ALHAMISI WIKI YA 12 YA MWAKA-B
25/6/2015
Somo: Mwa
16:1-12, 15-16
Zab:78:1-2,
3-5, 8, 9
Injili:
Mt 7:21-29
Nukuu:
“Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, Bwana amenifunga tumbo nisizae,
umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza
sauti ya Sarai,” Mwa 16:2
“Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona
ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake,” Mwa 16:4
“Malaika wa Bwana akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa
mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana Bwana amesikia kilio
cha mateso yako,” Mwa 16:11
“Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake
utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa
mbele yao ndugu zake wote,” Mwa 16:12
“Si
kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali
ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21
“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya,
atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha,
mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana
misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25
“kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si
kama waandishi wao,” Mt 7:29
TAFAKARI: “Onja moyoni Utamkayo Mdomoni.”
Wapendwa
wana wa Mungu, tunapoitazama historia ya ukombozi wa mwanadamu tangu kuumbwa
kwa ulimwengu, Mungu alisema na vyote vikawa. Uumbaji wa ulimwengu na vyote
vilivyomo ni matokeo ya neno la Mungu. Kwa neno yote yalifanyika kutoka utupu.
Ndiyo katika mazingira haya tunasema neno au maneno uumba. Ndugu yangu tusafiri
wote katika tafakari hii fupi tukiongozwa na neno hili; “onja moyoni utamkayo
mdomoni.” Mara nyingi kutokana na mazoea hutamka maneno bila kuyatafakari uzito
wake, kimo chake, na madhara yake. Maneno ayatamkayo mwanadamu tena yule mwenye
hofu yangu Mungu, maneno hayo uumba. Ni binadamu peke yake kwa upendeleo wa
kule kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kunampa nguvu na uwezekano huo wa
kuumba kama kiumbe shirikishi cha Mungu.
Binadamu
mwenye hofu ya Mungu kwa kutamka naneno yake yaweza kuwa baraka au laana. Haki
hii si kwa nguvu zake, bali kahesabiwa haki hii na Mungu mwenyewe kwa
upendeleo. Mbaya zaidi ni pale maneno haya yanapotamkwa na Mungu mwenyewe juu
ya mwanadamu kwa ajili ya mema na baraka zake. Mungu anayatamka maneno mazito
kwa Abramu baada ya kufanya agano naye, na kusema, “Uzao wako nimewapa nchi
hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto
mkubwa, mto Frati,” Mwa 15:18. Tazama Mungu anafanya agano hili ili hali akijua
Abramu hana mtoto. Baada ya Abramu na mkewe Sara kukaa miaka kumi katika nchi
ya Kanaani, wanasahau maneno yale ya Mungu, na hivyo Sara anampa Mumewe ushauri
ulio kinyume na ule mpango wa Mungu. “Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, Bwana amenifunga tumbo
nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu
akaisikiliza sauti ya Sarai,” Mwa 16:2. Mipango ya Mungu si mipango yetu.
Alisemalo Mungu kwa kinywa chake halitapita bure. Wapo miongoni mwetu
tumeshakata tamaa kabisa licha wakati fulani tuliweka maagano na Mungu. Maagano
haya yawezakuwa kwa njia ya sala maalumu, novena, na hata hija. Tatizo kubwa
tulilonalo hupenda kumfanya Mungu afikiri kama tunavyofikiri na wakati mwingine
tunamlazimisha kuenea kwenye ratiba zetu za kila siku bila kuruhusu mapenzi
yake yafanyika kadiri aonavyo yeye. Hatuwezi kamwe kumfungia Mungu kwenye wigo
wetu wa kufikiri. Mungu hawezi kuenea katika wigo huo.
Kucheleweshwa kwa nia na maombi yetu kutoka kwa Mungu kuna
sababu yake kubwa kwani Mungu anajua ni nini kinachotufaa, na mara tukipatapo
kiu yetu yote hufikia kikomo chake. “Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye
mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki nyoka? Au
akimwomba yai, atampa ng’e?” Lk 11:11-12. Kuchelewa kwake Mungu kujibu maombi
yetu kuna maana sana. Yatupasa kuwa na imani, na matumaini kwa kile
tulichokiomba. Hata hivyo Mungu awezi kuzuia kama tutapenda kutumia uhuru wetu
na kufanya kinyume na agano lile tuliloliweka naye. Hivyo chochote tutakacho
kipata kama tokeo la kujichukulia yote mikononi mwetu jambo hilo litatupasa
kuwajibika nalo. “Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada
ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe
mkewe.” Mwa 15:3. Sara inaiogopa aibu na hivyo anajaribu kuikimbia aibu kwa
kuharakisha uwepo wa kuwa na mtoto kupitia mjakazi wake Hajiri. Tendo hili
linamwajibisha Sara baadaye na hapo ndipo anapokosa amani ile aliyoitamani. “Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba.
Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake,”
Mwa 16:4. Badala ya Sara kupata furaha, anazidi kuongeza uchungu. Wapo miongini
mwetu wameshawamaliza waganga wote wa kienyeji kwa kutafuta mtoto. Je, nani
kakuambia binadamu anao uwezo wa kumpatia binadamu mwenzake mtoto kwa miujiza?
Watu hawa ni siri yao tu, ila yapo mambo mengi machafu huwanjiwa na wagango
hawa na huwa siri yao. FUNGUKA NA UMWELEKE MUNGU!
Injili yetu ya leo inakazia jambo hilo hilo la kuonja moyoni
yale tuyatamkayo mdomoni. Yesu anasema, “Si
kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali
ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21. Maneno maneno
tu hayatoshi. Yatupasa kuyaishi maneno hayo na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha
yetu. Hapo ndipo penye ufalme wa mbinguni. Kati yetu wapo mabingwa wa kuapa na
wakati mwingine kulitaja jina la Mungu kama ndege yule kasuku. Yatupasa
kulisikia neno na kulitenda. Kwa kufanya hivyo twaonyesha tu watu wenye ufahamu
wa Mungu, na yale yote tuyafanyayo msingi wake utakuwa imara daima. Hakuna kitu
chochote kitakacho weza kutuyumbisha kutoka kwenye imani hiyo. Kwa maana hiyo “Basi kila
asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili,
aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile,
isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25. Twaweza
kulifanya jambo hili kama tutaonja moyoni yale tuyatamkayo mdomoni.
Watu
wengi wanamshangaa Yesu mafundisho yake kwa sababu mamlaka yake yamebebwa na
maadili yake. Nguvu ya kimaadili ina kina kirefu kuliko nguvu itokanayo na
mamlaka tu ya kisiasa. Nguvu ya kimaadili huja yenyewe kwa kujionyesha nje
kadiri ya tabia ya mtu ilivyo njema na kamilifu. Waliomzunguka Yesu wanapigwa
na mchangao “kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si
kama waandishi wao,” Mt 7:29. Je, huyapima maneno yako kabla ya kuyatamka?
Tumsifu
Yesu Kristo!
MANENO
UUMBA.
No hay comentarios:
Publicar un comentario