jueves, 25 de junio de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 12 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 12 YA MWAKA-B
26/6/2015
Somo: Mwa 17:1, 9-10,15-22
Zab: 127:1-2, 3, 4-5
Injili: Mt 8:1-4
Nukuu:
Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa?” Mwa 17:17

Mungu akasema, Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake,” Mwa 17:19

Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao,” Mwa 17:21

“Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika,” Mt 8:1b

Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika,” Mt 8:3 

TAFAKARI: “Bwana ukitaka, waweza kunitakasa.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna tulinuiwalo kwa imani ambalo Mungu atashindwa kulifanya. Basi wewe uliyetayari nakuomba tuongozane katika tafakari hii juu ya neno hili; “Bwana ukitaka, waweza kunitakasa.” Maneno haya ni ujumbe wa kujisalimisha kwa Bwana wetu Yesu Kristo bila ya kujibakiza. Tunayasema maneno haya si kwa kuwafuatisha watu kwa jinsi wasemavyo, bali ni matokeo ya kuguswa kwetu kuliko kwa ndani kabisa. Tumeamua kupagusa pale pasipo gusika. Katika maisha ya binadamu yapo mambo ambayo waweza kushirikishana na rafiki yako wa ndani kabisa, ila lipo jambo ambalo hubakia nalo mwenyewe na Mungu wako. Jambo hili ndilo katika nafasi hii unaamua kuliweka wazi mbele ya Mungu wako ili upate uponyaji wa kweli. Wengi wetu hatupati uponyaji wa kweli kwa sababu hatupendi kulisema lile lililo la mwisho na linalo gusa uwepo wetu.

Utakapoweza kulisema hili bila hofu na shaka yoyote mbele ya Mungu ndipo upatapo uponyaji wa kweli. Mara nyingi hatupendi kusema yale yaliyo ndani ya moyo wetu tukiogopa aibu na hofu tuipatayo baada ya kusema jambo hilo. Swali kubwa na hofu yetu huwa hii: Je, tutabakia kuwa salama baada ya kusema jambo hilo? Ndugu yangu, elewa kwamba usemapo jambo hilo unalisema mbele ya Bwana na Mwokozi wa Maisha yako na siyo Edgar kama mtumishi katika sakaramenti ya upatanisho. Ni ukweli kwamba Edgar kama Padre ni Kristo mwingine, ila pale kwenye kiti cha upatanisho hasimami yeye kama Edgar, ila ni Kristo mwenyewe kwa mamlaka aliyopewa na Kristo mwenyewe chini ya utekelezaji wa Mama Kanisa.

Abramu anapopata ujumbe wa uwezekano  wa kumzaa mwana katika miaka yake hiyo ya tisini, anaona kama kichekesho. “Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa?” Mwa 17:17. Mungu ni Mungu kwa sababu nguvu na uwezo wake hatuwezi kuupima kwa vipimo vya kibinadamu. Yote yawezekana mbele ya Mungu. Yatupasa kuamini pasipo shaka. Mungu analithibitisha hilo kwa kumwangalia Sara mke wa Abramu licha ya umri wake kusogea. Mungu akasema, Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake,” Mwa 17:19. Huyu ndiye Mungu anayeweza kila kitu.

Mpango wa Mungu katika maisha yetu si wakubabaisha. Mungu afanyapo mambo yake hakosei hata mara moja. Hivyo tunapokuwa na imani mbele ya Mungu hatupaswi kwenda mbele zake kwa kubahatisha au kujaribu. Mungu wetu si wamajaribu. Jambo alisemalo linauhakika kabisa, na mara tunapojisalimisha kwake tunaamini kwamba vyote tunavyomwomba tumeshavipata. Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao,” Mwa 17:21. Muda na nyakati zote Mungu anazijua ambapo neema na baraka zake zitatushukia bila mawaa yoyote.

Huu ndiyo mwono wa wale wenye hofu ya Mungu. Leo katika injili yetu tunaona mtu mmoja mwenye hofu ya Mungu. Huyu ndiye mtu yule mwenye ukoma. Anapomwona Yesu anasema lile lililo moyoni mwake pasipo shaka,  “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika,” Mt 8:1b. Mungu kamwe hana kipingamizi chochote tunaposema lililo moyoni mwetu pasipo shaka. Huyu ndiye Mungu aliye hai. Mkoma huyu anapata uponyaji wa moja kwa moja kwa sababu imani yake haina shaka. Kesha jikabidhi mbele ya mikono ya Yesu. Ndugu yangu, mbona unaficha ukoma wako?

Wapendwa wana wa Mungu, sadaka ya Yesu pale msalabani ni tendo au mwono wa kutaka kwake sisi tuwe huru kwa kila kifungo cha dhambi. Kwa nini sasa wewe wajifungia katika kifungu hicho cha dhambi ili hali Kristo yupo tayari kukuweka huru? Muda wote Yesu anasema,  “Nataka; takasika” Mt 8:3.

Tumsifu Yesu Kristo!


JIACHIE KATIKA KIFUNGO CHAKO, YESU ANASEMA, “NATAKA, TAKASIKA.”

No hay comentarios:

Publicar un comentario