jumanne wiki ya 10 ya mwaka-b
9/6/2015
Somo: 2Kor 1:18-22
Zab: 118:129, 130, 131, 132, 133, 135
Injili: Mt 5:13-16
Nukuu:
“Maana
ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni
Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi,” 2Kor 1:20
“Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate
kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16
TAFAKARI:
“Ninyi ni chumvu ya dunia, na nuru ya ulimwengu: matendo yenu yamtukuze Baba
yenu aliye Mbinguni.”
Wapendwa
wana wa Mungu, swala ya imani halina mbadala, yaani kubadilika badilika kama
kinyonga. Kwa maana nyingine nI heri kuwa moto au baridi kuliko kuwa viguvugu.
Hatumwendei Mungu kwa hali ya kusitasita. Hivyo kujitoa kwa Mungu asilimia
tisini na tano haitoshi na hiyo siyo imani ya kweli. Hatumwendei Mungu katika
hali ya mashaka huku tukitamka kwa vinywa vyetu “Mungu ni mweza wa vyote.” Basi
niwaombe nyote tusafiri pamoja katika neno hili; “Ninyi ni chumvu ya dunia, na
nuru ya ulimwengu: matendo yenu yamtukuze Baba yenu aliye Mbinguni.” Ndugu
yangu waamini jambo hili?
Mtume
Paulo anaelezea Imani ya kweli ni kusimama katika NDIYO itokayo ndani yako.
Bila shaka wote tunamfahamu vizuri “chura.” Nina swala moja kwako, Je,
unapomtazama chura kasimama au kachuchumaa? Usicheke! Fanya utafiti unipe jibu.
Kwa upande wangu hadi leo sielewi pozi la chura ni “mwamko/kusimama” au
“mchuchumao/kuchuchumaa.” Hatupaswi kupata ugumu wa kimtazamo na kiimani kama
tuupatao kwenye pozi la chura. Hivyo imani yetu yapaswa kuwa NDIYO ya herufi
kubwa. “Maana ahadi zote za
Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu
apate kutukuzwa kwa sisi,” 2Kor 1:20. Kama tunataka Mungu atukuzwe kupitia
sisi, twapaswa kusimama imara na kuamini kile tunachokisimamia.
Kati yetu tupo ambao ni
mabingwa wa kuhama Kanisa moja na kwenda lingine kama walivyo wachezaji wa
mpira maarufu ulimwenguni. Tunapoishi Imani yetu hatuna lengo la kumfurahisha
mtu fulani au watu fulani. Lengo ni kumtukuza Mungu, na tendo hilo libakie kuwa
shuhuda kwa wengine. Mshangao huu na ushuhuda huu ndiyo unaotuelekeza
kumtangaza mtu kuwa kwenye heri au Mtakatifu. Ukilenga kumpendezesha mtu, au
kundi la watu, utaambulia huzuri na masikitiko kwa sababu yale yote yatupayo
furaha ya leo na sasa hayana umilele. Ipo siku yatachuja au kupitwa na wakati.
John Masifa alikuwa
mchezaji mzuri sana wa mpira wa mikono. Kwa kupitia kwake, timu yake ya chuo
ilipata vikombe vingi sana, na hivyo kulipamba jengo lile la utawala la Chuo.
Hivyo John Masifa aliweka nia ya dhati kabisa mara baada ya kumaliza masomo
yake angependa kurudi chuoni pale awe mkufunzi.
Kwa vile Mungu si
Edgar, yote yaliwezekana na akarudi Chuoni pale baada ya miaka mitano kama
Mkufunzi na mkuu wa chuo. Lakini jambo la kusikitisha hakuviona vile vikombe
katika jengo lile la utawala. Hivyo alianza kuvitafuta.
Siku mmoja akiwa
anatafuta kipande cha mbao katika moja ya stoo za zamani aliona pipa kumbwa
lililosheheni kila aina ya uchafu pembezoni kwa ukuta. Pipa hili lilimvutia, na
hivyo alikwenda na kuona kilichoko ndani yake. “Ha! Kumbe vikombe vyote na zile
picha zangu vimetupwa huku?” John Masifa alisema kwa masikitiko.
Ndugu yangu, kwa
uhakika Imani yetu msingi wake haujengwi kwa yale tu yatufurahishayo moyo kwa
wakati fulani katika maisha. Mambo hayo hayana umilele kwa yenyewe.
Mwanafalsafa Plato anatusaidia katika jambo hili. Plato anasema yote haya
tunayoyaona na hata kuyafanya ni kivuli tu cha uhalisia wa kitu kile kilichopo
katika ulimwengu wa mafaa-“good.” Je, kwa nini sana unapoteza muda wako wote na
kuweka roho yako kwenye uvuli wa vitu?
Wapendwa wana wa Mungu,
Yesu anatupa mpango mzima wa thamani yetu mbele ya Mungu. Sisi tu chumvi ya
dunia, na nuru ya ulimwengu. Je, nini maana ya maneno haya? Bila shaka tu
chumvi ya ulimwengu kimtindo wa maisha, namna ya kuishi na wenzetu katika
jamii. Yatupasa kuchanganyika na watu kwa matendo yetu mema ili tuwe kikolezo
kama ilivyo kazi ya chumvi. Pamoja na matumizi mengi ya chumvi, chumvu hutumika
kuhifadhi vyakula visiharibike, kukoleza na kuleta ladha ya chakula, na chumvi
pia utumika kuyeyusha barafu. Basi kuchanganyika huku katika jamii kwa matendo
yetu mema mfano wa chumvi, yaani kuhifadhi tunu njema za jamii/maadili na
kuruhusu uwepo wa Mungu kama hofu yetu. Kama chumvu, tuwe kikolezo cha upendo
pasipo na upendo, furaha pasipo na furana, haki pasipo na haki, na uwajibikaji
palipo na uzembe. Mwisho kama chumvi, yatupasa kuyeyesha barafu ya chuki na
visasi katika jamii, kuyeyusha maovu wanayofanyiwa wazee, walemavu wa ngozi na
wanyonge wasio na watetezi.
Wapendwa tusisahau sisi
pia ni nuru ya ulimwengu. Kana nuru maisha yetu ya lenge katika maadili mema.
Tutambulike mbele ya jamii tunayoishi kwa maadili mema na kupitia kwetu kama
barua zisomazwa, tuwe kielelezo cha wengine kuona nuru hiyo, kuifuata, na
kubadilika. “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu,
wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16. Taifa letu leo
linaangamia kwa mmomonyoko wa maadili. Kumbe haitoshi tu kusema, bali
mabadiliko haya yaanzie kwangu mwenyewe.
Tanzania
yetu ya leo inanitia hofu kubwa sana. Ni jana tu mtu kashitakiwa na kuhukumiwa
kwa kosa la wizi wa mali ya umama kwa uthibitisho wa kutosha. Mtu huyo huyo
jana usiku kasafishwa kosa lake na wezi wenzake waliovalia ngozi ya kondoo, na
leo asubuhi mtu huyo anaomba ridhaa yetu tumkabidi mali ile aliyotuibia jana.
Tunashawishika kwa ubwabwa wa maharage na soda ya Pepsi na kuuza uhuru wetu na
watoto wetu. Hakika Tanzania kama ni mwili basi saratani imeshakuwa “cronic.”
Tuyafungue macho na mioyo yetu kuuona ukweli huu.
Wapendwa
katika Kristo, si lengo langu kuongelea siasa kisiasa, bali ninaongelea siasa
kama sehemu muhimu ya maisha kijamii ambapo mimi na wewe tunaoufanya mwili wa
Kristo, yaani Kanisa ni sehemu ya jamii hiyo. Ni kosa kubwa kwa Mkristo kusema
siasa haimuhusu. Au tusichanganye siasa na dini. Kwa kukana ukweli huu ni
kutenda siasa. Leo katika Kanisa moja ya mambo muhimu katika masomo ya “fundamental Theology,” ni kuhusu “Political
Theology.” Huwezi kumtenganisha binadamu na jamii yake anayoishi. Kufanya hivyo
ni kuishi katika ndoto za kugushi mchana kweupeeee! Embu tujikumbushe ile sala
ya Bwana wetu Yesu Kristo, “Wala
mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba
mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi
tulivyo. Mimi siombi kwamba
uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile
kweli; neno lako ndiyo kweli,” Yoh 17:11, 15-17. Je, sala hii ya Yesu inasema
nini juu ya maisha yako kijamii?
Ndugu yangu, bado tupo
ulimwenguni, na inatupasa kuufanya ulimwengu huu kuwa sehemu salama ya kuishi kila
mmoja wetu bila kujali itikadi za vyama na wafuasi wake. Kama Watanzania jukumu
la kuilinda amani si kwa kundi fulani la watu waliojihesabia haki ya kuongoza
milele, bali ni jukumu la kila mmoja wetu. Mambo yatakapo haribika hakuna
atakayekutambua wewe kwa dhehebu lako. Kuilinda Amani ni kufanya tendo la siasa
kwa sababu linagusa jamii na sisi wote si visiwa wala milima, bali ni sehemu ya
jamii hiyo.
Tusifu Yesu Kristo!
TU CHUMVI YA DUNIA NA
NURU YA ULIMWENGU.
No hay comentarios:
Publicar un comentario