ALHAMISI
WIKI YA 10 YA MWAKA-B
11/6/2015
Somo:
2 Kor 3:15-4:1, 3-6
Zab:
84:9ab-10, 11-12, 13-14
Injili:
Mt 5:20-26
Nukuu:
“Basi ndiye Roho; walakini alipo Roho wa
Bwana, hapo ndipo penye uhuru,” 2Kor 3:17
“Kwa
maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe
kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu,” 2Kor 4:5
“Maana
nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo,
hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:20
“Basi
ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno
juu yako, iache
sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha
urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23
“Patana
na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka
kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani,” Mt 5:25
TAFAKARI:
“Patana na ndugu yako uwapo pamoja naye njiani”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni jambo la kawaida kuona ndugu wanagombana na mwisho wa siku wanaweka kando
tofauti zao na kuwa kitu kimoja. Hapa sina maana ya kuchochea ugomvi nikijua
kunakupatana, la hasha! Ninachosema ni kwamba ikitokea ndugu mmepishana kauli
si jambo jema mkaendelea kuzibeba tofauti zenu. Ukweli ni kwamba hata kama
umekosewa katika tofauti zenu, hakuna mshindi katika ugomvi huo kila mmoja
akibaki na tofauti zake. Ushindi wa kweli na wa roho ni kuchukua hatua na
kutafuta upatanisho hata kama wewe ndiwe uliyekosewa haki.
Ndugu yangu
tunayesafiri wote katika tafakari hii, usikubali hata mara moja kumbeba yeyote
katika moyo wako hasa kwa sintofahamu zilizotokana na ugomvi wenu. Kwa kukubali
kuishi kwa mtindo huo ni sawa na kuuza uhuru wako na kujifungia katika chumba
kidogo sana na kushindwa kutoka ili hali funguo za chumba hicho unazo wenyewe.
Usijitengenezee gereza lako mwenyewe pasipo sababu. Roho wa Mungu uliyepewe
bure na kufanya makazi ndani yako unamtesa na hapo hapo unakosa neema. Toka
kwenye kifungo hicho na uwe huru, na hapo roho wa bwana atakuwa nawe na
kukupatia wingi wa neema zake. Ndugu yangu, “alipo
Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru,” 2Kor 3:17
Wapo wengi kati yetu
huwa wanajisifu kwa kutoshiriki masakramenti kwa kumkomesha ndugu yake au
jirani yake aliyemkosea. Utamsikia anasema kwa kujivuna, “nina mwaka mmoja na
nuru si pokei Ekaristi Takatifu kwa kumkomesha kwa sababu sina muda wa kupoteza
kwa kuongea naye.” Je, jambo hilo kwako ni habari njema? Ndugu yangu, huko
ndiko kujihubiria mwenyewe habari za kuzimu. Kwa nini unajijengea jehenamu yako
mwenyewe, tena kwa kupenda? Mtume Paulo anasema, “Kwa
maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe
kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu,” 2Kor 4:5. Yafanye maisha yako kuwa
habari njema ya wokovu kila mahali uendapo na kuishi na watu. Yafanye maisha
yako kuwa barua ya kusomwa na watu ili kwa kupitia kwako wamwone Kristo. “Ninyi
ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu
wote; mnadhihirishwa kwamba
mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho
wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo
ya nyama,” 2Kor 3:2-3.
Ndugu yangu, wapo wengi
pia kati yetu ni mabingwa sana wa sura mbili mbili. Nachokata kusema ni kwamba,
wapo tunaoshiriki nao katika jumuiya ndogondogo, Kanisani, hata maisha yetu
utawani ambao muda wote humebeba zigo kubwa la chuki, visasi, hasira, wivu,
majivuno, na yale yote yanayofanana na haya na yasiyompendeza Mungu. Licha ya zigo hili kuulemea Moyo, hatupo tayari kuliweka
chini. Kukiwa kwenye sehemu za Ibadi huwa tunaliacha zigo hili mlangoni, na
mara baada ya Ibada zigo hili tunalikimbilia na kujitwisha na mara kunaondoka
nalo. Tupo tayari kulibeba zigo hili nyakati zote za majira ya mwaka, na ya
Vipindi vyote vya Liturjia vya Mama Kanisa. Leo Yesu anatupa angalisho: “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo
haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,”
Mt 5:20. Mbele za watu na jumuiya tunazoishi twajionyesha sisi ni wema na
hatuna tatizo na mtu, na wakati mwingine twa tamani hata kwenda mbinguni kwa
miguu yetu tukithibitisha utakatifu wetu machoni pa watu.
Wapendwa
wana wa Mungu, ukitaka sala yako, na maombi yako yapate kibali mbele ya Mungu,
jipatanishe wewe mwenyewe, wewe na uliyekosana naye, na pia wewe na Mungu.
Hivyo “basi ukileta sadaka yako
madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,
iache sadaka yako mbele
ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe
sadaka yako,” Mt 5:23. Wengi na hasa wale tuliokosewa hupenda kuyarefusha mambo
sana, na wakati mwingine tungependa tunyunyuziwe ubani kwa cheteso cha dhahabu
ili tuwe tayari kwa kuyaongelea yale yaliyotutatiza.
Jambo
la muhumu kupita yote kama umekosana na ndugu yako au ye yote yule, patana naye
mngali injiani. Maana yake nini? Kupatana na ndugu yako mngali njiani ni
kufanya juu chini kupatana na ndugu yako angali yu hai. Wengi tumeshuhudia watu
hawapendi kupatana na kuishia kuapizana pasipo sababu. Wapo wengine hata baada
ya kuzidiwa wakiwa kitandani karibu ya kufa wanapoomba upatanisho na ndugu yake
kunakuwa na mkwamo bila mwitikio wowote na mwisho mtu huyo hufariki katika hali
ya majonzi makubwa. Hivi unajisikiaje
ndugu yako kufa akikuomba upatane naye nawe kwa kiburi chako hukusikia na
hatimaye ndugu yako anafariki? Ndugu yangu, “Patana
na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije
akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani,” Mt
5:25. Je, kwa kutokupatana na ndugu yako angali hai, utajibu nini mbele ya
Kadhi-Mungu mwisho wa siku?
Tumsifu
Yesu Kristo!
Patana
na ndugu yako uwapo pamoja naye njiani
No hay comentarios:
Publicar un comentario