JUMATATU
WIKI YA 10 YA MWAKA-B
8/6/2015
8/6/2015
Somo: 2Kor 1:1-7
Zab: 33:2-3, 4-5, 6-7,
8-9
Injili: Mt 5:1-12
Nukuu:
“Na
ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa
faraja yote; atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale
walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu,”
2Kor 1:3-4
“Kwa
kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu
inazidi kwa njia ya Kristo,” 2Kor 1:5
“Na
tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo
washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja,” 2Kor
1:7
“Heri
walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 5:3
TAFAKARI:
“Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na
kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia;
kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kila kazi au taaluma fulani hapa duniani ina maadili yake ambayo huendana na
taaluma ile. Mfano: Kama wewe ni tabibu wa afya ya binadamu jamii inategemea
uwe na maadili ya taaluma yako hiyo, na kutokana na uwanja wako huo, jamii
inategemea kwa uhakika wote uwe mtetezi wa uhai. Kadhalika nasi kama Wakristo,
wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo, yatupasa pasipo shaka kuyaisha maadili
yanayoendana na Imani yetu. Maadili hayo hatakama yangekuwa na uzuri gani, na
faida gani katika kuyaishi, yanaupende wake wa pili, yaani, mapaswa yake.
Kuishi ukweli huo kutakudai sana kujitoa sadaka ili dhima yake ikamilika na
kuonekana.
Sehemu hii ya pili,
yaani sadaka itupasayo kuitoa kwa kuyaishi maadili hayo kama wafuasi wa Kristo,
ndiyo Mtume Paulo anayoizungumzia katika somo hili la kwanza, mwanzoni mwa
waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho. Kwa vile Bwana wetu Yesu Kristo
aliona inafaa na kumpendeza Baba wa Mbinguni kupitia njia ya mateso ili mimi na
wewe tuwe huru kutoka utumwa wa dhambi, ni kwa namna hiyo hiyo tunaalikwa
kuyapokea mateso yetu kwa furaha ndani na katika Kristo kwa sababu ni katika
Yesu Kristo mateso hayo hupata maana. Kwa mantiki hii, “Na ahimidiwe
Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika
dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu,” 2Kor 1:3-4.
Hivyo ndani na katika Kristo mateso hutufariji na kuwa sababu ya furaha yetu.
Mtazamo huu wa Kiimani
tunapoyakabili mateso yetu, hautushawishi kufikia hitimisho la mateso hayo kwa
nguvu zetu wenyewe. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa mabaji yake saba aliyotukarimia
na anayozidi kutukarimia Roho Mtakatifu yanatusaidia kuyakabili yale
yatuzungukayo. Hata hivyo hatuwezi kukwepa ukweli huu kwamba yote huwa hivyo na
kufanyika hivyo kwa huruama na matakwa yake Mungu kwetu. Hapa ndipo twaweza
kuona maana ya mateso na kile kinachotokana na mateso yetu ndani na katika
Kristo-UTAKATIFU. Hivyo tumaini letu katika mateso ni hili: “Kwa
kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu
inazidi kwa njia ya Kristo,” 2Kor 1:5. Kwa mantiki hii ni kosa kubwa la kiimani
kukata tamaa kama tunamwamini Kristo.
Wapendwa wa Mungu, kama
wewe ni mdau wa mateso ndani na katika Kristo, yakupasa kuwa FARAJA kwa wale
wote wenye mateso, na hasa yale yasiyo na majibu ya moja kwa moja na ya
kueleweka. Wewe uijuaye siri hii ya teso lenye uhusiano wake na teso la Kristo,
ndiye unayechukua nafasi ya Kristo katika tendo hili la kuwafariji wengine
wenye mateso. Hivyo, “Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara,
tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa
washiriki wa zile faraja,” 2Kor 1:7. Ninaamini pasipo shaka kwamba mateso yetu
ndani na katika Kristo yanasababu yake katika wokovu wako/wangu.
Injili yetu ya leo
inatuelezea sehemu ya kwanza ya sababu ya kile tulicho na tupasacho kukuishi.
Hiki siyo kitu kingine bali ni maadali ya kile tunachopaswa kukiishi kama
wafuasi wake Kristo. Maadili haya kwa maneno mengine ni zile HERI ZA MUNGU.
Tuelewe kwamba tumeumbwa ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho turudi
kwake mbinguni. Kuyafanya haya kwa ukamilifu wake kunatutaka kuyaishi maadili
hayo, yaani hizi heri za Mungu kwa uaminifu.
Wapendwa katika Kristo,
heri hii ya kwanza, yaani, “HERI WALIO MASIKINI WA ROHO,” “MAANA UFALME WA
MBINGUNI NI WAO,” ndio msingi wa heri nyingine zote. Pasipo kuwa na umaskini wa
roho, yaani kuwa na nafasi ya kutosha ya Mungu ndani yako, huwezi kuziishi
kikamilifu heri nyinge zote. Uhusiano wetu na Mungu ni sehemu muhimu sana kuona
sababu ya kuyafanya hayo yote kuelekea katika hitimisho letu, yaani uzima wa milele.
Hivyo umasikini huu wa kiroho hutufanya tuone sababu ya haya yafuatayo; kujua
ukweli huo, kufanya jambo hilo, na kuona thamani ya kile tukifanyacho hata kama
matokeo yake hatutayaona katika uhasilia wake kwa muda mfupi tunaoishi hapa
duniani. Masikini wa roho ni Mkristo yule mwenye hofu ya Mungu, na wale ambao
kwa dhamiri zao njema huongozwa na hofu hii ya Mungu ndani yao na kutenda
kadiri ya mwono wa kimungu hata kama hawamjui Kristo au Mungu tunayemwanini na
kumwabudu.
Hivyo ni yule mwenye
umasikini wa roho katika maana niliyoizungumzia hapo juu atakaye ona huzuni za
wengine kwa sababu hali hiyo imo ndani mwake, na hivyo ufarijika na kufarijiwa
kwa kutenda tendo hilo la huzuni. Upole wa mtu nje ya hali ya kuzaliwa nayo, ni
tabia ile aijengayo mtu, na kumwona mwinge zaidi ya mahitaji yake mwenyewe. Ni
hali ya kujali zaidi wengine, kuliko kujionea huruma mwenyewe kuliko pitiliza.
Msingi huu ni ule ule wa umasikini wa roho. Kuirithi nchi wa wale wapole ni
kuwa wahenga. Mtu huwa mhenga kwa sababu ameacha kitu cha kujifunza au kuigwa
na wengine. Kinyume cha kuwa Mhenga ni kuwa Lihoko-roho isiyo salama/bad
spirit.
Mpendwa ukiwa maskini
wa Roho utawajali wenye njaa, na kutenda haki kwa kila mmoja. Ni kwa kufanya
tendo hili bila kujibakiza nasi tutakidhiwa mahitaji yetu na Mungu kwa kipimo
hicho hicho. Hivyo, “Wapeni watu vitu,
nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata
kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile
mpimacho ndicho mtakachopimiwa,” Lk 6:38. Huku ndiko kushibishwa na Mungu
kuliko kwa haki.
Mwenye hofu ya Mungu
ndani mwake ambao msingi wake umetokana na umasikini wake wa roho, hujazwa
rehema (nguvu ya pekee katika kutenda) kwa sababu ndani mwake kuna nafasi ya
Mungu, malipo yake ni neema juu ya neema. Hivyo neema hufuata palipo na neema. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo,
jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba
ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Tazama Kristo
anavyokupenda!
Usafi wa moyo ni hali
ile yakutokuyabeba yasiyoendana na hali na tabia ya Mungu. Makazi ya Mungu na
hasa Roho Mtakatifu ni kwenye mahekalu-miili iye isiyo kuwa na hatia yo yote.
Uwepo wa Mungu ndani ya mahekalu haya ni fursa ya kumwona Mungu. Roho huyu Mtakatifu
hawezi kupata makazi yake kwenye mahekalu yasiyo na nafasi. Hivyo ni wale tu walio masikini wa
roho wenye nafasi ya Mungu ndani ya mioyo yao, na hivyo watamwona Mungu. Mioyo
safi ni hakikisho la kumwona Mungu muda wote kwani mtu huyu kesha jianda kwa
lolote.
Ni katika umasikini
wetu wa roho twaona na kujali wengine wawe na utulivu wa ndani kama tulio nao
sisi. Wito huu unatusukuma pasipo hiyana kuwa wapatanishi pale amani ile
inapokosekana. Kristo akiwa ndiye mpatanishi wetu kwa Baba yake wa Mbinguni,
nasi kwa kufanya tendo hilo la upatanishi kwa wengine twahesabiwa haki ya kuwa
wana wa Mungu. Ni maskini wa roho pasipo shaka yoyote aishie bila makuu, na
ambaye kwa hali hiyo yupo tayari kuifia haki katika kweli. Hawa ndiyo wafia
dini wa nyakati zetu ambao wapo tayari kufa kwa ajili ya wanyonge waminywao
haki zako na matajiri katika jamii tunayoishi sasa. Ukweli ni kwamba wanapoifia
haki hii, ufalme wa mbinguni ni wao. Huku ni kuishi katika hali ya watoto
wadogo, wafanyayo yote katika yote bila kujibakiza kwa sababu hawana shaka na
baba /mama yao.” Waacheni
watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa
Mungu ni wao,” Mk 10:14
Masikini
wa roho, mwenye nafasi ya Mungu ndani yake, hawezi ogoba shutuma zitolewazo juu
yake kwa ajili ya haki au kutenda haki. Haki na Wema ni baadhi ya sifa na asili ya Mungu. Hapa ndipo kwenye furaha ya
kweli tunapoifia haki tukijua mtetezi wetu ndiye chanzo na ukamilifu wa furaha
ya kweli ndani yetu. Yesu anatukumbusha jambo hili na kutupa angalisho kwa
kusema, “kwa kuwa itamfaidi mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya
nafsi yake?” Mk 8:36.
Wapendwa
wana wa Mungu, jambo la kushangaza badala ya kuishi maadili haya ya Ukristo
wetu, yaani, heri hizi za Mungu,
tumekuwa tunaishi kwa nyakati zote na mitindo tofauti tofauti ya HERI NANE ZA SHETANI kama ifuatavyo;
1. Heri
yao waliochoka sana, waliobanwa na shughuli na kukosa muda wa kukutana na
wakristo wenzao Jumapili, na shughuli za Jumuiya kila wiki. Kwa maana hao ni
wafuasi wangu waaminifu.
2. Heri
yao wanaofurahia kutambua tabia za macleri na mapungufu ya watumishi wa Mungu.
Kwa maana hao ndio vitendea kazi vyangu.
3. Heri
yao Walei na Watawa na Makleri wanaosubiri kuambiwa kufanya kitu na kutegemea
kupongezwa hata kama hawakufanya kitu. Hakika hao naweza kuwatumia vyema.
4. Heri
wanaoguswa na kukwazika kwa vitu vidogovidogo na kuacha Ukristo wao; kwa
kutokwenda Kanisani, kutoshiriki masakramenti na kuacha kusali. Kwa maana hao
ni wamisionari wangu.
5. Heri
yao hao wanaojitangaza au kudai kuwa wanampenda Mungu na wakati mwingine
wanawachukia jirani zao na ndugu zao. Hakika
hao ni mali yangu Milele.
6. Heri
yao watenganishi na waletao fujo na chuki. Wataitwa wana wangu.
7. Heri
yao wasiokuwa na muda wa kusali kabisa, na kuzisadifikisha kazi na majukumu yako
kuwa ndiyo sala. Maana hao wananiombea mimi.
8. Heri
yako wewe unayesoma haya na wewe unayeyasikia haya na kufikiri ni kwaajili ya
watu wengine na siyo wewe mwenyewe. Hakika
nimeshakupata tayari.
Tumsifu Yesu Kristo!
Furahini, na kushangilia katika mateso ndani na katika Kristo; kwa
kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni
No hay comentarios:
Publicar un comentario