake. Ni Saha huyu huyu
aliyemshawishi Ibrahimu kutembea na Hajiri ili amzalie mtoto, baada ya kuona
umri wake umesogea. Ibrahimu anafadhaika sana kwa kitendo hiki cha mkewe Sara.
Hata hivyo, ikiwa yote hayo ni mpango wa Mungu katika safari
ya ukombozi wa mwanadamu, ‘pasipo njia Mungu hufanya njia.’ Mungu analifumbua
fumbo hili kwa Ibrahamu na kusema, “neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa
ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti
yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa,” Mwa 21:12. Fumbo la Mungu kati
ya Sara, Hajiri, na Ibrahimu ni kwamba, “katika Isaka uzao wa Ibrahimu
utaitwa.” Hapa ndipo kwenye mtego, na mkono wa Mungu. Mara nyingi Mungu aweza
kufanikisha mambo yake kwa njia ya pekee na wakati mwingine si rahisi kufahamu
kwa akili zetu kama binadamu.
Kwa upande wetu binadamu kuelewa mafumbo mazito kama haya
twaitaji utulivu wa ndani. Ni katika utulivu Mungu hujidhihirisha. Mfano, Mungu
anajidhihirisha kwa Nabii Isaya kwa namna hii: “Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana
akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele
za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko
la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na
moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu,”
1Fal 19:11-12. Tunapopatwa na jambo la kutuhuzunisha, moyo wetu hupitia hatua
mbalimbali kama upepo wa nguvu, tetemeko la nchi, na moto. Katika hali hizi
zote za uchungu na hasira Mungu hawezi kamwe kujidhihirisha ndani yetu. Hivyo
katika hali kama hiyo yakupasa kutulia na kutokufanya chochote zaidi ya
kutafakari hali ile. Kwa maana nyingine usifanye maamuzi yoyote ukiwa katika
hali ya hasira. Mwisho wa hasira yako
maamuzi uliyoyafanya yatakugharimu maisha yako, na hali yako. Ibrahimu
hakuchukua taharuki ya kumlaumu mkewe Sara kwa kitendo kile kisichopendeza.
Ibrahimu anazama katika tafakuri, na katika sintofahumu hiyo, Mungu
anajidhihirisha. Mungu hamtupi mja wake hata mara moja. Mungu anampango na kila
mmoja wetu, hata kama kwa namna tulivyo iliwashangaza watu au bado
inawashangaza wele tunaoishi nao. Kuzaliwa kwako
hakukutokana na makosa wala bahati mbaya, na maisha yako si tokeo la bahati tu
ya asili.
Wazazi wako wanaweza kuwa
hawakupanga kukuzaa lakini Mungu alipanga. Mungu hajashangazwa hata kidogo na
kuzaliwa kwako. Kwa kweli, alitegemea uzaliwe. Hapo zamani kabla hujatungwa
mimba na wazazi wako, ulitungwa katika mawazo ya Mungu. Alikufikiri kwanza. Si
jambo baya, wala bahati au tukio la bila kutegemewa kwamba wewe unapumua kwa
wakati huu. Uko hai kwa sababu Mungu alitaka kukuumba! Maandiko Matakatifu
yanasema, “Bwana atatimiza kusudi lake kwangu,” Zab 138:8. Hivyo ni kwa mtazamo
huu Mungu anampango na Ishmaeli. “Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye
ni uzao wako,” Mwa 21:13. Kwa maana nyingine Ishaeli ni damu ya Ibrahimu, hivyo
si vizuri Ibrahimu kumtelekeza Ishmaeli.
Wapendwa wana wa Mungu, damu nzito kuliko maji. Somo la Injia
tunaona ni kwa namna gani mapepo wanatambua mamlaka ya Yesu na kuweweseka.
Mapepo wanapohisi uwepo wa Yesu, amani yao yote hutoweka. Hili ndilo lile jina
lililopita majina yote, na kwalo hakuna nguvu za kuzimu zinazoweza kustahimili
kishindo chake. “Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru
kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile,” Mdo 16:18. Ni kwa namna hii mapepo yanakiri Jina la Yesu
na mamlaka yake. “Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa
Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?” Mt 8:29. Uwepo wa Mungu ni mwanzo na mwisho wa
vyote, yaani alfa na omega. Katika maana hii, wanachojitetea hawa mapepe kuhusu
muhula wao, hakina maana yoyote kwa uwepo wa Mungu. Taratibu za Mungu
haziingiliwi na roho yoyote ile au
kiumbe chochote kile. Ikiwa hivyo, huyu
siye Mungu mwenye mamlaka (alfa na omega). Mamlaka ya Kristo ni ya milele kwa
sababu, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho
chote kilichofanyika,” Yoh 1:3
Ni ukweli usiotia shaka kwamba wengi tunajiuliza kwa nini basi
Yesu anayaruhusu yale mapepo yawaingie wale Nguruwe na kusababisha hasara kubwa
kwa yule mfugaji? Kwa nini Yesu asingetumia njia nyingine na huyu anayejikwamua
katika mazingira magumu kimaisha na kimapato kwa njia hii ya ufugaji asipate hasara? Wapendwa wana wa
Mungu, tunarudi pale pale kwamba, “damu nzito kuliko maji.” Yesu Kristo amekuja
kumweka binadamu huru kutoka vifungo vya dhambi. Uhai wa binadamu ni lengo la
kwanza na makusudi ya Mungu na uumbaji wake wote. Binadamu ni mtawala wa viumbe
vyote, na kuviendeleza, binadamu akiwa kiumbe shirikishi cha Mungu katika
uumbaji wake wa pili. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu;
wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote
pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26. Hivyo Yesu
kuwaruhusu wale pepo kuwaingia wale Nguruwe kumelenga hadhi hii aliyopewa
binadamu. Mungu hawezi kuacha sura na mfano wake upotee bure.
Hivyo Yesu anayaruhusu yale mapepo na kusema, “Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi
lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini,” Mt 8:32. Hadhi aliyonayo binadamu ni kubwa sana mbele ya uso wa Mungu.
Yesu analisema jambo hili na kutufunulia kiu yake juu ya nafasi na uwepo wetu
mbele ya Mungu. “Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi
hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora
ninyi kuliko mashomoro wengi,” Lk
12:6-7. Ndugu yangu kwa nini wajidharau basi na kujiona hufai mbele za hao
wanaokuzunguka. Elewa jambo hili: Yesu mara zote anakuambia hivi, “nakupenda
kuliko kitu chochote katika ulimwengu huu, na ndiyo maana sikuona aibu kufa
kifo cha aibu kwa sababu yako.”
Kwa tendo hili Yesu alilolifanya, kuwaruhusu mapepo kuwaingia
wale nguruwe, watu wa kijiji kile hawakumwelewa. Watu wale walijawa hofu na
furaha. Furaha kwa sababu ya tendo lile la kimungu na watu wale kupona, na hofu
kwa sababu hawakujua ni jambo lipi lingine baya litakaloweza kutokea kwao kama
mtu huyu ataendelea kuwa kijijini pale. Kama kwa muda mchache tu ule nguruwe
wale wote walipoteza uhai, itakuaje mtu huyu akiendelea kukaa nasi hapa
kijijini mwetu? Wakasema nishiiiida! Hivyo
“na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao
walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao,” Mt 8:34. Ndugu yangu huyu ndiye
Yesu anayetupenda bila kipimo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE YESU
ASANTE KWA KUNIPENDA KAMA NILIVYO. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario