jueves, 11 de junio de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 10 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 10 YA MWAKA-B
12/6/2015
Somo: 2Kor 4:7-15
Zab: 115:10-11, 15-16, 17-18
Injili: Mt 5:27-32
Nukuu:
Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu,” 2Kor 4:7

Siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu,” 2Kor 4:10

Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti,” 2Kor 4:11

“Tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi,” 2Kor 4:14

Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake,” Mt 5:27-28

TAFAKARI: “Tu vyombo vya udongo.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa namna ya pekee masomo yetu mawili yanamlenga binadamu katika uwezo wake na mapungufu yake. Uwezo wa binadamu utiwa nguvu na kusimama imara endapo kutakuwa na muunganiko wa kweli na wa haki kati yake na Muumba. Muunganiko huu msingi wake mkubwa ni kujitambua kwake huyu mwanadamu kunakolenga kuweka wazi mafanikio yake, na udhaifu wake. Msingi huu unawezekana kujengwa tu pale ambako binadamu huyu atakubali kujinyenyekeza. Hivyo unapojinyenyeza unafungua ufahamu mwingine wa kujiona kama ulivyo, na si kama watu wasemavyo ulivyo, au mazingira yako unayoishi yanavyokuelekeza na kukutafsiri. Huku ndiko kujitambua kama “u chombo cha udongo.”

Ndugu yangu, ni pale tu unapojitambua kama u chombo cha udongo ndipo zile hazina zilizojificha, mathalani vipaji vyako hujidhihirisha. Ni wakati wa kuishi kile ulicho katika ukweli wake. Tulio wengi hatuishi kile tulicho, bali twaishi vivuli vya wengine. Tunajivika vinyago vya wengine na mwisho wa siku tunabakia kuwa vituko tu. Moja ya sababu kubwa ya watu wengi kutokuwa na furaha ya kweli ndani yao ni kwamba hawajawahi kuishi kile walicho hata mara moja. Hupenda kuwa kama mtu fulani muda wote. Unapoikataa nafsi yako, unajikataa wewe mwenyewe. Je, ni kwa namna gani unaweza kuwa na furaha ya kweli katika mazingira kama haya? Ni lini basi utavijua vipaji na karama zako kama hukuwahi kuwa kile alichokuumba Mungu? Utawezaje basi kuvithamini vipaji vya wengine kama vyako huvijui? Hivyo, Mtume Paulo anatukumbusha jamba hili, na kusema, Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu,” 2Kor 4:7

Ni katika kujiona kama vyombo vya udongo twaweza kuyakabili yote katika maisha na kuyachukulia bila woga kwa sababu tunajua anayetuimarisha na kutupa nguvu, ni Kristo mwenyewe. Ni kwa sababu hii kwamba, Siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu,” 2Kor 4:10. Hatuna hofu ya kufa wala kupata mateso kwa sababu mwenye nguvu na mamlaka ya mwili na roho ni Mungu mwenyewe, na kwa hali ya kibinadamu twa mtazama Kristo, neno aliyefanyika mwili akakaa kwetu. Hivyo Yesu anatutia nguvu na kutufanya imara kwa neno hili, “msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum,” Mt 10:28. Nani kama Mungu? Wapo wengi sana leo tunaishi kwa hofu, tena wakati mwingine hofu ya kurogwa na tunapoteza wakati mwingi kuhangaika kwa waganga na kupoteza rasilimali nyingi sana kupitia mlango huu wa shetani. Je, lipi lililo la heshima na baraka kwako; kufa mikononi mwa Kristo, au kufa mikononi mwa mganga wa kienyeji? Mtume Paulo anasema, kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti,” 2Kor 4:11. Hii ndiyo heshima kubwa kwa Mkristo kama mfuasi wa Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, ndani na katika Kristo ndiko kwenye uhakika wa kweli kwa sababu pamoja na kuyaonja mauti, Kristo yu hai milele. Je, hizo hirizi unazozivaa, na hayo mazindiko uliyochimbia kwenye kuta za nyumba yako yanausalama zaidi ya usalama ndani na katika Kristo? Ndugu yangu, “tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi,” 2Kor 4:14. Uzima wa kweli upo kwa Kristo tu, na si vinginevyo. Ni vyema kuanzia leo ukafuta kabisa ziara zako lizo rasmi na zisizo rasmi kwa waganga wa kienyeji. Safari hizo sinakukosesha neema na uzima wa Mungu na kujivunia wingi wa laama.

Kujitambua kama chombo cha udongo kutakuweka macho kutokudondoka katika dhambi kirahisi. Na hata baada ya kudondoka katika dhambi unyenyekevu huu kama chombo cha udongo utakufanya ufanye toba ya kweli na kurudisha uhusiano wako na Mungu. Kwa upande mwingine kujitambua kama chombo cha udongo kutakufanya uzame zaidi ndani kuhusu uzito wa dhambi na hathari zake. Kumbe dhambi haihesabiki tu kwa kufanya tendo halisi, bali hata kwa kuwaza na kuvutwa kwa hisia ya kufanya dhambi hiyo. Mizania ya dhambi ipo sawa kwa kufanya au kutokufanya ili hali tu tamaa ile ya kufanya jambo hilo ipo ndani yako. Kilichokosekana hapo ni mazingira halisi ya kulitenda jambo hilo, ila uzito wa dhambi ni ule ule. Tafsiri hii ya dhambi inatupeleka mbali zaidi na kututoa katika mtazamo wa kizamani wa kusema kuna dhambi ndogo na kubwa. Yesu anatupa angalisho katika jambo hili: Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake,” Mt 5:27-28. Je, si yale yamtokayo mtu moyoni mwake ndiyo yamtiayo unajisi? Je, si ndani ya moyo wa mtu ndipo kwenye vyanzo vya yale yote yamjazayo mtu na kumfanya kile alicho?

Wapendwa wana wa Mungu, “Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni? Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi,” Mt 15:17-18.

Tumsifu Yesu Kristo!


TU VYOMBO VYA UDONGO ILI  ADHAMA  KUU YA UWEZO IWE YA MUNGU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario