sábado, 20 de junio de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI WIKI YA 12 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 12 YA MWAKA-B
21/6/2015
Somo I: Ayu 38:8-11
Zab: 106:23-24, 25-26, 28-29, 30-31
Somo II: 2Kor 5:14-17
Injili: Mk 4:35-40

Nukuu:
Au ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni,” Ayu 38:8

tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao,” 2Kor 5:15

Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena,” 2Kor 5:16 

Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya,” 2Kor 5:17 

Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji,” Mk 4:37 

Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” Mk 4:40 

TAFAKARI:Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya kumi na mbili ya mwaka “B” wa Kanisa. Leo wazo kuu kwa masomo yetu yote matatu ni kutafakari nini sababu ya woga ndani mwetu kama kweli twamwamini Mungu. Wakati mwingine twashikwa na woga wa vitu vya kawaida kabisa na kukosa mwelekeo wa maisha. Ni hofu au woga wa vitu vya kawaida kabisa kama asemavyo Mzaburi, “hapo waliingiwa na hofu pasipokuwapo hofu…” Zab. 53:5a.

Mfano:-
Kuogopa giza sana kiasi cha kutothubutu kutoka chumba kimoja kwenda kingine wakati wa usiku, Kuogopa kutembea barabarani mpaka uwe na mtu, Kuogopa wadudu na viumbe kama mende, chura, panya, kinyonga, mjusi, Kuogopa watoto wachanga na wazee. Mtu akiona kikongwe anapita yupo tayari hata kubadili njia ili asipishane naye, Hofu ya maisha yatakavyokuwa magumu, Hofu ya maisha ya kesho, Hofu ya kuolewa na kuoa: wakikijiuliza itakuwaje watakapoanza maisha ya ndoa? Hofu ya matukio magumu ya maisha huleta roho inayotufanya tumchukie MUNGU na kutenda dhambi. Hofu huzaa kushtuka shtuka na kufanya mtu kuugua magonjwa ya mwili, Pia hofu ni  mbaya zaidi inapokutawala

Hofu za mtindo huu hazipaswi kutawala maisha yetu, isipokuwa hofu ile ya Mungu. Yesu anatuambia, “msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” Mt 10:28. Hofu hii ya Mungu ndiyo itakayotupeleka katika ukamilifu alioukusudia Mungu juu ya maisha yetu. Huku ndiko kuwa na hofu ya Mungu. Wengi wetu wanafikiri kwa kuwa na haya ya leo na kesho, mfano: Fedha, mamlaka, na wingi wa mali ni mwarubaini wa hofu na woga wao, la hasha. Wakati mwingi mambo hayo utuongezea hofu zaidi kama hatuna msingi Imara katika Imani. Utajikuta unapoteza muda na nguvu zako kuyalinda mambo hayo usiku na mchana. Ayubu anasema, Au ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni,” Ayu 38:8. Yapo mambo mengi katika maisha yetu ya kila siku hatuna nguvu ya kuyazuia kwa uwezo wetu wa kibinadamu.

Watu wengi wenye maisha ya kawaida na ya hofu ya Mungu, huishi kwa raha na amani ya kweli. Watu hawa wakitumia muda wao vizuri, huweza kufanya mambo mengi katika maisha yao na hata kubadili maisha na fikra za wale waliojifungamanisha na utajiri, mamlaka na  fedha. Upeo huu wakuona mbali ya kile ulicho kwa manufaa ya wengine, ni kielelezo na sababu ya sadaka ya Bwana wetu pale msalabani. Kristo kwa sadaka yake ametupa maana mpya ya maisha, na hatma yake. Yeyote anayeishi maana hii mpya ya maisha kamwe hawezi kuongozwa au kutawaliwa na hofu nyingine zaidi ya hofu ya Mungu. Mtume Paulo ananena kutoka moyoni, tena alikufa {Kristo} kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao,” 2Kor 5:15. Mkristo anayeishi kwa sababu yake mwenyewe bado hajaelewa fumbo hili la maisha mapya ndani na katika Kristo.

Fumbo hili jipya ndilo wanaloliishi wale waliojitoa na wanaojitoa maisha yao wakfu kwa ajili ya kundi zima la wana wa Mungu. Sadaka yao na maisha yao yote ni kujitoa bila kujibakiza, na kuteketea kwa kutoa nuru kama mshumaa. Hiki ndicho kiini cha maisha ya kitawa. Na kila mlei kadiri ya nafasi yake, akiwa amejifungamanisha na agano lake, huishi fumbo hili la maisha mapya ya ufufuko. Mtume Paulo anayazungumzia maisha haya mapya ya ufufuko akisema, hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena,” 2Kor 5:16. Hapa Mtume Paulo hakani ubinadamu wa Kristo, ila anakazia zaidi maisha mapya ya ufufuko kwa yeyote yule anayemwamini Kristo. Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya,” 2Kor 5:17. Maisha ya Mkristo ni maisha ya upyaisho, yaani kila siku kuwa wapya kuelekea ukamilifu hata kama udhaifu upo. Hivyo mara zote, “mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Hii ndiyo dira ya maisha ya Mkristo aliye hai na mwenye hofu ya Mungu.

Pamoja na ukweli huu, wanafunzi wake Yesu walijawa na hofu licha ya kuwa karibu na njia, ukweli, na uzima. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji,” Mk 4:37. Mtafaruku huu uliondoa amani yote waliyokuwa nayo Mitume. Wakati haya yanatokea Mfalme wa Mbingu na dunia, Bwana wetu Yesu Kristo, alikuwa kwenye usingizi msizo. Uzingizi wa Yesu haikuwa sababu ya kupuuza ukweli ule wa dhoruba, bali ulikuwa uthibitisho wa kile alicho, yaani Mfalme wa Amani. Yesu anawathibitishia wanafunzi wake, na sisi pia mambo makuu matatu mazito na yapekee aliyoyatamka katika kinywa chake, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Je, tunayo sababu ya kuwa na woga au hofu tukiwa ndani na katika Kristo? Yesu anatuambia, kama alivyowaambia mitume wake, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” Mk 4:40.

Katekista Sabas Msemakweli alikuwa muhudumu katika kigango cha Mt. Michaeli kilichokuwepo mazingira ya Waislamu. Katekista huyu alifanikiwa sana kuleta mazungumzo na uelewano kati ya waamini wake na Waislamu waliokizunguka kigango kile. Katika jambo hili alijitahidi sana.

Katekista Sabas alipenda sana kujumuika na marafiki zake Waislamu kila jioni akiwa na nafasi kwa kupata Kahawa na kucheza bao. Siku moja jioni kulizuka mada juu ya uwepo wa majini maeneo ya Makaburi. Waislamu wote waliamini hivyo, na kumfanya Katekista kutokwa na jasho kuelezea ukweli wa makaburi na kutokuwepo kwa majini hayo, akichukulia sababu ya kuwepo kwa msalaba kwenye makaburi ya wakristo. Katekista Sabas alisema hivi, “tunapomzika Mkristo na kusimika msalaba katika kaburi lake ni ishara ya ulinzi, na amani kwa mfu yule hadi hapo ufufuo wa wafu. Hivyo, Padre au wakati mwingine mimi ninavyoongoza ibada ya maziko huwa tunasema maneno haya huku tukiushikilia msalaba kwa kuchora ishara ya msalaba katika kaburi lile, ‘Uandikwe ishara ya Bwana + Mkombozi wetu Yesu Kristo aliyekukomboa kwa ishara hii, Upumzike kwa amani.’” “Hapo hakuna jini anayeweza kugusa kaburi hilo,” Katekista Sabas alisema kwa msisitizo.

Baada ya mabishano hayo bila kufikia muhafaka, Mwiislamu mmoja katika kundi lile alitoa ushauri. “Je, Sabas unaweza kwenda usiku wa manane kwenye makaburi mwenyewe na kurudi salama?” “Bila shaka naweza na mkitaka leo usiku nitakwenda,” Sabas alisema kwa msisitizo. “Je, tutajuaje kama kweli ulikwenda usiku huo kwenye makaburi hayo?” Said alimwuliza Sabas.
Mwisho walikubaliana kwamba watakusanyika mbali kidogo na makaburi hayo, na Katekista Sabas atachukua kipande cha nondo na kukisimika pembezoni mwa moja la kaburi usiku ule. Nao watamsubiri kuona kama kweli atarudi. Kwa uhakikisho Katekista Sabas akasema, “tena nitaenda nikiwa nimezalia kanzu yangu ya utume iliyobarikiwa na Baba Paroko wangu.” Basi muda ulipofika wote wakaongozana na kufika njiani walipokubaliana, kisha Katekista akaelekea makaburini akiwa na kipande chake cha nondo na kigogo cha kupigilia nondo ile ardhini.

Muda ulikwenda bila kumwona Sabas akirejea kutoka makaburini. Baadhi ya marafiki zake wale, walikimbia kurudi majumbani mwao. Said, kulipokuwa karibu kunapambazuka alijitia moyo na kwenda kuona kulikoni rafiki yake hakurudi. Kufika makaburini pale aliukuta mwili wa marehemu Sabas pembezoni mwa kaburi lile kitu ambacho kilimfanya Said kuitafuta nondo ile. Kwa mshangao aliona nondo ile ikiwa imeshindiliwa ardhini kwa kutoboa sehemu ya pindo la kanzu ya Katekista Sabas.

Hivyo sababu ya kifo chake moja kwa moja ilitokana na mshtuko alioupata baada ya kuhisi kanzu yake imeshikiliwa na kitu kisichojulikana wakati akijaribu kuondoka.

Wapendwa katika Kristo, hofu ni mbaya sana. Wengi wetu tunakufa kwa sababu ya hofu tu. Fundisho tunalopata hapa ni kwamba, haijalishi kuwa hodari wa kuyafahamu yaisha ya Ukristo wangu na taratibu zake, kama sijaweza kuishi Imani hiyo kwa ukamilifu na bila hofu. Wapo wengi wenye imani kama ya Katekista Sabas. Watu hao ni wale wanaosisitiza Kristo ni ngome yao, lakini viunoni wamesheheni mizingo ya mahirizi. Ni wale ambao hulitaja jina la Kristo kama mweza wa mambo yote, lakini ukingoni mwa milango yao na kona za nyumba zao kumesheneni mazindiko. Je, wewe ni mmoja wao?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU, TUONDOLEE WOGA KATIKA MAISHA YETU, ILI TUKUFUATE PASIPO SHAKA YOYOTE. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario