JUMANNE WIKI YA 13 YA MWAKA-B
Somo: Mwa 19:15-29
Zab: 25:2-3, 9-10, 11-12
Injili: Mt 8:23-27
Nukuu:
“Ikawa
walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala
usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea,” Mwa
19:17
“Tazama,
mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako
ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe
na yale mabaya, nikafa,” Mwa 19:19
“Ndipo
Bwana akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni
kwa Bwana,” Mwa 19:24
“Lakini
mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi,” Mwa 19:26
“Wanafunzi
wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia,” Mt 8:25
“Akawaambia,
Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na
bahari; kukawa shwari kuu,” Mt 8:26
“Wale
watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?” Mt 8:27
TAFAKARI: “Tusipobadilikia na
kumrejea Mungu, kiama ki juu yetu hata sasa.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kuangamizwa kwa Miji ya Sodoma na Gomora kwa matendo yao mbaya hakuna
tofauti na ulimwengu wetu huu wa leo. Ni hivi jusi tu huko Marekani wamepitisha
sheria ya kuhalalisha ndoa za jinsia moja. Mungu alivyomuumba mtu mwanamke na
mwanaume alijua wazi ni kwa njia hiyo halali Taifa lake litakua na kuongezeka.
Kwa hatua hii ya binadamu kutengua kile kilichokuwa sababu ya uumbaji wake, ni
kupalia moto hasira ya Mungu.
Pamoja na
juhudi alizozifanya Ibrahimu kutuliza hasira ya Mungu kwa kumtaka Mungu
asiangamize miji ile ilihali wapo wachache wenye haki, juhudi hizo zinagonga ukuta
kwa sababu uovu uliwaingia hadi wakawa vipofu mioyoni mwao na akilini mwao.
Hata hivyo Mungu ni mwingi wa rehema na huruma. Familia ya Lutu inanasuliwa na
angamizo hilo la moto. “Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe
umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi
kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa,” Mwa 19:19. Ila mke wa
Lutu anabadilika na kuwa Jiwe la chumvi kwa kutokufuata masharti na maelekezo
kutoka kwa malaika wa Mungu. “Lakini mkewe
Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi,” Mwa 19:26. Kosa lake ni
kujeuka na kutazama yaliyokuwa yanatokea kule alikotoka.
Ni
kweli uliowazi kwamba, msukumo wa kupitisha sheria ziendazo kinyume, uhalisia,
na makusudi ya Mungu (kiimani), mara nyingi husukumwa na migandamizo ya
kisiasa, na ajenda binafsi, hivyo kuweka uhalali wa serikali hiyo kuendelea
kuwa madarakani. Ukweli wa kitu ubakia kuwa kweli hata kama kwa wakati huu
wengi walio vipofu mioyoni mwao na akilini mwao wataubeza. Bila shaka yaliyotokea
Sodoma na Gomora ndiyo yanayotokea kwenye miji na jamii yetu leo, na mfano hai
ni hili lililopitishwa huko Marekani.
Uzinifu
wa hali hii ni chukizo kwa Mungu. Huku ni kwenda kinyume kabisa na makusudia ya
uzazi na maana ya Ndoa Takatifu. Tendo la ndoa ni Takatifu linapofanywa kwa
utaratibu aliouweka Mungu mwenyewe. La sivyo hatuwezi kukwepa adhabu ya Mungu. “Ndipo Bwana akanyesha juu ya Sodoma na juu ya
Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa Bwana,” Mwa 19:24. Dhambi ya uzinifu
katika Agano la jipya imekemewa sana na Kristo.
Amri hii si tu kuwa
inazuia uzinzi na uasherati bali pia uchafu wa aina zote kwa kutenda, kwa
maneno na hata kuwaza. Katika hubiri la mlimani Yesu aliifundisha na kuifafanua
amri hii akasema: “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia,
Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake,”
Mt 5:27-28. Wale wote wanaoitwa kwa jina la Mungu hawapaswi kuwa wenye
kuwaka tamaa za uzinzi na uasherati.
Amri hii inahusu
kuheshimu kifungo cha ndoa. Maandiko Matakatifu yanasema kuwa “Ndoa na
iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi
Mungu atawahukumia adhabu” Ebr 13:4. Ndoa ni takatifu na inawaunganisha
mme na mke kuwa mwili mmoja. Maandiko yanasema: “Kwa hiyo mwanamume atamwacha
baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
Mwa 2:24.
Ukubwa wa Uvunjaji wa Amri Hii ni hayo
niliyokwisha kusema kwenye jamii yetu leo, na mbaya zaidi hili lililotokea
Marekana kwa kupitishwa sheria ya kutambua ndoa za jinsia moja. Kwa mantiki
hii, sidhani kama kuna mtu ambaye hajui jinsi udhalimu wa uasherati na uzinzi
ulivyokithiri katika ulimwengu huu. Kiwango cha uvunjaji wa amri hii ni kikubwa
na kinatisha. Mioyo ya watu imekufa ganzi kwa uovu huu. Katika baadhi ya
mataifa na hata baadhi ya madhehebu ya dini uzinzi, uasherati, ushoga, ndoa za
mikataba na za watu wa jinsia moja vyote vimepitishwa na kuhalalishwa kisheria.
Mtandao wa internet
umejaa picha za uchi na matendo ya kujamiiana (ponografia). Mataifa yenye nguvu
yanashinikiza mataifa mengine ili nayo pia yaruhusu na kuhalalishwa ushoga kuwa
moja ya haki za binadamu. Wanadamu hawaoni tena udhambi/ ubaya wa dhambi hii.
Kumbukumbu za kuongezeka kwa ushoga nchini Marekani zipo
hivi: Newsweek, Machi 12, 1990 “47% ya Wamarekani wanaamini kuwa mahusiano ya
kimapenzi kati ya wanaume wanaokubaliana yapaswa kuhalalishwa.” Baada ya
kutafakari haya yote, Bill Graham, mhubiri maarufu, alisema “Kama Mungu
hatakuja hivi karibuni na kukikomesha kizazi hiki, itabidi aombe radhi kwa
aliyowatenda wakazi wa Sodoma na Gomora”. Inatisha, watu wamevuka mipaka yote.
Je, nini mtokea ya udhalimu huu?
Kwanza kabisa, uvunjaji wa amri hii ni kati ya mauovu
ambayo yalisababisha watu wa wakati wa Nuhu kuangamia kwa gharika na miji ya
Sodoma na Gomora kuangamizwa kwa moto kadiri ya mtazamo w asomo letu la leo.
“Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa
kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri;
wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. Bwana akasema, Roho yangu
haitashindana na mwanadamu milele… Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni
makubwa duniani …,” Mwa 6:1-5. Yesu anasema watu wa wakati huo “walikuwa wakioa
na kuolewa” Lk 17:27. Hii ni sawa na kusema walikuwa wakioa na
kuacha na kuoelewa na kuachika, hawakufuata wala kuheshimu taratibu za ndoa.
Kwa ukengeufu huo Mungu akawaangamiza. Maandiko Matakatifu yanaliweka wazi jambo
hili, “uasherati, uzinzi na kuingilia kinyume na maumbile ni udhalimu, sehemu yao ni katika ziwa la moto” 1Kor 6:9.
Wapendwa wana wa Mungu,
amri hii inakataza kila aina ya uchafu na udhalimu wa kujamiiana, na kila aina
ya mihemuko inayoongoza huko. Kila wazo na tendo linaloelekezwa huko ni
uvunjaji wa amri hii na ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. Maandiko yanasema:
“Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila
yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya
kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu …? Sasa basi,
mtukuzeni Mungu katika miili yenu”. 1Kor 6:18-20
Injili
inatutaka tuwe watu wa Imani ya kweli. Hatuwezi kumkiri Yesu kuwa ni njia,
kweli na uzima, na wakati huo huo kukosa Imani naye. Imani hii thabiti ni kwa
vipindi vyote; wakati wa mambo yakiwa shwari na wakati wa migogoro katika
jamii. Leo swala la uzazi, familia, na mahusiano ni changamoto kuwa sana.
Yatupasa kusimama katika kweli, na kulisema jambo hilo kwa Imani iliyo kweli.
Haitoshi kupiga kelele tu kuwa tunaangamia, bali tunapopiga kelele tunaangamia
tuwe tumesimama imara katika Imani.
Ni
kweli yatupasa kumwendea Yesu muda wote, na hasa katika mikwamo iliyozidi akili
na maarifa yetu. Mitume wanalifanya jambo hilo wanapoona chombo chao cha
kusafiria kikiwa matatani. “Wanafunzi
wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia,” Mt 8:25.
Kanisa kama chombo kielekeacho uzima wa milele, na sakramenti ya wokovu wetu
kwa wabatizwa wote, mara zote hukaa kama familia na kupeleka maombi mbele ya
Kristo ambaye Kanisa ni mwili wake. Tufanyapo jambo hilo kama mwili wa Kristo
ulioingiliwa na udhaifu (dhambi), twapaswa kusimama katika Imani ya kweli. Yesu
anatoa karipio kwa wanafunzi wake na si pia katika nyakati zetu na kusema,
“Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na
bahari; kukawa shwari kuu,” Mt 8:26. Je,
ndugu yangu, unaimani kweli kwa kile umwombacho Mungu? Au waenda kwake ukiwa na
wasiwasi? TUZIOMBEE FAMILIA ZETU ILI ZIBAKI SALAMA.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU KITAZAME
KIZAZI CHETU UTUHURUMIE. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario