miércoles, 3 de junio de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI 9 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI 9 YA MWAKA-B
4/6/2015
Somo: Tob 6:10-11a; 7:1, 9-17; 8:4-10
Zab: 128:1-2, 3, 4-5
Injili: 12:28b-34
Nukuu:
            “Inuka, dada, tumwombe Bwana atuonee huruma na kutukinga salama.” Tob 8:4b
nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:30-31

“Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu,” Mk 12:34b

TAFAKARI: “Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tujikumbushe katekesi yetu, na hasa nini sababu ya kuumbwa kwetu? Bila kukukosea, tumeumbwa ili tumjue, tumpende, tumtumikie, na mwisho turudi kwake mbinguni. Hii ndiyo sababu kubwa ya kuumbwa kwetu. Kwa maana nyingine hatupo katika ulimengu huu kwa bahati mbaya. Tupo katika ulimengu huu kwa malengo: Tumjue aliyetuumba na makusudi yake, tumpende kwa sababu katupenda yeye kwanza, tumtumikie kwa mapaji yote aliyotujalia, na baada ya kuyafanya  haya yote kwa uaminifu turudi kwake mbinguni kwenye umilele.
Wapendwa twaweza kuyafanya hayo yote kama ndani mwetu tunayo hofu ya Mungu. Hofu ya Mungu ndani mwetu ni ule msukumo wa kuyafanya yale yote yampendezayo Mungu. Tunayafanya haya si kama watumwa kwa hofu ya Mtwana, bali kwa sababu tu wana na warithi wa ufalme wa Mungu. Twawajibika kuyafanya haya kutokana na wadhifa wetu mbele ya Mungu-waana wa Mungu. Hofu hii ya Mungu ndicho kinachoyasukuma maisha mapya ya ndoa kati ya Tobia na Sara. Tobia anamuwasa mke wake, na kusema, “Inuka, dada, tumwombe Bwana atuonee huruma na kutukinga salama.” Tob 8:4b
Injili ya leo inatupa sababu kuu mbili za kuumbwa kwetu. Sababu hizi ni amri, kwa maana yake hakuna uchaguzi wa kufanya au kutokufanya. Yatupasa kulitenda hilo na kulifanya kuwa ndiyo tabia yetu kama wana wa Mungu. Yesu anapoulizwa ni amri ipi iliyokuwa kubwa kulizo zote, anajibu kwa ufupi uliyobeba mstakabadhi mzima wa maisha ya mwanadamu. Mjumuhisho huo wa pamoja ni hivi: nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:30-31
Sehemu ya kwanza ya amri hii imebeba  lengo la kuumbwa kwetu na kuwa hapa duniani, yaani “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.” Sehemu ya pili inatutaka tutambue, na kumpenda jirani zetu. Je, jirani yako ni nani? Jirani kwa mwono halisi wa Imani yetu kama Wakristo, imevuka mipaka ile ya kimazingira. Kwa maana hiyo jirani yangu ni yeyote yule mwenye uitaji (rejea Msamaria mwema Lk 10:33).
Je, hali ndivyo ilivyo kwenye mazingira yetu ya leo Tanzania? Leo inapotokea ajali badala ya kupata msaada ndiyo kwanza wanakumalizia kabisa. Tumefikia mahali hata tunazivua maiti nguo. Huku ni kukosa kabisa hofu ya Mungu na kuwa mbali na ufalme wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUWEZESHE KUWAFIKIA WOTE TUNAOKUTANA NAO. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario