jueves, 4 de junio de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 9 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 9 YA MWAKA-B
5/6/2015
Somo: Tob 11:5-17
Zab: 145: 1-2, 6b-7, 8-9a, 9bc-10
Injili: Mk 12:35-37
Nukuu:
“Tobiti akamkumbatia Tobia na kulia kwa furaha: “Ninakuona mwanangu! Wewe ni mwanga wa macho yangu!” Kisha akasema,“ Atukuzwe Mungu! Litukuzwe jina lake milele! Watukuzwe malaika wake wote watakatifu. Yeye aliniletea mateso haya lakini sasa amenionea huruma, na naweza kumwona mwanangu Tobia!”” Tob 11:11c-15.

Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako,” Mk 12:36

TAFAKARI: “Yote yawezekana kwa Mungu, mwamini”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, baada ya mateso ya muda mrefu ya  kupofuka kwake Tobiti, Mungu kupitia malaika wake Rafaeli, anaponywa upofu wake. Mungu aliye yote katika yote, huwatumia watu tunaoishi nao kufikisha hazma yake kwetu, na hasa wale wanaomtegemea na kumwamini. Wakati mwingine masharti ya uponyaji yaweza kuwa njia za kawaida kabisa ambazo kwayo hutupa mtihani mwingine kuyasadiki mambo makuu hayo ya Mungu. Kwa maana nyingene, Mungu utumia vile alivyoviumba kwa kuponyesha vile vilivyodhaifu. Upofu wa Tobiti unaponywa kwa nyongo ya samaki. (Rejea pia simulizi la Jemedari Naaman 2Fal 5:1-14)

Majaribu karika maisha licha ya kukuza imani yetu, utujengea ustahimilivu. Ustahimilivu huu ni maandalizi ya kutumika vyema baada ya kulishinda jaribu hilo. Ni kufundwa vyema ili kuwa mkufunzi mzuri kwa wale watakao patwa na tatizo mfanano kama lako. Kumbe wakati mwingine hatupaswi kulalamika tu kusikokuwa na maana na kukata tamaa. Kuyashinda majaribu ni kuvumilia katika Imani thabiti hadi mwisho. “Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22b.

Uvumilivu  katika majaribu tukiwa na Imani thabiti ndiyo njia pekee ya kushinda tukitumaini pia mkono wa Mungu. Bila shaka uvumilivu huu katika Imani ya kweli ndiyo jibu la uponyaji wa upofu aliokuwa nao Tobiti. “Tobiti akamkumbatia Tobia na kulia kwa furaha: “Ninakuona mwanangu! Wewe ni mwanga wa macho yangu!” Kisha akasema,“ Atukuzwe Mungu! Litukuzwe jina lake milele! Watukuzwe malaika wake wote watakatifu. Yeye aliniletea mateso haya lakini sasa amenionea huruma, na naweza kumwona mwanangu Tobia!”” Tob 11:11c-15. Mara zote tuyashindapo majaribu yetu sifa na shukrani tumrudishie Mungu aliye yote katika yote.

Injili yetu ya leo, Yesu anaondoa mashaka ya waandishi  juu ya Mamlaka aliyokuwa nayo. Yesu anajibu kama ifuatavyo, na kadiri ya utabiri ulivyo juu yake. Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako,” Mk 12:36. Mamlaka ya Yesu na uhasilia wake yaliwekwa wazi siku ile aliyojeuka sura mlimani akiwa na wanafunzi wake: Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye. Mambo yalikuwa hivi, “Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5. Hapa tunaona uthibitisho wa Yesu kuwa ni mwana wa Mungu, si kwa kujitamkia Yeye, bali Mungu mwenyewe. Jambo la pili tunafunuliwa njia sahihi ya kufuata katika nyakati zote za maisha yetu hapa duniani. Yesu Kristo ni mwana mpendwa wa Baba aliyependezwa naye na ni huyu tu twapaswa kumsikiliza.

Ni katika uthibitisho huo wa Yesu unaompa mamlaka ya kutamka maneno haya: “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Ndugu yangu nikueleweje unapoyaamini matunguri na kuyapa kipao mbele katika mafanikio yako? Shetani aweza kukupumbaza kwa muda mfupi tu na kukuinua kwa mbwembwe kwa muda mfupi tu, kwa sababu hana umilele. Ila anguko lake ni kubwa sana na kishindo chake usikika pande zote. Hii ni Imani ile aliyoifananisha Yesu ya yule mtu asikiaye maneno yake na kutokuyafanya, ambaye Yesu anamfananisha na “mtu mpumbavu (Azaniye anajua kumbe hajui), aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.” Mt 7:26-27. Ndugu yangu usisahau kwamba, “THE BLOOD OF JESUS IS THE MASTER KEY.”  Ndugu yangu, yote yanawezekana kwa Mungu, mwamini.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NIJALIE UVUMILIVU KATIKA MAJARIBU YANGU. AMINA    

No hay comentarios:

Publicar un comentario