sherehe ya moyo mtakatifu wa yesu
12/6/2015
somo
I: Hos 11:1b, 3-4, 8c-9
Zab:
Isa 12:2-6
Somo
II: Efe 3: 8-12, 14-19
Injili:
Yoh 19:31-37
Nukuu:
“Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo,”
Hos 11:4a
“Moyo
wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja,” Hos 11:8c
“Kwa
maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati
yenu; wala sitaingia ndani ya mji,” Hos 11:9bcd
“Kristo
akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu
pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao
ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu,”
Efe 3:17-19
“Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa,
hawakumvunja miguu; lakini
askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji,” Yoh
19:33-34
“Hapana
mfupa wake utakaovunjwa. Watamtazama yeye waliyemchoma,” Yoh 19:36b, 37b.
TAFAKARI:
“Yesu anakupenda upeo, amepoteza kila kitu, na kufa kifo cha aibu ili
asikupoteze.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa
anaadhimisha sherehe ya Moyo Mtakatifu Yesu. Ni wakati muhafaka wa kuyatafakari
mapendo yote ya Mungu kwa Mwanadamu tunavyoitazama safari nzima ya ukombozi wa
mwanadamu uliokamilishwa na tukio kubwa la sadaka ya Kristo pale Msalabani.
Moyo ni kielelezo, na ni alama ya upendo. Ni katika Moyo huu wa Yesu tunaona
mapendo yote ya Mungu. Ni katika Moyo wa
Yesu na hasa pale Msalabani pamoja ya
safari nzito na mateso mazito yakiambatana na karaha za kila aina njiani
kuelekea golgota, Moyo huu unafunguliwa kwa mkuki na yanatoka maji na damu.
Kwetu sisi kama wafuasi wake Kristo, Moyo wake Kristo u wazi kwa yeyote kuyaonya mapendo yake, na
pili kwa kutoka maji na damu, moyo huu ni chemchemi ya neema. Hivyo tutafakari
fumbo zima la sherehe hii kwa neno hili, “Yesu anakupenda upeo, amepoteza kila
kitu, na kufa kifo cha aibu ili asikupoteze.”
Wapendwa wana wa Mungu,
neno “upendo,” “mapendo,”au “nakupenda,” si neno geni masikioni mwetu. Neno
hili tunalitumia sana, na wakati mwingi neno hili limepotoshwa na kupoteza
maana yake halisi. Kwa maana nyingine neno upendo ni moja ya maneno maarufu
sana yanayotumiwa na binadamu leo ambalo
maana yake halisi imekwisha “chakachuliwa.” Neno upendo leo linauhushiano wa
karibu sana na mahusiano ya “kimapenzi.” Kwa mantiki hii neno hili linapotamkwa
kwa wengine badala ya kuleta furaha na faraja kama ulivyo wazi moyo wa Yesu,
neno hili upendo linakuwa kitonesha maumivu ya ndani.
Upendo tunaosheherekea
leo Kikanisa ni upendo ule ulio tayari kujitoa bila kutumaini chochote, na
kujitoa bila kujibakiza. Haya ndiyo makusudi ya Mungu katika safari nzima ya
wokovu wetu na kukamilika katika Kristo Yesu. Hivyo, “hakuna aliye na upendo
mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” Huu ndiyo
upendo wa Yesu kwako na kwangu. Kwa kutupenda upeo hakujibakiza hata chembe. Hakuona
aibu kutenda yote kwa sababu yangu na yako, licha njia na mateso aliyoyapata
yalikuwa ya aibu sana.
Yesu alikubali
kudharauliwa kupita dharau zote, kwa kukupenda wewe na mimi. Na tazama bado
anatupenda, na anazidi kusema nakupenda kila tuutazamapo msalaba Mtakatifu,
akiwa ameinyoosha mikono yake; “nimeyapokea yote kwa kukupenda, na nimekufa kwa
kukupenda, ili nisikupoteze.” Rafiki yangu, sema asante Yesu kwa kunipenda mara
tatu! Asante Yesu kwa kunipenda, Asante Yesu kwa kunipenda, Asante Yesu kwa kunipenda.
Wapendwa wana wa Mungu,
jiulize ni mara ngapi nashindwa kuonyesha furaha na upendo huu kwa wengine? Je,
isingenilazimu kumshukuru Mungu kwa kila pumzi ninayoivuta? Je, uhai wangu leo
una maana yoyote bila upendo wa Kristo aliyenipenda upeo? Ni ukweli usipingika
kwamba kama binadamu twapenda kupenda na kupendwa. Hali hii ya kupenda na
kupendwa inapokolea na kujivika upofu, utuelekeza katika “upendo miliki,” na
“upendo nipe nikupe.” Haya siyo makusudio ya Mungu kwetu. Upendo wetu hatima
yake siyo kumilikishana, bali kuwekana huru katika kumpenda Mungu, kumjua
Mungu, kumtumikia Mungu, katika kulenga zaidi furaha ya kweli ndani na katika
muumba wetu na hasa mahusiano yetu na wengine. Kwa nyakati zote Mungu hakuchoka
kuonyesha upendo wa aina hii. “Naliwavuta
kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo,” Hos 11:4a
Ndugu
yangu, ni kweli kwamba yatupasa kupenda kadiri ya asili yetu, ubinadamu wetu,
ila upendo huu ufunue upendo ule wa Kimungu ndani yetu, kwa wenzetu, na
mazingira yetu. Upendo usiovuka mipaka ya umimi ni upendo usio na mwelekeo wa
Kimungu. Upendo usio na mwelekeo wa Kimungu ni upendo usio na ukomavu kiroho.
Ni upendo dhaifu. Ni moyo uliodumaa na usiokuwa na mabadiliko ya ndani. Mungu
anasema hivi kupitia Nabii Hosea, “Moyo
wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja,” Hos 11:8c. Jamii
yetu leo na hasa Taifa letu la Tanzania lisingekuwa kama lilivyo leo kama
upendo wetu na hasa viongozi wetu tuliowapa dhamana kutuongoza kama wangevuka
mipaka ya umimi.
Upendo
huu unaotupelekea kujifunua zaidi kwa
mapendo ya Kimungu, ndiyo unaomtambulisha Mungu katika mazingira yetu ya kila
siku. Mungu atabaki kuwa Mungu. “Kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi;
mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji,” Hos
11:9bcd. Ila kwa kuishi upendo wake nje ya mipaka yetu
ya umimi Mungu huyu huwa Immanuel, yaani Mungu pamoja nasi, na huyu ndiye
Kristo aliyejitoa sadaka kwa ajili yangu na wewe.
Ndugu
yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, hakuna aliyekutana na Kristo kiroho
akabaki kama alivyo kuwa mwanzo. Kukutana na Kristo kiroho ni kumruhusu Kristo
akufanye hai muda wote. Uhai wa Kristo ndani yako ndiyo msukumo wa kuyaona yote
kama Kristo kama aliyoyaona yeye. Mfano: namna yako ya kuwaona watu na mahitaji
yao utabadilika. Namna yako ya kuwaona wakosefu na hasa wewe mwenyewe
utabadilika. Namna yako ya kutoa hukumu kwako mwenyewe na kwa wengine
utabadilika. Hivyo, “Kristo
akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu
pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao
ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu,”
Efe 3:17-19. Huku ndiko kufanywa upya ndani na
katika Kristo.
Wapendwa
wana wa Mungu, Moyo Mtakatifu wa Yesu unaoleta uhai mpya ndani yetu ndiyo
furaha ya kweli. Na furaha ya kweli ni kama “kikohozi” huwezi ukakizuia.
Kufunguliwa kwa Moyo wa Yesu mkuki kulidhihirisha furaha hiyo ya Mungu
iliyokuwa ndani ya Moyo wa Yesu licha ya mateso yake pale msalabani. Moyo huu
tangu siku ile upo wazi wa ajili yako na yangu tunapokumbana na sintofahamu za
maisha. Hata pale tunapopata utulivu katika mahangaiko yetu ni vyema tukaenda
kupumzika mahali salama yaani ndani ya moyo huu wa Yesu. Tendo hili la Moyo wa
Yesu kuwa wazi ni utimilifu wa maneno yake mwenyewe Yesu aliposema; “Njoni
kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami
nitawapumzisha.” Mt 11:28. Utulivu wa kweli, upole wa kweli, na unyenyekevu wa
kweli unapatikana ndani ya Yesu. Yatupasa kujifunza wake kwani ni rahisi kwa
sababu njia na masharti yake ameshatufundisha na kutuonyesha. Ni kupenda kama
alivyotupenda sisi bila kujibakiza. Hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu, “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole
na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa
maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,” Mt 11:29-30.
Furaha
kama kikohozi huwezi kuificha ni pale
pia yalipotoka damu na maji, ikiwa ni chemchemi ya neema. Neema hizi
tunaendelea kuzipata ikiwa ni mwendelezo wa upendo wa kweli wa Kristo kwetu kwa
kupitia masakramenti yake. Je, unavikwazo juu ya chemchemi hizi na neema zake,
yaani, haya masakramenti? Kama jibu ni ndiyo, TAFAKARI NA CHUKUA HATUA.
Moyo
Mtakatifu Yesu Yesu, Utuombee.
Tumsifu
Yesu Kristo!
ASANTE
YESU KWA KUNIPENDA. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario