domingo, 28 de junio de 2015

TAFAKARI: SHEREHE YA WATAKATIFU PETRO NA PAULO MITUME

SHEREHE YA MT. PETRO NA PAULO, MITUME
29/6/2015
Somo: Mdo 12:1-11
Zab: 33
Somo II: 2Tim 4:6-8, 17-18
Injili: Mt 16:13-19 
Nukuu:
Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi,” Mdo 12:11

Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7

Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18

Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16

Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18

Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16.19

TAFAKARI: “Utume si lelemama, bali ni kuvumilia hadi ushindi wa kweli.”

Wapendwa wana wa Mungu, neno utume si geni masikioni mwenu. Ila tusikiapo neno utume yatupasa kwanza kabisa tuelewa ukweli huo na uhasilia wa maisha hayo ya kiutume kwamba hayana uhusiano na faida binafsi. Ni utumishi uliotukuka, na usiojifungamanisha na maslahi binafsi. Ni msukumo wa maisha unaotutaka kujitoa zaidi kwa ajili ya wengine bila kujali faida yetu binafsi. Utume kamwe hauwezi kuwa na malengo ya faida binafsi. Mtu anapokuambia ametoka utume, au anaenda utume ni vyema kuelewa kwamba anaenda kumenyeka, kutaabika na kujichosha kwa ajili ya wengine. Msukumu huu haupaswi usukumwe na ufahamu au vigezo vya wale tunaowahudumia, ila kwa kila tunayemuhudumia bila kujali anatujua au la.

Hivyo leo Mama Kanisa anavyosherehekea siku ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, anasadifu ukweli huu, yaani watu hawa walikuwa ni MAJITU YA SIFA, katika maana ya kwamba waliyatoa maisha yao bila kujibakiza pasipo woga wowote. Ingawa sitazama sana katika wasifu wa Petro na Paulo Mitume, ila historia ya maisha yao inaonyesha jambo hili. Petro anajulikana zaidi kama kiongozi na mwakilishi wa Kristo katika kundi la wale wa mwaminio Kristo na kuyaishi maagizo yake. Paulo anasimama kama mmisionari shupavu aliyeyafanya yote ndani na kwa ajili ya Kristo. Hivyo leo Kanisa linasheherekea zawadi ya maisha yao katika kutenda na kulisimamie lile alilolianzisha na kuliacha Kristo, na kulipeleka duniani kote kama Kanisa la kimisioni.

Ni wazi watu hawa wawili yaani Petro na Paulo wanayafanya mambo haya makubwa katika maisha yao kwanza kwa kujitambua wao wenyewe, na pili kuishi utambuzi huo katika kukutana na Kristo kila siku. Ukomvu wao wa Imani ni matokea ya kumtaabikia Kristo kila siku katika kuutoa ushuhuda wa kweli. Somo la kwanza linaeleza kwa undani ni kwa namna gani Petro aliutoa ushuhuda huo bila woga. Mwisho anasema maneno haya baada ya kutoka gerezani kwa miujiza. “Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi,” Mdo 12:11. Ufahamu huu kwa Petro hauna tena shaka juu ya kile anachokiamini.

Injili ya leo kwa namna nyingine inatupa wasifu wa Petro kwa undani na kutuelekeza nini hasa maana ya kiti chake na nafasi yake kati ya Mitume. Mtume Petro ndiye pekee aliyejibu swali ya Yesu kwa ufasaha, licha kwamba kwa mujibu wa Yesu jibu lile ni ufunuo kutoka kwa Mungu. Yesu anapowauliza wanafunzi wake, Je, watu wanasema kuwa mimi ni nani, Petro anajibu baada ya ukimya mkuu: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16. Yesu anaridhika na jibu hili, na hapo hapo anamnyenyekesha Petro kwa kusema, “Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17. Ufahamu huu wa Petro, na kufunuliwa huku kwa siri hii juu ya Kristo, kunamhesabia haki juu ya kiti kile alichokikalia hadi leo, Petro kama halifa wa kwanza, na Mababa watakatifu waliomfuata kama maalifa wa Kristo. Yesu mwenyewe anaweka kiti hiki rasmi kwa kusema, “wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18. Wapendwa, Kanisa letu linamisingi yake. Moja ya misingi yake hiyo ni uongozi Imara usio wa yumbishwa.

Wapendwa, baada ya kuwekwa rasmi kiti hicho kama alama ya uongozi imara kichungaji, anayekalia kiti hicho anapewa mamlaka kamili juu ya wale watakao kuwa chini ya uongozi huo. Yesu anayatoa mamlaka hayo kwa kusema, Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16.19. Kwa kupitia kiti na mamlaka haya, Kanisa linakuwa rasmi chombo cha msamaha na huruma ya Mungu. Kanisa pia linapewa mamlaka ya kufundisha, kuonya, kukataza na hata kufungia yale yanayoenda kinyume cha Imani na ufuasi wa Kristo.

Ndugu yangu, chuma kinapoitwa “Iron Still,” kimepita katika moja mkali sana. Uimara wa chuma hiki ni tokeo la chuma hicho kuvumilia joto hilo kali bila kupoteza uhasilia wake. Mitume, na hasa Petro na Paulo ambao leo Mama Kanisa anawasherekea, walitaabika vya kutosha kuhusu jina la Yesu. Somo la Pili linaeleza kwa undani mahangaiko na taabu alizozipata Mtume Paulo. Mtume Paulo anasema kama ni vita ameishinda na mwendo ameumaliza. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7. Faida kubwa aliyoipata katika utume wake huo wa pekee ni kuilinda Imani ambayo si kwa faida yake mwenyewe, bali kwa Kanisa zima. Msingi wa maisha ya Mtume Paulo ni kauli mbiu yake hii: “kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.” Flp 1:21. Hii ni hatua ya juu kabisa kwa mfuasi wa Kristo. Hapa ni kuishi kile unachokiamini na kukubali kuyapata yote kutokana na imani hiyo.

Wapendwa wana wa Mungu, hatua aliyoifikia mtume Paulo ni hatua ya kutokutishika na jambo lolote. Ni hatua ya kuishinda hofu na kuukumbatia uzima wa milele ingawa tunajua wote lazima tutakufa. Ni kujiachia katika mikoni ya Kristo, na kuacha yeye atende kadiri apendavyo. Ni kutokuwa na shaka yoyote juu ya: sababu ya kuja kwake Yesu Kristo kwetu, kuteseka kwake, kusulubiwa kwake, kifo chake na ufufuko wake. Mtume Paulo analiweka fumbo hili kwa maneno haya: Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18. Je, ninaweza kuyatamka maneno haya bila hofu yoyote ninapokabiliwa na changamoto za maisha yangu ya kila siku? Ndugu yangu Utume si lelemama, bali kuvumilia hadi ushindi wa milele.

Tumsifu Yesu Kristo!


WATAKATIFU PETRO NA PAULO MITUME, MTUOMBEE. AMINA.

No hay comentarios:

Publicar un comentario