JUMATANO
WIKI YA 10 YA MWAKA-B
10/6/2015
Somo
2Kor 3:4-11
Zab:
98:5, 6, 7, 8, 9
Injili:
Mt 5:17-19
Nukuu:
"Si
kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali
utoshelevu wetu watoka kwa Mungu,” 2Kor 3:5
“Naye
ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa
roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha,” 2Kor 3:6
“Kwa
maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina
utukufu,” 2Kor 3:11
“Msidhani
ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali
kutimiliza,” Mt 5:17
“Basi
mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha
watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:19a
“Bali
mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa
mbinguni,” Mt 5:19b
TAFAKARI:
“Utoshelezo watu watoka kwa Mungu kupitia mwanaye Mpendwa Yesu Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo kwa undani tutafakari nini kitoshelezo cha mwanadamu. Ni vyema kujitazama
wenyewe kwanza kabla ya kumtazama mwanadamu na utoshelezo wake kwa ujumla. Je,
wajisikia kutoshelezeka kwa hali na namna unavyoishi? Kulijibu swali hili
itakupasa kuyachambua mambo haya yafuatayo; Sehemu ya kwanza jaribu kuyapitia
mambo yale yote yanayokupa furaha. Ukiwa bado umebaki katika hatua hii ya
kwanza kwa hayo mambo yanayokupa furaha, kila moja wapo ya hilo linalokupa
furaha lilinganishe na uzima wako wa milele. Jiulize swali hili: Je, kunauhusiano
wa moja kwa moja na maisha yako baada ya kifo, yaani umilele wa maisha yako?
Kama hakuna uhusiano wa moja kwa moja na uzima wako wa milele, je, mkwamo huo upo wapi? Kuchukua hatua katika
mkwamo huo, yakupasa kujiona kuwa una siku ya leo tu. Hatua hiyo utakayoichukua
iwe na uhusiano wa moja na uzima wako wa milele.
Sehemu ya pili ya
kutafakari utoshelezo wako jaribu kuyapitia mambo yale yote yasiyokupa furaha.
Na bado ukiwa katika mambo hayo, ni vema ukajiuliza swali hili; Je, mahangaiko
hayo yanautukufu mbele yake ukilinganisha na hali yako ya sasa na umilele wa maisha yako baada ya kifo? Kama
hayana, je, mkwamo wake upo wapi? Wapo wengi leo wanateseka kwa ajili ya
kuteseka, na mateso yao hayana utukufu na uhusiano wa moja kwa moja na umilele wao.
Mfano; kutamani nyumba nzuri ya ghorofa ya jirani yako na kutokulala usingizi
ukiikodolea macho usiku kucha, hakuta kuwezesha kuwa na nyumba kama hiyo kamwe
kama hutojishughulisha na jambo lolote
na ufanyi chochote kubadili hali hiyo. Ukweli ni kwamba, hakuna sababu la
kulalamika chumba kina giza wakati unashindwa kuwasha hata kijinga cha moto
kuleta hata mwanga kidogo katika chumba kile.
Wapendwa katika Kristo,
tunapoyatamani yale yaliyo nje ya uwezo wetu kama wanadamu twaweza kuyapata au
kuyafikia kama tumefanya vyema yale yaliyochini ya uwezo wetu kama binadamu.
Hapa ndipo ule msemo unapopata maana, yaani “Grace works on nature,”-“Neema
hufanya kazi katika mazingira asili,” na si vinginevyo. Ni kwa kulitambua jambo
hili, Mtume Paulo anatoa kauli hii yenye ukomavu wa Imani: "Si
kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali
utoshelevu wetu watoka kwa Mungu,” 2Kor 3:5.
Hii ndiyo neema ya Mungu inayotuwezesha kutoka pale tulipo na kwenda pale
alipo. Utoshelevu huu kutoka kwa Mungu haudondoki tu kama mana kule jangwani,
bali kwa kututaka pia tufanye yale yanayotuhusu kama wanadamu. “Aliye kuumba
wewe pasipo wewe, hawezi kukukomboa wewe pasipo wewe,” Mt. Augustino wa Hippo.
Je, hali ilikuwaje kabla ya Yesu Kristo na
wakati wake? Ni ukweli usiotia shaka kwamba uhusiano Kati ya mwanadamu na
Muumba wake ulioneka wa mbali sana, na tena wa kutisha. Mungu alionekana kama
mtoa adhamu za papo kwa papo, na wakati mwingine kutafsiriwa kama mpanga mtindo
fulani wa maisha ambao kwa upande wetu Binadamu hata tungejitahidi kwa namna
gani tusingeweza kujitoa katika hali hiyo.
Jambo la kushangaza zaidi wakati wa
Yesu, Torati ile ambayo ndiyo ilikuwa mstakabali wa Taifa la wana wa
Mungu-Waisraeli, ilikwisha chakachuliwa vya kutosha na hivyo Taifa hili
lilikuwa linafuata Tafsiri yake tu kwa sehemu kubwa. Jambo
muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu Wayahudi na hasa mafarisayo na
waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha
ya dini na matendo yake kupitia masimulizi) iliyojulikana kwa ujumla kama
TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka
Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)
Kwa mantiki hiyo hapo
juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa
350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed)
katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na
waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga
jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati. Ni ukweli wa
Mungu uliopotoshwa.
Yesu anasisitiza
kuishika na kuiishi Torati kama mafundisho ya kweli ya Mungu na makusudio yake,
anasema, "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati au manabii; la,
sikuja kutangua, bali kutimiza. Kwa maana, amini, nawaambia, Mpaka mbingu na
nchi zitakapoondoka, yadi moja wala nukta moja ya Torati haitaondoka, hata yote
yatimie," Mt 5:17-18.
Ukweli huu wa Torati
kama mafundisho na maagizo ya kweli ya Mungu waweza kuusoma pia katika sehemu
nyingine za injili kama ifuatavyo;
-Mt 7:12; 12:5; 22:40;
-Lk 2:22; 10:26; 16:16;
24:44
-Yoh 1:17; 1:45; 7:19;
7:49
Yesu ni ukweli na
amekuja kusimamia kweli ya Mungu akitambua ukweli huo utatuweka huru.
"Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno
langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo kweli
itawaweka huru," Yoh 8:31-32. Ni ukweli huu anaongelea Mtume Paulo ambao
utatutosheleza. “Naye ndiye
aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa
maana andiko huua, bali roho huhuisha,” 2Kor 3:6. Andiko hapa analolisema Mt.
Paulo ni ule uchakachuaji wa Torati niliosema hapa mwanzo. Yesu Kristo amekuja
kutuhuisha na ile kweli iliyokuwa tangu mwanzo, yaani Torati (mafundisho ya
kweli ya Mungu na makusudio yake katika kumkomboa mwanadamu).
Ndugu yangu uliyesafiri
nami katika tafakari hii, fanya tafiti moyo na uone ni mambo gani yanayokupa
utoshelevu wa kweli ndani yako. La
sivyo, maisha yako kama mfuasi wa Kristo
yatakuwa kama mchezaji ngumu bora
anayetupa makonde yake kwenye hewani mwanzo hadi mwisho wa ngumi. Je, hapa kuna
ushindi? Kama tunataka ushindi, yaani, utoshelevu wa kweli ndani yetu, lazima
utoke kwa Mungu, na kupitia kwa Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Kwani, “amwaminiye
Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya
Mungu inamkalia,” Yoh 3:36
Tumsifu Yesu Kristo!
YESU KRISTO NDIYE UTOSHELEVU WETU WA
KWELI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario