JUMATANO WIKI YA 12 YA MWAKA-B
24/6/2015
Somo: Mwa 15:1-12, 17-18
Zab: 104:1-2, 3-4, 6-7, 8-9
Injili: Mt 7:15-20
Nukuu:
“Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda
zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri,
Mdameski?” Mwa 15:2
“Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali
atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi,” Mwa 15:4
“Kisha akamwambia, Mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa
Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi,” Mwa 15:7
“Jihadharini
na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa
ndani ni mbwa-mwitu wakali,” Mt 7:15
“Vivyo
hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya,”
Mt 7:17
“Mti
mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri,” Mt
7:18
“Kila mti
usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni,” Mt 7:19
TAFAKARI: “Kila mti mwema
huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kila kiumbe hapa duniani na zaidi binadamu, anakilio chake au
kiu yake ndani ya moyo wake. Ni kweli kila kukichwa husukumwa na kiu hiyo
lakini mwisho wa siku hujisalimisha katika hali fulani, au kitu fulani ili hali
tupate jibu la kiu hiyo. Hofu hutujia tungali bado kupata jibu la kiu yetu
kunakotokana na mambo mengine katika maisha kutokubaki kama yalivyo, bali nayo
hubadilika kadiri siku zinavyokwenda. Umri ni mojawapo ya mambo yasiyobaki kama
yalivyo, na hivyo ujeuka kuwa tishio na hofu katika subira yetu ya kile
tukitamanicho ila bado kukipata.
Abramu kiu
yake kubwa ni kumpata mtoto wake wa kumzaa na awe mrithi wake. Bila shaka hiyo
ndiyo kiu yake tangu ujana wake. Abramu inamlazimu kujisalimisha kwa Mungu ili
kupata jibu la kiu yake. “Abramu akasema, Ee
Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki
nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski?” Mwa
15:2. Anajisalimisha kutokana na uhusiano wake na Mungu
ulivyokuwa wa karibu. Ni kweli kwamba kujisalimisha kwetu hakuwezi kuwa mbali
na mazingira yetu na hali ya maisha yetu ya kila siku. Abramu kujisalimisha
kwake kwa Mungu ni matokea ya uhusiano wake na Mungu uliojenga dira mzima ya
maisha yake.
Jibu la
Mungu haliwezi kuwa tofauti na uhusiano wetu naye. Mara nyingi kuna hali tu ya
kucheleweshewa ombi letu. Kwa Mungu muda na nyakati si kitu kwake kwa sababu
yeye ni alfa na omega/mwanzo na mwisho. Kwa upande wetu binadamu, muda
unatugusa kwa sababu kuishi kwetu hata duniani ni kwa kipindi fulani tu. Kwa
hiyo muda wako ni uhai wako. Unavyopoteza muda wako bure ndivyo hivyo hivyo upotezavyo
uhai wako. Kwa kuyaona mahangaiko ya Abramu, Mungu anamjibu. “Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu
hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi,” Mwa
15:4. Kiu ya moyo wake Abramu inapata jibu. Mahusiano ya mtindo huu; Abramu na
Mungu ni mahusiano ya kimaagano. Hivyo Abramu anafanya agano na Mungu, na
anamtolea sadaka ya kuteketezwa. Huu ni uthibitisho wa kutokusalitiana, na pia
kubaki katika uhusiano wa kudumu. Naye Mungu anabariki agano lile na kusema,
“Mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili
uirithi,” Mwa 15:7.
Kinachotushinda wengi ni kulishika agano kiaminifu. Maisha
yetu kwa asilimia kubwa ni maisha ya kiagano hata kama hatutoi sadaka za
kuteketezwa, na kwa uelewa zaidi Kristo ndiye kikomo cha sadaka zote za
kuteketezwa kwa sadaka yake ya pale msalabani (Ebr 10:11-13). Uhusiano wa
Abramu na Mungu, ni uhusiano uliojijenga katika msingi wa Imani na Wema wa kweli. Matokea ya uhusiano
wa mtindo huu huwa mema pia. Mungu kamwe hawatupi visogo wanaomcha na
kumtumainia kila siku. Kuchelewa kwetu kutokupata kwa wakati kile tuombacho ni
mpango wa Mungu, kwani wakati ufahao hutupatia mara moja na kwayo hutosha kabisa.
Katika injili, Yesu anatufundisha hali ya uhusiano wetu na Mungu
ipasavyo kuwa. Kitu cha kwanza kabisa katika nyakati zetu, Yesu anatuwasa, kwa
kusema, “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi
ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali,” Mt 7:15. Watu hawa waongo
si kwenye nyanja tu za Imani/kidini, bali hata kwenye nyanja za kijamii. Maneno
haya ya Yesu yanaujumbe mahususi hasa kwetu Watanzania tunapoelekea kwenye
uchaguzi Mkuu kwaka huu. Je, tutawajuaje? Tuwapima kwa matendo yao kwa sababu,
“kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya,” Mt
7:17. Kama historia yake imetawaliwa na wema na hofu ya Mungu, basi kile
atuambiacho kitakuwa na mashiko. “Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala
mti mwovu kuzaa matunda mazuri,” Mt 7:18.
Mara zote mtu hutoa kile alichokuwa nacho. Huwezi kutoa kile usichokuwa nacho.
Ni kwa mantiki hii ya
kutoa kile ulichonacho ndivyo kila mmoja wetu kaitwa kwa namna ya pekee kuishi
wito wake hapa duniani. Ni katika kuishi hiki ulicho kwa ukamilifu na uaminifu
wake kutakakompendeza Mungu. Tendo hilo litakuwa sababu ya neema zake kwako ili
ufikie taji lile alilokuandalia yaani utakatifu wako. Kama wewe ni mlei,
hulazimiki kuishi maisha ya kitawa au ukleri ili ufikie taji hili. Kaa pale
ulipo kwa uaminifu, na hapo ndipo utakapo kutana naye. Hiyo ndiyo Galilaya yako
(Mk 16:7). Kila mmoja wetu akae nafasi yake kwa uaminifu na hapo ndipo
tutakapokutana naye. Maneno haya ya Yesu ‘mti mwema hauwezi kuzaa matunda
mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri,’ yanatuashiria hukumu yetu ya mwisho.
Kwa kuishi kwetu hapa duniani kila mmoja wetu lazima “awe zaidi.” Haupo hapa
duniani kwa bahati mbaya. Yakupasa kuwa zaidi pale ulipo kadiri ya wito wako.
Usipokuwa zaidi katika mema ujue kifuatacho ni kuhukumiwa milele. “Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni,” Mt 7:19.
Je, wasubiri hali hiyo ikufike?
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU TUJALIE TUZAE MATUNDA MEMA KILA SIKU KADIRI YA WITO WETU. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario