JUMAMOSI WIKI YA 11 YA MWAKA-B
20/6/2015
Somo: 2Kor 12:1-10
Zab: 33:8-9, 10-11, 12-13
Injili: Mt 6:24-34
Nukuu:
“Namjua
mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa
katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo
alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu,” 2Kor 12:2
“Kwa
habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu,
isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu,” 2Kor 12:2
“Na
makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa
mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita
kiasi,” 2Kor 12:7
“Naye
akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.
Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu
yangu,” 2Kor 12:9
“Kwa
hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa
ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu,” 2Kor 12:10
“Hakuna
mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda
huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na
mali,” Mt 6:24
“Bali
utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:33
“Basi
msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku
maovu yake.” Mt 6:34
Wapendwa wana wa
Mungu, leo katika tafakari hii niwaombe tusafiri wote katika neno hili: “Neema
yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.” Neema
inayozungumziwa hapa ni nguvu ya pekee, “The will power of God,” katika mambo
yale ambayo kwa ubinadamu wetu ni vigumu kuyapatia ufumbuzi wa kudumu na
waharaka. Sharti mojawapo la kupata Neema hii ya pekee ni kutambua kwa undani
udhaifu wako. Mfano: Serikali ya Tanzania inaongozwa na dola tokeo la Chama cha
Mapinduzi. Hiki ndicho chama tawala, na ndicho chama kinachoongoza dola la
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa upande wa maisha ya kiroho ndani mwetu
kuna “dhambi dola,” yaani dhambi tawala, au “udhaifu dola,” yaani udhaifu tawala.
Dhambi hii yawezekana kila mara uendapo kuungama ndiyo inayojitokeza, na hivyo
kufikia wakati ukaanza kujisikia kama kero fulani. Unapotambua udhaifu huu,
ndipo unapoongelea uhitaji wa neema ya pekee-“The will power of God,” kuishinda
dhambi hii tawala au udhaifu huo. Yawezekana dhambi dola, au tawala kwako ni
Kiburi, au majivuno, au umbea, au uasherati, au wivu, aka.
Ni katika sintofahamu
hii, Kristo ni kielelezo cha yote katika yote. Huyu ndiye Kristo Mfufuka mwenye
mamlaka yote mbinguni na duniani. Ndiye tunayepaswa kumfahamu, kufundishwa
naye, kumfuata, na kuishi kadiri ya maagizo yake. Hivyo Mtume Paulo katika
mwono huu anasema, “namjua mtu mmoja katika
Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui;
kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka
mbingu ya tatu,” 2Kor 12:2. Mtu huyu ndiye kwenye mamlaka ya kutuondoa kutoka
kwenye kifungo cha dhambi dola. Mara nitambuapo dhambi dola hii ndani mwangu,
na kumkumbatia Kristo katika usalama wangu, Kristo ndiye wakumsifia kwa sababu
kakubali kuubeba udhaifu wangu ili mimi niwe na afya ya roho na mwili. Huyu
ndiye wa kusifiwa kwa sababu kakubali kuwa masikini na kudharauliwa ili mimi
niwe tajiri na kuheshimiwa. “Kwa habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini
kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu,”
2Kor 12:2. Hatua hii katika maisha ya kiroho ni uthibitisho wa ukomavu.
Dhambi hii tawala au
dola, au uthaifu huu, hutunyenyekesha na kuanza kutubadilisha kuelekea ukamilifu.
Dhambi hii ndiyo Mtume Paulo anaisemelea kuwa ni MWIBA KATIA MWILI WAKE. “Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa
wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili
anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi,” 2Kor 12:7. Kutunyenyekesha huku ni
kutufanya tusijivune kupita kiasi, na hasa kuwanyooshea vidole wengine. Mfano:
Kama wewe ni Baba au Mama wa familia tazama familia yako na utatambua ndani
yake upo mwiba. Kwa mfano kwenye familia yenu mpo nane, atakuwepo mmoja ambaye
ni tofauti kabisa kimwelekeo na kitabia. Huyu ndiye mwiba wenu wa
kuwanyenyekesha katika, kusema, kutenda, kuishi, kuonya, kushauri, kukaribia,
na kuhukumu wengine. Hata kwenye familia zenye watawa au makleri, mwiba utufanya kuwa na adabu na kuchagua maneno ya
kusema mbele za watu. Mwiba huu utufanya tusijivune kupita kiasi. Je, kwenye
familia yenu, ukiachana na wewe mwenyewe hakuna mwiba?
Je, tufanyeje katika
hali hii? Je, tuikimbie aibu kwa kuwakana ndugu ambao katika familia zetu ndiyo
miiba? Je, kama hali hiyo ya mwiba, yaani udhaifu au dhambi tawala ndani yangu
niishi kama haupo? Ndugu zangu, kukimbia udhaifu si kuutafutia dawa. Hatua ya
kwanza tambua udhaifu wako. Hatua
ya pili, omba neema ya Mungu ya pekee, “The will power of God.” Na hatua ya tatu kamwe usibanduke ndani na
katika Kristo, kwa sababu yeye ndiye anayetosha katika udhaifu au dhambi
tawala. Mtume Paulo katika hali ya mahangaiko yake kuhusu mwiba wake,
alipomkumbatia Kristo bila kuwa na mashaka yoyote alipata jibu kutoka kwa
Kristo. Naye alimwambia, “Neema yangu
yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia
udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu,” 2Kor
12:9.
Hali
hii ya kuyapokea madhaifu yetu, na kuyaelekeza kuliko njia salama yaani kwa
Kristo, bingwa na tabibu wetu wa roho na mwili, ndiko udhaifu huu ubadilika na
kuwa nguvu ya kusonga mbele, nguvu na nuru kwa kuwafundisha wengine, nguvu ya
kusimama na kuongea bila kutafuana au
kumung’unya maneno, nguvu ya kutoa ushuhuda wa kweli ambao kwayo wengi
huongoka. Hivyo
Mtume Paulo anasema, “napendezwa
na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo.
Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu,” 2Kor 12:10. Tatizo kubwa tulilonalo
tulio wengi hupenda kuficha madhaifu yetu, na kuvaa vinyago ambavyo hutusitiri
tu kwa muda mfupi. Siku vinyago hivi vitakapochoka, ndipo tunakuwa gumzo la
mji, kwani Mungu hata mara moja hamfichi mnafiki. Mungu atakuumbua tu mchana
kweupeeee! Huku ndiko kuishi maisha ya kiroho kiundumelakuwili.
Yesu anatupa angalisho
na kusema, “hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa
maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau
huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24. Kutumikia mabwana wawili ni
kutokuutambua mwiba wako, au udhaifu wako. Hata ukifanikiwa ni kwa muda mfupi
tu. Je, kwa nini twapaswa kumtumikia bwana mmoja? Sababu ya wazi na ya moja kwa
moja ni kuondoa ile roho iliyojigawa vipande vipande. Mfano; kama umepata
mialiko miwili ya harusi inayofanyika muda ule ule na siku ile ile, yakupasa
kuchagua moja wapo utakayokwenda hata kama zote zina uzuri au zimetofautiana.
Kuchagua huku ndiko Yesu anapotushauri kuutafuta kwanza ufalme wa Mbinguni, na
kuondoa roho ya kujigawa vipande vipande. Naye Yesu anasema, “Bali
utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:33. Ndugu yangu, unaloneno zaidi ya ukweli huu wa
Bwana wetu Yesu Kristo?
Ni ukweli usiotia
shaka kwamba ukishaingia katika mfumo huu, na mtazamo huu wa fundisho hili ya
Yesu, kuutafuta ufalme wa mbinguni kwanza, huwezi kupata presha unapowaona watu
wakipigana vibega kwa kumwangaikia mfalme tumbo na utajiri wake. Kristo
anapokuwa katikati ya yote, yeye atakupatia kadiri ya mahitaji yako na kwa
wakati wake. “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia
yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” Mt 6:34. Ndugu yangu yatupasa kumuishi
Kristo leo na sasa katika yale yote yampendezayo. Ingawa kesho inasikikia
akilini mwetu, tuelewe kesho hiyo ipo mikono mwa Mungu katika uhalisia wake.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU, KWANGU WATOSHA. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario