JUMAPILI
YA 13 YA MWAKA-B
28/6/2015
Somo
I: Hek: 1:13-15, 2: 23-24
Zab:
29:2, 4, 5-6, 11, 12a, 13b
Somo
II: 2Kor 8:7-9, 13-15
Injili:
Mk 5:21-43
Nukuu:
“Yaani, Mungu
hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea,” Hek 1:13
“Kwa maana aliviumba
vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za
kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yoyote ya uharibifu, wala ahera haina
milki kama ya kifalme hapa duniani,” Hek 1:14
“Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa
maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa
matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9
“bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae
upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe
sawasawa,” 2Kor 8:14
“Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye
aliyekusanya vichache hakupungukiwa,” 2Kor 8:15
“Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata
alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi
sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako
juu yake, apate kupona, na kuishi,” Mk 5:22-23
“Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na
miwili, na kuteswa mengi kwa
mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata
kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia
habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake
tu, nitapona,” Mk 5:25-28
“Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani,
uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34
“Lakini Yesu, alipolisikia
lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu,” Mk 5:36
“Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa
babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo
yule kijana,” Mk 5:40
“Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake,
Msichana, nakuambia, Inuka,” Mk 5:41
TAFAKARI:
“Umeumbwa uishi milele, liguse vazi la Yesu, Inuka.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kumi na tatu ya mwaka “B” wa Kanisa.
Masomo yetu yote matatu ya leo yanalenga katika fundisho hili: “Umeumbwa uishi
milele, liguse vazi la Yesu, Inuka.” Wapendwa wana wa Mungu, nikuombe basi
tusafiri wote katika tafakari hii yetu ya leo. Mungu anakupenda na mara zote
haachi kukuwazia mazuri.
Mauti ni kati tukio
kubwa linalomtia hofu mwanadamu. Tunapata hofu kwa sababu hatujui kule
tuendako, na hata habari tuambiwazo kuhusu huko tuendako hatuzisadiki. Ndugu
yangu, hakuna ukweli na uhakika wa kule tuendapo zaidi ya ukweli wa sadaka ya
Bwana wetu Yesu Kristo pale Msalabani. Kwa kifo chake msalabani, mauti haina
nguvu tena juu ya maisha yetu. “Kwa maana ikiwa kwa
kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao
wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa
yule mmoja, Yesu Kristo,” Rum 5:17. Ndani na katika Kristo hatuna hofu tena
kuhusu mauti. Kifo chetu leo, na kwa yeyote yule anayemwamini Kristo, na kuishi
kadiri ya imani hiyo, kifo kimebaki kuwe ni mlango tu wakuelekea kule
tulipoandaliwa, yaani uzima wa milele. Ni kwa sababu hii, “Yaani, Mungu
hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea,” Hek 1:13. Wewe na
mimi tumeumbwa ili tuishi milele.
Uthibitisho wa jambo
hili, yaani tumeumbwa ili tuishi milele, ni uumbaji wa huu ulimwengu na
uratibishaji wake ulio wa namna ya pekee kabisa. Mazingira la ulimwengu huu,
yaani sayari tunayoishi, yameandaliwa kwa makusudi makubwa ya uhai wetu. “Kwa
maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo
ulimwenguni ni za kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yoyote ya uharibifu,
wala ahera haina milki kama ya kifalme hapa duniani,” Hek 1:14. Ila dunia hii ni mahali tu pa maandalizi ya
ule uzima wa milele. Hapa siyo makao yetu ya kudumu. Ni kweli kabisa twapaswa
kuufanya ulimwengu huu uendelee kuwa sehemu salama ya kuishi, ila siyo mwisho
wa kila kitu. Twapaswa kujiandaa vizuri tukiwa hapa duniani, ila hatupaswa
kuwekeza nguvu zetu zote hapa duniani kama ndiyo sehemu yetu ya kudumu. Tupo
safarini, tunapita kuelekea kule tulipoandaliwa, yaani maisha ya umilele.
Uzima huu wa milele
ambao ndiyo shabaha yetu tungali hapa duniani, tunaweza kuufikia kwa neema ya
Kristo mwenyewe. Licha ya kwamba wale wasiomjua Kristo bado waweza kuokolewa
kwa dhamiri zao safi wangali hapa duniani, tendo la kuongozwa katika dhamiri
iliyo safi ni neema au zawadi kutoka kwa Mungu. Haya si mastahili yetu binafsi.
Kwa upande wako na mimi tunayemjua Kristo na kujaribu kuishi kadiri ya matakwa
yake kila siku, twaitaji Neema yake. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi
alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi
mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Hakika huu ni upendo wa ajabu
sana kwetu kwa kufanywa matajiri kwa Kristo kukubali kuwa masikini.
Umasikini
wa Bwana watu Yesu Kristo uliotupatia utajiri wetu mwili na roho,
unatuwajibisha kwa tendo hilo hilo kufa kila siku kwa ajili ya wengine. Kila
mmoja wetu kadiri ya wito na vipaji vyake alivyopewa bure, yampasa kupungua
pale alipo ili uhai uongezeke pale alipo. Tunakufa kwa ajili ya wengine si kama
adhabu au kujionyesha kwamba tunaweza, “bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae
upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe
sawasawa,” 2Kor 8:14. Haya ndiyo maisha ya kisadaka tuyapasayo kuyaishi kila
siku kama Wakristo, na wenye hofu ya Mungu.
Ndugu
yangu, ukweli ni kwamba hakuna aliyefilisika kwa kujitoa sadaka kwa ajili ya
wengine. Kadiri tujitoavyo sadaka bila kujibakiza ndivyo kwa namna hiyo hiyo
tunaongezewa pale tulipojitoa bila kujibakiza. “Aliyekusanya vingi, hakuzidi,
wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa,” 2Kor 8:15. Hii ndiyo maana
halisi ya sadaka ya Kristo pale msalabani, na fundisho kwa wale wote
wamwaminio.
Injili
yetu ya leo inaeleza kwa upana fumbo sababu ya kuumbwa kwetu na dhamiri mzima
ya Mungu juu ya kuumbwa kwetu. Tumeumbwa tuishi milele, hivyo yatupasa kuligusa
vazi la Yesu, na mara zote kuinuka kama ishara ya uhani ndani mwetu. Yesu
anaanza safari yake kwa kupata taarifa ya kuzidiwa kwa mtoto wa Mkuu wa
sinagogi. “Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata
alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi
sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako
juu yake, apate kupona, na kuishi,” Mk 5:22-23. Yesu anapokea wito huo, na
akiwa njiani tazama mwanamke mwenye ugonjwa wa kutoka damu kwa muda wa miaka
kumi na mbili, anapata uponyaji na msiba wake kutoweka.
Uponyaji
wa mwanamke huyu ni tokeo la msukumu wa Imani wa kulishika vazi la Yesu. “Na
mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya
matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo,
bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia
habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake
tu, nitapona,” Mk 5:25-28. Je, vazi la Yesu leo ni lipi?
Wapendwa
wana wa Mungu, hakuna shaka kabisa leo katika Kanisa vazi la Yesu li hai na
lina nguvu sana. Vazi la Yesu katika Kanisa leo ni neema na uponyaji tuupatao
kupitia masakaramenti yake, na wahudumu wake waliowekwa wakfu kwa sababu hiyo.
Hizi ndizo chemichem za uhai na uzima. Je, ni mara ngapi nashiriki neema hizi?
Kama ninavyovikwazo, ninampango ngani kuondokana na vikwazo hivyo? Je, nitaishi
hivi hadi lini katika hali hii ya kufa na msiba huu?
Baada ya
uponyaji wa ajabu wa mwanamke huyu, hatua iliyofuata ni kujisalimisha mbele ya
Yesu. Kujisalimisha kwake mbele ya Yesu, kunamhesabia haki ya uzima wa milele. “Akamwambia,
Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba
wako tena,” Mk 5:34. Ndugu yangu, katika hatua mbalimbali za maisha Yesu
ametuponya kwa kujua au kutokujua, ila hakuna hata mara moja tumejisalimisha
kwake. Je, kujisalimisha kuna maana gani?
Kila mtu hatimaye hujisalimisha kwa mtu au kitu fulani.
Kama sio kwa Mungu, utajisalimisha kwa matarajio au maoni ya watu wengine, au
pesa, chuki, hofu, au kwa kiburi chako au tama mbaya, au ubinafsi. Ulibuniwa
kumwabudu Mungu-na kama utashindwa kumwabudu, utatengeneza vitu vingine
(sanamu) ili uvipe maisha yako. Unao uhuru wa kuchagua usalimishe maisha yako,
lakini huko huru na matokeo ya uchaguzi huo. E. Stanly Jones alisema, “kama
hutajisalimisha kwa Kristo, utajisalimisha kwa machafuko.” Kujisalimisha si
njia bora tu ya kuishi; bali ni njia pekee ya kuishi. Hakuna kitu kingine cha
kukufanikisha. Njia nyingine zote hukuongoza kwenye kukukatisha tamaa, na
kuziangamiza nafsi. Tafsiri ya King James huita kujisalimisha “huduma yenu
yenye maana.” Rum. 12:1 Tafsiri nyingine inasema, “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu,
itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo
ibada yenu yenye maana,” Rum 12:1. Kusalimisha maisha yako si hisia za
kipumbavu lakini ni tendo la akili na busara ambalo unaweza kulifanya kwa ajili
ya maisha yako. Ndiyo maana Paulo alisema, “Kwa
hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye,”
2Kor 5:9 Nyakati zako za busara zitakuwa zile ambazo unasema ndiyo kwa Mungu.
Wapendwa katika Kristo,
baada ya mwanamke huyu kujisalimisha na kupokea uzima, Yesu anapewa taharifa ya
kule aendapo kwamba binti yule aliye mgonjwa kesha fariki. Kristo anavunja hofu
yetu juu ya umauti na kusema, “Usiogope, amini tu,”
Mk 5:36. Tunaamini kwamba uzima wapatikana kwa Kristo tu. Huyu ndiye Bwana wa
Uhai. “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa
Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai,” Mt 22:32. Hata hivyo
waliokuwa kwenye msiba hawasadiki maneno haya ya Yesu. “Wakamcheka sana.
Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na
wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana,” Mk 5:40. Yesu anathibitisha
kweli hii leo kwamba, kifo siyo mwisho wa kila kitu. Hivyo hakuna sababu ya
kuogopa, bali “kuamini tu.”
Ndugu
yangu, tunapokwelekea Kristo katika majonzi na dhiki zetu huyafuta machozi yetu
na kuturudishia furaha ya kweli. Fuhara hiyo ndiyo hii; INUKA! Kwa maana
nyingine “TOKA KWENYE KABURI HILO,” na uwe huru. Hivyo Yesu “akamshika
mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia,
Inuka,” Mk 5:41. Yesu leo anakuambia wewe na mimi INUKA! Yesu anatuambia
tumwamini na wala tusiogope. Uzima tuutamanio ni kwa Kristo tu twaweza kuupata.
Zebedayo
ambaye alijulikana kwa jila la “kadogoo,” alileta hofu kubwa kwa majirani zake
kwa ujambazi wake uliokithiri. Alikoswa mara nyingi kuchomwa moto, na hata
kupigwa risasi. Alishawahi kufungwa mara nyingi tu, hata hivyo hakuona sababu
ya kuacha ujambazi wake.
Siku moja
usiku alivamia nyumba mtaa wa jirani kwa lengo la kuiba dhahabu. Alifanikiwa
kuingia hadi ndani na kwa bahati nzuri au mbaya siku ile kulikuwa na mama
mwenye nyumba tu. Mama huyu aliingiwa na hofu kumwona Kadogoo akiwa ndani na
amebeba Bastola. “Nataka zile dhahabu mara moja, la sivyo ujiandae kufa,”
Kadogoo alisema bila kupepesa macho. “Dhahabu utapata zote, je, leo ushakula
chakula?” Mama mwenye nyumba alimjibu kwa ujasiri. “Sikuja hapa kuhubiri
injili, nipe dhahabu zangu nisepe kabla kiwingu hakijatanda hapa,” Kadogoo
alimjibu kwa hasira.
Hivyo
mama yule alichukua dhahabu yote iliyokuwa kwenye kabati na kumkabidi. Kadogoo
akiwa anataka kuondoka, Mama yule alimwita na kumwambia, “Hapa pia nina laki
nane naona zitakusaidia.” Kadogo alipokuwa anapokea fedha zile, mara moja mama
yule alimtengea chakula kilichokuwepo na kumwambia, “Kula ushibe na ujue Mungu
anakupenda kama ulivyo.”
Kadogoo
alimwangalie yule Mama kama dakika tano hivi bila kusema chochote, na mwisho
akafungua kinywa chake na kusema, “siwezi kukumbuka ni lini nilianza kuimba na
hata kuwadhuru watu kwa kuchukua vilivyo vyao kwa nguvu. Pia, sijawahi kukutana
na mtu aliye jasiri kama wewe ambaye umeweza kuniambia kitu ambacho sijawahi
kuambiwa hata na mzazi wangu aliyenizaa. Hivyo naomba niondoke kama
nilivyokuja.”
Mara
Kadogo aliacha zile dhahabu na fedha na kuondoka. Kuanzia siku ile Kadogo
alipita kwa kila aliyemtendea vibaya na kuomba msamaha. Hivi leo Kadogo ni mmoja
wa viongozi wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Je, ni mara ngapi tuna mwona
Kristo kwa wale ambao kwa tabia zao tumeshawatenga? Mama huyu amekuwa sababu ya
uzima kwa Kadogoo, kwa kuthubutu kulitenda tendo lile la Yesu-INUKA! Ni kwa
kuwagusa wengine ambapo hawajawahi kuguswa twawapatia uzima wa kweli.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU NIPE UZIMA WAKO WA KWELI KILA SIKU, NA NIFANYE SABABU YA UPONYAJI NA UZIMA
KWA WENGINE. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario