JUMANNE WIKI YA 9 YA MWAKA-B
2/6/2015
Somo: Tob 2:9-14
Zab: 111:1-2, 7-8, 9
Injili: Mk 12:13-17
Nukuu:
“Niliwaendea waganga mbalimbali, lakini
hakuna aliyeweza kuniponya; mwisho nikawa kipofu kabisa. Kwa miaka minne
sikuweza kuona chochote,” Tob 2:10cd
“Hata
walipofika walimwambia, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala
hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli
waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo?” Mk 12:14
“Yesu
akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni
Mungu. Wakamstaajabia sana,” Mk 12:17
TAFAKARI: “Hata katika
majiribu tusiyoyajua tusimame katika Imani na kweli, na tutende haki daima.”
Wapendwa
wana wa Mungu, majaribu licha ya kwamba ni changamoto kubwa katika maisha ya
binadamu, hasa hasa pale mwanadamu huyo anapokutana na sintofahamu zilizozidi
uwezo wake, majaribu hayo kwa maisha ya kiroho huwa kipimo cha ukomavu wa
Imani. Tunapotafakari kupatwa kwa upofu Tobiti, na Yesu kuwataka wampe Kaisari
yaliyo yake Kaisari, ni vyema tulitafakari neno hili; “hata katika majaribu
tusiyoyajua tusimame katika Imani na kweli, na tutende haki daima.”
Tobiti
anakutwa na upofu siku moja jioni akiwa amejilaza uani mwake bila kujifunika
kwa sababu kulikuwa na joto. Tendo hili ni la kawaida sana kulifanya hasa ndugu
zetu wa pwani na mazingira yale yenye hali ya joto kwa muda mrefu. Jambo la
ajabu ni kile kilichofanywa na ndege yule tuliyemzoea, mbayumbayu. Ndege huyu
anamnyea vitu machoni mwake na hivyo Tobiti anapatwa na upofu. Upofu huu
unamjia kama ndoto na inakuwa ndio ukweli.
Katika
hali ya kibinadamu ni vigumu kupokea ukweli huu hasa tunapotazama mazingira ya
kutokea jambo hili. Kwa jamii yetu ya Tanzania tendo hili ni rahisi sana
kulihusisha na maswala ya Kishirikiana. Watu wetu leo husukumwa na kuamini sana
mambo haya ambayo kisayansi ni vigumu kuyahakiki au kuyathibitisha. Hatuachi
kusema hapa kuna mkono wa mtu. Mahangaiko ya Tobiti ni makubwa sana kama
anavyosema, “Niliwaendea waganga mbalimbali, lakini hakuna
aliyeweza kuniponya; mwisho nikawa kipofu kabisa. Kwa miaka minne sikuweza
kuona chochote,” Tob 2:10cd. Kauli hii ya Tobiti ni hatua ya nne kati ya hatua
tano za kifo.
Wapendwa, ni vyema kuzijua hatua hizi tano
za kifo ili tujue kama kweli katika mahangaiko yetu katika hali ya sintofahamu
kama tunasafiri na Mungu na katika Imani iliyokweli. Hatua ya kwanza ya kifo ni
hali ya ‘KUTOKUJALI’ mara upatapo jambo au kuhisi kitu fulani kisichokuwa cha
kawaida. Nitachukuwa mfano wa ‘hisi’ ya ugonjwa wa malaria ili tusafiri wote
katika tafakari hii. Kutokujali huku ni pale tunapojisikia mwili wetu haupo
vizuri, hata hivyo tunaendelea kufanya shughuli zetu za kila siku.
Hatua ya pili ya kifo, ni ile hali ya
mshituko ambayo hapa tutaipa jina la ‘YAWEZEKANA.’ Hatua hii ni pale tunapoanza
kupingana na dhamiri na kuanza kujihoji na kusema, “sijui nikapime malaria au la,
yaonekana nina malaria. Ngoja niangalie hadi kesho nione hali itakuaje.” Hii ni
hatua ya pili ya kifo.
Hatua ya tatu ya kifo ni kuchukua ‘HATUA.’
Walio wengi hujipeleka sehemu husika na kufanya uchunguzi kwa yale
yanayotusibu. Hapa ni pale unapochukua hatua madhubuti na kwenda kupima malaria
hayo na kujua ukweli wa kile kinachokusumbua hasa ni nini. Wakati mwingine
hatua hii wengine upeleka kwenye tafiti hizi na kujua kinachotusumbua kwa
sababu uzidiwa na hali hii ya ugonjwa. Hii ni hatua ya tatu ya kifo.
Hatua ya nne ya kifo ni kukata ‘TAMAA.’
Hatua hii mara nyingi mgonjwa ukosa imani ya dawa anazozitumia kwa sababu haoni
mabadiliko, wauguzi wanaomuhudumia, na hata ndugu wanaomuhudumia. Hatua hii ya
kifo ni mbaya sana kwa sababu huanza kutuondoa katika Imani tuliyokuwa nayo
mwanzo, na kuanza kupapasa papasa sehemu nyingine. Hapa ndipo tunapoona watu
wangiangaika kwa kubahatisha tiba. Kama ni familia utakuta wengine wanachanja
mbuga kwa waganga wa kienyeji, na wengine kwanye nyumba za uponyaji ili mradi mtu
apone. Mtu anayefikia katika hatua hii anahitaji mtu wa kumpa ushauri nasaha.
Hatua hii ya kifo tusipopata utulivu wa ndani na kuyakubali na kuyapokea
mahangaiko tunayoyapata, utufanya kupoteza yote tuliyokwisha jijengea kiimani.
Ushauri nasaha ni Muhimu sana kuiokoa roho hii wakati huu. Wengi ukubwa na
umauti haraka kwa kujawa hofu.
Hatua ya tano na ya mwishi ni
‘KUJISALIMISHA.’ Ni watu wachache sana uifikia hatua hii ya tano ya kifo. Wengi
huishia hatua ya tatu na ya nne. Kujisalimisha katika hatua hii ni matokeo ya
majibu mazuri ya ushauri nasaha. Mtu anapotambua ukweli wa kile kinachomsumbua
hata kama kiuhalisia bado amefichwa ukweli huo na kuwa fumbo, kuikubali hali ya
mateso hayo ni hatua muhimu sana ya kukipokea kifo ambacho ndiyo mlango
uliobaki kuelekea kule tuliko haidiwa na Kristo mwenyewe.
Kujisalimisha huku ni kusema pamoja na
Kristo, “Ee baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Lk 23:46. Hakika tukiweza
kuyatamka maneno haya na Kristo katika mateso yetu yasiyokuwa na majibu rahisi
katika hali hii ya mwisho katika ulimwengu huu, mioyo yetu hujazwa faraja na
kukipokea kifo si kama adhabu na hukumu, bali rafiki na njia ya kwenda kule
aliko mkombozi wetu Yesu Kristo. Huku ndiko kusimama katika Imani na kweli, na tutende haki daima, yaani, kutosaliti
Imani yako na kumsaliti yule aliyekufia ili uwe huru mwili na roho, na kifo
kisiwe tena laana kwako. Huku ndiko kumtendea haki Kristo na Roho Mtakatifu.
Wapendwa
wana wa Mungu, Injili yetu ya leo inasema neno hilo hilo ila kwa namna
nyingine. Kutokana na hali ya ukandamizi ya dola ya Kirumi, hasa kwa kulipa
kodi, baadhi ya Mafarisayo na Maherodi wanamtaka Yesu atoe majibu ya changamoto yao kama ni
halali kuendelea kulipa kodi ile kwenye dola ile dhalimu. Na kwa upande wa pili kuuliza huku kumelenga
kutikisa Mamlaka ya Kristo. Nao wanamwambia, “Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u
mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini
katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au
siyo?” Mk 12:14.
Baada ya kujua lengo
lao la pili, yaani kutikisha Mamlaka yake, Yesu anataka kuona fedha hiyo ili
afikishe ujumbe wake. Baada ya Yesu kuwauliza fedha ile inachapa ya nani na wao
kumjibu, Yesu anawajibu kwa kuwaambia,
“mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu.
Wakamstaajabia sana,” Mk 12:17. Maneno haya ya Yesu wengi tumeyachukua ndivyo
sivyo, na hata kuhalalisha uovu kwa kusema hakuna ubaya ninapoyatenda hayo ya
kipagani-Kaisari, na nikiyatenda ya Mungu-Matakatifu katika maisha ya kila siku.
Ukweli wa maneno haya ya Yesu ni huu, “Hata katika majiribu tusiyoyajua
tusimame katika Imani na kweli, na tutende haki daima.” Tenda lile
lililoamuriwa, ila usipoteze utashi wako na Imani yako. Na unapoheshimu utashi
wako na kushikilia Imani yako, huwezi kuogoba mateso na sintofahamu kwa kile
utakachokumbana nacho. Hali hii ya kuheshimu utashi wako na kushikilia Imani
yako hushinda hofu ya kifo. Ukufanya kuwa tayari kukikabili kifo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU KUWA NAMI HADI SIKU WA MWISHO YA PUMZI YANGU. AMINA.
No hay comentarios:
Publicar un comentario