JUMAMOSI WIKI YA 9
YA MWAKA-B
6/6/2015
Somo: Tob 12:1, 5-15, 20
Zab: Tob 13:2, 6efgh, 7, 8
Injili: Mk 12:38-44
Nukuu:
“Lakini
Rafaeli akawaita faraghani Tobiti na Tobia, akawaambia, “Mtukuzeni Mungu;
tangazeni sifa zake kwa watu wote kwa ajili ya fadhili alizowafanyia,” Tob
12:6a
“Mtukuzeni
na kulisifu jina lake. Watangazieni watu wote matendo ya Mungu kama ipasavyo na
wala msichoke kumshukuru,” Tob 12:6b
“Yafaa
kutunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu ni lazima yatangazwe kila
mahali kama ipasavyo. Tendeni mema nanyi hamtapata madhara,”Tob 12:7
“Afadhali
sala pamoja na ukweli na kusaidia maskini pamoja na kutenda haki kuliko kuwa
tajiri na kukosa uaminifu,” Tob 12:8
“Afadhali
kusaidia maskini kuliko kulimbikiza dhahabu,” Tob 12:8b
“Sadaka
kwa maskini humwokoa mtu na kifo na kumtakasa dhambi zake zote,” Tob 12:9a
“Wale wanaowasaidia maskini watajaliwa uhai,” Tob
12:9b
“Lakini wale wanaotenda dhambi na kufanya uovu
hujiletea madhara wao wenyewe,” Tob 12:10
“Jihadharini na waandishi, wapendao
kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na
viti vya mbele katika karamu; ambao
hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu
iliyo kubwa,” Mk 12:38-40
“Huyu mjane maskini ametia zaidi
kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali
iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo,
ndiyo riziki yake yote pia,” Mk 12:43-44
TAFAKARI: “Mtukuzeni Mungu; tangazeni sifa zake kwa watu wote kwa
ajili ya fadhili alizowafanyia, tendeni mema kwa watu wote”
Wapendwa wana wa Mungu, tukifanya
tathimini ya kina kuhusu maisha yetu, na namna Mungu anavyotuchukulia hasa pale
tunapokwenda kinyume na matakwa yake, hatunabudi kumtukuza Mungu, kutangaza
makuu yake, na kutenda mema kwa watu wote. Malaika Rafaeli anawaasa Tobia na
Sara kuwa na mwelekeo huo katika maisha. Kuna Baraka tele tunapotambua nafasi
ya Mungu katika maisha yetu, na kumshukuru kila wakati. Ndugu yangu, ingefaa kila sekunde useme neno ASANTE kwa
Mungu. Tupo kama tulivyo; kuwaza, kupanga, kufanya, na uhuru hata wa kwenda
kinyume na mpango wake Mungu kwa upendo wake aliotukirimia. Kwa kweli Mungu ni
waajabu sana!
Wapendwa ni mara ngapi waona umuhimu huu wa kutoa shukrani
kwa Mungu, hata kwa yale madogo anayokutendea, mfano kukukinga na magonjwa,
ajali, kukupa afya njema, na hata uelewano mzuri na jirani zako? Kufanya tendo
hili la shukrani ni kutangaza makuu ya Mungu kwa kile anachokufanyia. “Mtukuzeni
na kulisifu jina lake. Watangazieni watu wote matendo ya Mungu kama ipasavyo na
wala msichoke kumshukuru,” Tob 12:6b.
Hatua
ya pili ya kutangaza matendo makuu haya ya Mungu inatuwajibisha kwenda mbali
zaidi. Huku ni kuona na kutambua kuwa wapo wengine walioumbwa kama wewe ila
hawana fursa ulizojaliwa wewe. Kwa kutambua jambo hili, yakupasa kufanya kitu
kwa wale wote wanaohitaji upendo huo wa Mungu aliokujalia wewe kwa wakati na
nafasi uliyokuwa nayo. Hata kama ni siri yako na Mungu, yakupasa kuonyesha
upendo huo kwa wengine. Hivyo, “Yafaa kutunza siri ya mfalme, lakini matendo ya
Mungu ni lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tendeni mema nanyi
hamtapata madhara,”Tob 12:7. Huku ni kujiweka karibu na vizuri zaidi na Mungu.
Kutenda mema huku kusibakie kama wazo fulani tu la kufikirika katika uzuri
wake. Yatupasa kuliweka katika tendo halisi kama Mungu anavyotufanyia matendo
halisi na wakati mwingine tunabaki katika mshangao mkubwa.
Hatua
hii ya pili katika kushukuru ni muhimu sana. Hapa ndipo tunapouweka upendo wa
Mungu katika mazingira yetu ya kibinadamu. Hapa ndipo tunapompa Mungu umbile
letu, kama alivyo lifanya neno kuwa mwili. Hapa ndipo ninapomwona masikini kama
ndugu na mmoja ya familia yangu. Hivyo, “Afadhali sala pamoja na ukweli na
kusaidia maskini pamoja na kutenda haki kuliko kuwa tajiri na kukosa uaminifu,”
Tob 12:8. Baraka na neema alizokujalia Mungu si kama upendeleo kwako ila Mungu
anakutaka utoe kwa upendo na ukaribu aliokujalia kuzipata mali hizo. Huna
kilichochako katika uhalisia wa umiliki wa hicho ulicho nacho. Vitu vyote na
mali zote ni vyake Mungu. Mali yetu halali ni dhambi zetu. Hivyo, “Afadhali
kusaidia maskini kuliko kulimbikiza dhahabu,” Tob 12:8b
Ni
vigumu sana kama tutakuwa na mwelekeo wa kujilimbikizia mali tu kwa sababu
ndiyo mtindo wa kimaisha. Tumepewa mali ili tuzitumie vyema si tu kwa sababu
yetu binafsi, ila kwa wengine pia. Ndugu yangu, kwa wewe kuwa na mali ulizokuwanazo si kwamba una
nafasi ya pekee sana mbele ya Mungu. Kumbuka hata yule ambaye ameumbwa kwa sura
na mfano wake Mungu, yaani huyo aliyekupa mali hizo ana nafasi iliyo sawa na
wewe mbele yake. Kwa kujali wajibu huu wa kuwaona wengine katika utajiri wetu
ndipo tunapopata uhai. “Wale wanaowasaidia maskini watajaliwa uhai,” Tob 12:9b.
Kinyume cha maneno haya ya Mungu kupitia malaika wake Rafaeli ni ukweli
usiopingika. Tusipoyafanya haya kwa ukamilifu wake, tutegemee madhara. “Lakini
wale wanaotenda dhambi na kufanya uovu hujiletea madhara wao wenyewe,” Tob
12:10
Angalisho:
Tunayafanya haya yote si kwa vile jamii inatutaka tuyafanye hivyo, bali ni
msukumo wa ndani na ulio wa kweli kutoka kwa Mungu, mara na baada ya kutambua
uwepo wa Mungu kwetu na sababu ya maisha yetu hapa duniani. Jambo hili halikuwa
msingi wa kweli wa maisha ya mafarisayo. Waliyafanya hayo yote ili kujizolea
umaarufu “ujiko” kwa binadamu. Yesu anatoa angalisho na onyo kwao na kwetu leo
pia. “Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi
marefu, na kusalimiwa masokoni, na
kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa
unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa,” Mk 12:38-40.
Hatari ya mafarisayo haikuishia hapo tu katika kupata huo umaarufu/ujiko kutoka
kwa wanadamu, bali walienda mbali zaidi hata kuwadhulumu wajane ambao iliwapasa
kuwapigania. Je, leo katika jamii yetu Tanzania tunakwepa dhambi hii?
Ndugu yangu, haijalishi Mungu kakujalia utajiri wa namna
gani. Unachotakiwa kufanya ni kujua kwamba ulichonacho umeazimishwa tu kwa
wakati, na itakupasa siku moja utoe hesabu yake. Basi kabla ya kashfa hilo ya
matumizi mabaya ya mali na vipaji uliyokopeshwa kwa muda mfupi kukupata mbele
ya uso wa Mungu, tathinini namna unavyotumia mali hiyo na vipaji hivyo alivyokujalia
Mungu. Yesu anatupa kielelezo cha namna ya kufanya. Yesu anapowatazama watoa
sadaka katika hekalu, anawanong’onezea wanafunzi wake, na kusema “Huyu mjane
maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali
iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo,
ndiyo riziki yake yote pia,” Mk 12:43-44. Je, mali na utajiri ulikuwa nao
unatoa vyote kwa wahitaji kwa ukaribu uliokirimiwa na Mungu?
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU TUJALIE NEEMA YA KUISHI NA KUTOA KWA WENGINE KADIRI
UNAVYOTUKIRIKIA. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario