JUMAPILI
WIKI WA 11 YA MWAKA-B
14/6/2015
Somo I: Eze 17:22-24
Zab: 91:2-3, 13-14,
15-16
Somo II: 2Kor 5:6-10
Injili: Mk 4:26-34
Nukuu:
“Na
miti yote ya mashamba itajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeushusha chini mti mrefu,
na kuuinua mti mfupi, na kuukausha mti mbichi, na kuusitawisha mti mkavu; mimi,
Bwana, nimenena, nami nimelitenda jambo hili,” Eze 17:24
“Basi
siku zote tuna moyo mkuu; tena twajua ya kuwa, wakati tuwapo hapa katika mwili,
tunakaa mbali na Bwana. (Maana twaenenda
kwa imani, si kwa kuona.),” 2Kor 5:6-7
“Kwa
maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo,
ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda,
kwamba ni mema au mabaya,” 2Kor 5:10
“Ufalme wa Mungu, mfano
wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na
mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye,” Mk 4:26-27
“Ni
kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko
mbegu zote zilizo katika nchi, lakini
ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi
makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake,” Mk 4:31-32
TAFAKARI:
“Twaurithi Ufalme wa Mungu kwa kuishi udogo kitakatifu, na kutenda madogo
madogo kwa uaminifu.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya kumi na moja ya mwaka “B” wa
Kanisa. Masomo ya leo yote matatu yanakuelekeza kutafakari neno hili; twaurithi
ufalme wa Mungu kwa kuishi udogo kitakatifu, na kutenda madogo madogo kwa
uaminifu.” Kabla ya kuzama katika tafakari hii yatupasa kuelewa vizuri jambo
hili. Cheo chetu mbele ya Mungu ni UTAKATIFU wetu na si vinginevyo. Ni ukweli
usiotia shaka kwamba kwa maisha yetu hapa duniani kila mmoja wetu kaitwa kuishi
kwa namna fulani kadiri ya wito na vipaji vyake. Lakini baada ya maisha haya,
mbele za Mungu twapaswa kwenda tukiwa tumefuzu kwa cheo kimoja tu ambacho ni
sawa kwa wote, nacho ni utakatifu wako.
Ni kwa mtazamo huu kwa
sehemu ya kwanza, kila mmoja wetu anaweza kuwa mtakatifu kwa kuishi kadiri ya
wito na vipaji vyake, na mazingira yake yanayomzunguka. Sehemu ya pili katika
ukweli huu ni kwamba, Mungu hajavutiwa na mambo makubwa sana ili ufikie cheo
hiki, yaani utakatifu wako. Uwe umefanya jambo kubwa au dogo, mizani ya
kulifanya jambo hili kuwa takatifu ni UAMINIFU katika kulitenda jambo hili. Na
sehemu ya tatu katika ukweli huu ni kwamba Mungu hajavutiwa sana na umaarufu wa
mtu; mfano familia aliyotoka, utajiri, na hata vipaji vya pekee sana ili
kufikia cheo hiki, yaani utakatifu. Mizani ya kupima ukweli wa mtu kuelekea
cheo hiki ni udogo wake, ambao ni tunda la unyenyekevu wake, na hofu yake juu
ya yule aliyemuumba, yaani Mungu Mwenyewe. Mambo haya matatu ni muhimu sana
kuyafahamu ili ujue ufalme wa Mungu namna ulivyo, unyenyekevu upasao kufuatwa,
na uaminifu katika kutenda.
Wapendwa kila mmoja
wetu kaitwa kuwa mtakatifu na huko ndipo kumwona Mungu siku ya kiama. Katika kuutafuta
utakatifu huu, Mungu hajafanya upendeleo wowote zaidi ya kuliwezesha lile ambao
machoni mwetu linaonekana haliwezekana. Wapo waliokuwa na maisha mabaya
mwanzoni na mwisho wa siku wamekuwa watakatifu. Mfano ulio wazi ni wa Mt.
Augustino wa Hippo. Mungu utuwezesha kwa neema zake kuwa kila ambacho kwa uwezo
wa kibinadamu hakiwezekani. Huyu ndiye Mungu. “Na
miti yote ya mashamba itajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeushusha chini mti mrefu,
na kuuinua mti mfupi, na kuukausha mti mbichi, na kuusitawisha mti mkavu; mimi,
Bwana, nimenena, nami nimelitenda jambo hili,” Eze 17:24.
Tunapoinuliwa
kutoka hali zetu mbaya na kuuona mwanga wa Mungu, mtindo wetu wa kuishi ugeuzwa
na kuwa tofauti. Imani huwa dira ya kila kitu tufanyacho tukielewa kwa undani
hali yetu, mahusiano yetu na wenzetu,
mahusiano yetu na mzingira yetu, na mahusiano yetu na Mungu. Hivyo “basi
siku zote tuna moyo mkuu; tena twajua ya kuwa, wakati tuwapo hapa katika mwili,
tunakaa mbali na Bwana. (Maana twaenenda
kwa imani, si kwa kuona.),” 2Kor 5:6-7. Hatuwezi kuujua ukweli juu ya Mungu
kama hatutayaoanisha mambo hayo matatu. Hivyo kuujua undani wangu ni safari ya
kuelekea kule nisikokujua. Kuujua uhusiano wangu na wengine ni safari ya kuanza
kuyaelewa mafumbo ya Mungu. Kuujua uhusiano wangu na mazingira yangu, ni safari
ya kujua siri ya Mungu ilijificha katika uumbaji wake, mambo ya ajabu
yanayonizunguka-ulimwengu na vitu vyake. Na mwisho haya mambo matatu kwa ujumla
wake yataniongoza vyema kuujua ukuu wa Mungu ndani yangu na umelele
aliotuandalia.
Hatua hii ya maisha ni mwaliko wa kuishi
utulivu wa ndani. Ni kuitafuta sauti hii moyoni mwako. Ni kuiheshimu dhamiri
yako. Na kuiheshimu dhamiri ni kuishi maisha ya kujinyenyekeza kunakolenga
kufahamu yale yaliyojificha ndani yako, kwa wenzako, mazingira yako, na Mungu.
Kuishi mtindo huu wa maisha ambao utakuitaji kufanya zoezi la dhamiri kila
siku, ni kujiandaa kwa kufa kifo chema. “Kwa
maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo,
ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda,
kwamba ni mema au mabaya,” 2Kor 5:10.
Wapendwa wana wa Mungu,
utakatifu wetu upimwa kwa udogo wetu, na kutenda kwetu kwa uaminifu. Yesu
katika kuufananisha ufalme wa Mungu ametumia sana mwono huu. Ni kweli kwamba
huwezi kuurithi ufalme wa Mungu kama huna cheo cha utakatifu. Hivyo udogo huu katika utakatifu wa mtu
unafananishwa na mbegu. Hakika mbegu na kile kutokacho baada ya mbegu hii kumea
kuna utofauti mkubwa. Hivyo, “Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu
aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa
akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua
yeye,” Mk 4:26-27. Mfano huu wa mbegu unatufikirisha mbali zaidi na kutambua
kwamba mambo madogo madogo ndiyo yatupayo utakatifu yakitendwa kwa uaminifu na
Imani. Mtu aliyemwaga mbegu hizo akuanza kuzikodolea macho na kuona zinavyomea,
bali aliamini na kwenda kulala.
Ufalme wa Mungu ni
kudhubutu kuwa kitu fulani chema na kufanya kile ambacho kadiri ya
mazingira na mtazamo wetu hakiwezekani.
Ni kufanya vile vile yale ya kawaida sana ila kwa upekee sana. Amini jambo hilo
na litenda bila shaka, naye Mungu
atabariki ulichojitoa bila shaka juu ya uwezo wake. Ni katika hali hii Yesu
anafananisha ufalme wa Mungu na mbegu ya haradali. Hivyo ufalme wa Mungu, “ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo
katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa
kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani
waweza kukaa chini ya uvuli wake,” Mk 4:31-32. Mungu hutenda mambo makuu kwa
wale wamwaminio.
Matunda ya haya madogo
madogo tuyafayanya kwa wote bila kuonyesha utofauti, hulipwa hapa hapa duniani
kwa njia tofauti na wakati mwingine hatuelewi imewezekanaje kuwa hivyo.
Linawezekana jambo hili usilifurahie moja kwa moja, ili Mungu alifanyapo
hulenga pia kutufundisha kupitia kwako wewe ambaye wakati huo haupo tena katika
hali ya uzima kibinadamu.
John ambaye alijulikana
sana kwa jina “SINA ROHO MBAYA,” alikuwa na maisha ya kawaida sana. Alikuwa na
mji wake ila nyumba yake ilikuwa ya tope na aliezeka kwa nyasi. Umaarufu wa
jina lake katika kijiji chake na vijiji vya jirani ulitokana na utayari wake wa
kuwa mstari wa mbele kuwazika wanakijiji wenzake na vijiji vya jirani. Utayari
wake ulimtambulisha hivyo katika jamii ile.
Mji wake ulikuwa karibu
sana na barabara kuu ya magari, kama wengi tulivyozoe kujenga karibu na
barabara ili kupata urahisi kiusafiri na kimawasiliano. John aliugua malaria na
baada ya wiki moja alifariki. Ila kwamba twajua wote ipo siku tutakufa, umauti
wa John yawezekana ulimjia haraka kwa sababu ya
kukosa msaada wa haraka wa kumfikisha hospitalini kutokana na maisha
yake yalivyokuwa duni. Mauti ilimfika nyumbani mwake.
Siku ya maziko yake,
watu wangi walifika kumzika kwa sababu alijulikana sana. Ila huduma ya Misa ya
wafu haikuwezekana kwa sababu kifo chake kilitokea wakati mmoja na kifo cha
askofu wa jimbo hilo. Hivyo mapadre na watawa walikusanyika jimboni kwa maziko
hayo ya Askofu. Kwa vile tukio kama hili la kifo cha Askofu huwakutanisha watu
wengi na hata Maskofu wa majimbo jirani, Maskofu walihudhuria kwa wingi pia.
Askofu mmoja kutoka
mbali ya majimbo haya jirani akiwa kwenye msafara wa kuwahi maziko haya ya
Askofu huyu aliyefariki. Kwa bahati mbaya au nzuri, gari yake ilipata hitilafu
karibu na Msiba huu wa Bwana John-sina roho mbaya. Askofu huyu alipotaka kujua
kulikoni mkusanyiko ule kwenye umji ule, aliambiwa kuna msiba na hakuna uwezo
wa kuwa na Misa licha ya uchaji na mfano mzuri wa maisha ya John.
Baada ya kufanyika mawasiliano
ya siku kati ya Paroko wa parokie ile ya John na Askofu huyu, Misa ilifanyika
nyumbani kwa John na ilikuwa mshangao wa ajabu sana. Baada ya Misa ile, dereva
wa yule Askofu alijaribu kwenda kuiwasha gari kama kujaribu hivi kama litawaka.
Cha ajabu, gari iliwaka na hapakuwa na tatizo lolote. Kila mtu alibaki
kujiuliza imekuwaje jambo hili? Haikuwahi kufikirika jambo kama hili katika
mazingira kama yale na hasa kwa mtu kama John, masikini na asiye na makuu
kupata huduma ya Misa kama ile.
Askofu aliendelea na
safari huku akiwasiliana na Maaskofu wenzake walio tangulia kwenye Maziko ya
Askofu mwenzao. Jambo lingine la ajabu ni kwamba muda ulipofika wa kuanza Misa
ile ya kumzika Askofu yule kulitokea na mvua kubwa sana ikiambatana na upepe
mkali na kutoruhusu Misa ili kufanyika kwani maandalizi ya Misa ile yalifanyika
nje ya Kanisa kutokana na wingi wa watu. Mara baada ya Askofu huyu kuwasili
jimboni, mvua ile ilikatika na kijua kilianza kuchomoza. Mambo ya mazishi
yaliendelea kama ilivyopangwa baada ya kusimama kwa muda wa masaa mawili hivi.
Ndugu yangu, uliyesafiri nami katika tafakari hii, huyu ndiye Mungu ambaye
umlipa kila mtu kadiri ya hitaji lake hasa kwa wale wamtumainio kila siku
katika udogo wao. Je, jina lako la utani hapo ulipo linaendana na huduma katika
udogo na utakatifu wako? Chunguzi jambo hilo! Maneno huumba.
Tumsifu Yesu Kristo!
No hay comentarios:
Publicar un comentario