JUMATATU
WIKI YA 12 YA MWAKA-B
22/6/2015
Somo:
Mwa 12:1-9
Zab:
32:12-13, 18-19, 20,22
Injili:
Mt 7:1-5
Nukuu:
“Nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na
kulikuza jina lako; nawe uwe baraka,” Mwa 12:2
“Nami
nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote
za dunia watabarikiwa,” Mwa 12:3
“Abramu
akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote
walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili
kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaan,” Mwa 12:5
“Msihukumu,
msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile
mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa,” Mt 7:1-2
“Basi,
mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo
ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii?” Mt
7:3
“Mnafiki
wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema
kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako,” Mt 7:5
TAFAKARI: “Imani ya kweli ndiyo msingi wa
ufahamu wote.”
Wapendwa wana wa Mungu, maisha ya kawaida
kabisa tunapoishi zaidi ya mtu mmoja hujengwa katika kuaminiana. Kitendo cha
kuaminiana ni matokeo ya imani tulinayo juu ya yule au wale tunaoishi nao.
Mfano, ninaposafiri na kuingia duka lolote au hoteli yoyote na kununua maji,
ninayoimani maji yale ni salama. Kitu cha kwanza kabisa ni Imani niliyonayo.
Hatua ya pili ni ufahamu kama tokeo la imani ile, yaani ninapokuwa salama au
kutokuwa salama baada ya kunjwa maji yale. Hatua hii ndiyo tunayoiita ufahamu
wa jambo lile.
Abramu ni mfano thabiti wa Imani ya
kweli. Abramu ukiwa umri umeenda, yapata miaka 70, anapata ujumbe wa kutoka
mazingira aliyoyazoea na kwenda asipokujua. “Bwana
akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba
yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha,” Mwa 12:1. Embu fikiria inavyotuwia vigumu
kuondoka mazingira tunayoyajua na kwenda mazingira tunayoyajua inavyokuwa
vigumu. Pili, Abramu anaondoka na mali zake zote kwenda katika nchi ya ahadi
asiyoijua, bali kwa kuonyeshwa kuwa ni nchi ya kanaan. “Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na
vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani,
wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaan,” Mwa
12:5. Hili ni tendo la ujasiri sana kwa
binadamu kufanya. Abramu anaishinda hofu ya sintofahau ya kesho yatakuaje.
Ingawa Abramu
anahaidiwa kubarikiwa na kupata ulinzi wa kutosha, jambo hili si rahisi
kuliamini kwa kirahisi. “Nami
nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote
za dunia watabarikiwa,” Mwa 12:3. Tunakuwa
salama zaidi kwa mazingira tunayoyajua kuliko yale tusiyoyajua. Hapa ndipo
penye ugumu kwa binadamu kufanya maamuzi ya kina kuhusu maisha yake. Abramu
anashinda mtihani huu mgumu. Ni ukweli usiotia shaka kwamba kwa binadamu hakuna
mtihani mgumu kama kufanya maamuzi msingi ya maisha yake, yaani kuacha njia
aliyoizoea na kuanza njia nyingine au kuacha maisha aliyoyazoea na kuanza
maisha mapya na mazingira mapya.
Injili ya leo
inaongelea kwa undani juu ya kutoa hukumu. Jambo la msingi kabisa kulifahamu,
Yesu apingi utoaji wa hukumu ulio haki na kweli. Tatizo ni pale tunapowahukumu
wengine pasipo haki na kweli. Jambo la pili ni hili; hukumu tunayoitoa kipimo
chake kiwe kweli iliyondani mwetu. Hatua hii inaturudisha kwenye Imani thabiti
kwa kile tukifanyacho, yaani tutoapo hukumu. Imani hii asili na chanzo chake ni
Mungu mwenyewe kwetu kama zawadi, na pili
Imani ni tunda la Neema na upendo wa Mungu. Hivyo tufanyapo hukumu yoyote
Mungu apaswa kusimama katika tendo hilo, yaani haki ya kweli. Hatupaswi kuweka
hisi zetu za kibinadamu katika kuhukumu lililo haki. Haki lazima itendeke kama
ilivyo. Hata pamoja na haki kutendeka kama ilivyo, upendo wa Mungu lazima
utawale. Lengo lisiwe kumpoteza yule anayehukumiwa kwa haki, bali lengo liwe
kumpata. Hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu, “Msihukumu, msije
mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile
mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa,” Mt 7:1-2. Hukumu iwe ya haki, na kipimo kiwe
upendo, yaani kumpata yule aliyepotoka. Huku ya kifo haina nafasi katika maana
halisi ya mafundisho ya Yesu.
Hukumu hiyo isibebwe na
hisia za chuku, wala kulipiza kisasi, na wala isiwe kwa kumpendezesha binadamu.
“Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho
ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe
huiangalii?” Mt 7:3. Hukumu tuitoayo ibebwe
na nguvu ya maadili tuliyonayo. Tusipolifanya hili, hukumu yetu itakuwa ya
kinafiki kabisa mbele ya jamii na mbaya zaidi mbele ya Mungu. “Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika
jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la
ndugu yako,” Mt 7:5. Vibanzi vyetu ni mapungufu yetu tuliyonayo. Mara zote
tujitahidi kuyasafisha na kuachana nayo mapungufu yetu ili hukumu tuitowayo kwa
wenzetu ibebwe na nguvu ya kimaadali tuliyonayo.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU TUPE NEEMA YA
KUTENDA HAKI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario