JUMAMOSI WIKI YA 12 YA MWAKA-B
27/6/2015
Somo: Mwa 18:1-15
Zab: Lk: 1:46-47, 48-49, 50, 53, 54-55
Injili: Mt 8:5-17
Nukuu:
“akasema,
Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi
mtumwa wako,” Mwa 18:3
“Akamwambia,
Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana
wa kiume,” Mwa 18:10a
“Kwa
hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na
bwana wangu mzee?” Mwa 18:12
“Bwana
akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana,
nami ni mzee? Kuna neno gani lililo
gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani,
na Sara atapata mwana wa kiume,” Mwa 18:13-14
“Yesu
akamwambia, Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7
“Yule
akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu;
lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona,” Mt 8:8
“Yesu
aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni,
Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10
“Naye
Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini,” Mt 8:13
“ili
litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa
udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu,” Mt 8:17
TAFAKARI: “Ukarimu
ni baraka.”
Wapendwa
wana wa Mungu, bila shaka si mgeni wa neno hili ukarimu. Mtume Paulo anatupa
maana halisi ya neno ukarimu. “Lakini
nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa
ukarimu. Kila mtu na atende kama
alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu
humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” 2Kor 9:6-7. Ni kwa maana hii
Ukarimu ujeuka kuwa baraka kwani ndivyo Mungu apendavyo tufanye.
Ibrahimu anabarikiwa na
kuhaidiwa kutokana na ukarimu wake. Anapowaona wageni wale watatu, anawahudumia bila kujibakiza. Naye anasema,
Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako
nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako,” Mwa 18:3. Wageni hawa watatu ni
fumbo zima la UTATU MTAKATIFU, Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Huu ni
ugeni mkubwa sana. Tupatapo mgeni au wageni, yatupasa kuwahudumia kama walivyo
kadiri ya kile wanachohitaji wakati ule. Tulifanye jambo hili bila kuwa na
upendeleo au utofauti wa kulifanya kutoka na mwono wa yule tuleyekutana naye
kama mgeni. Ibrahimu anajitoa bila kujibakiza kutokana na hali yake.
Ukarimu ni uwepo wa kimungu ndani
yetu. Unapofanya tendo la ukarimu unahakisi uwepo wa Mungu ndani
yako. Mungu ni MKARIMU! Tunapowakarimia wenzetu wenye mahitaji mbalimbali
twafanya tendo la Kimungu, na tendo hilo Mungu usimama hapo. Mungu hutujibu
mara moja tulifanyapo tendo hili bila kujibakiza. Ibrahimu anapewa uhakikisho
huo mbele ya Mungu. Naye “Akamwambia,
Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana
wa kiume,” Mwa 18:10a. Ndugu yangu, unapomkarimu mtu usiangalie alikotoka,
undugu uliokua nao naye, ukabila wako naye, ukanda wenu, na hata utaifa wenu.
Yatupasa kulenga kwenye hitaji la mtu husika, na tulifanye jambo hilo bila
kujibakiza.
Ni
ukweli usiotia shaka kwamba kadiri ya mtazamo wetu wa kibinadamu, na hali
tuliyonayo kibailoogia-elimu viumbe, ni vigumu kuamini kutendeka kwa yale
ambayo kiualisia yeshapitwa na wati wake. Hatuwezi kutegemea mwanamke mwenye
umri wa uzee wake kuwepo uwezekano wa kumpata mtoto. Maandiko matakatifu
yanatuambia kwamba Sara alikwisha fikia kikomo katika desturi ya wanawake. Hapa
ilimaanisha kwamba kwa hali ya kawaida, ilikuwa vigumu kupata mtoto. Hivyo
jambo hili kwa Sara ni kama kichekesho fulani. “Kwa
hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na
bwana wangu mzee?” Mwa 18:12. Pamoja na
kihoja hiki, Mungu anasimama na kuonyesha umungu wake pale mitazamo yetu,
desturi zetu na uwezo wa akili zetu unapofikia kikomo chake. Huyu ndiye Mungu!
Wapendwa wana wa Mungu,
Mungu wetu siyo wa kushindwa hata mara moja. Mungu wetu ni mweza wa mambo yote,
na huyafanya mambo hayo si tu kwa kuonyesha ukuu wake, bali ndivyo ilivyo asili
yake. Kama yeye ndiye mwanzo na mwisho-alfa na omego ni kitu gani chini ya jua
kitamshinda? Kama uwepo wetu leo na sasa ni kwa sababu yake, je, atashindwaje kuyarekebisha
maisha na mfumo wetu? Hivyo Mungu anasimama katika ukweli huu na kumwambia
Ibrahimu, “Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami
ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la
kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara
atapata mwana wa kiume,” Mwa 18:13-14. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Injili
ya leo ni mwendelezo wa Mungu wetu mweza wa vyote. Mungu hutujibu mara
tunapomwelekea bila shaka yoyote. Imani ndiyo msingi wa yote tuyaombayo kwa
Mungu. Tunapomwelekea Kristo katika mahangaiko yetu, na kuwa imara katika
imani, jibu lake ni moja tu.
“Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7. Tunakosa neema hii pale
tunapoanza kubabaika katika imani. Mara nyingi twapenda kupata majibu ya haraka
kwa kile kinachotusumbua bila la kujua hathari zake, na hasa hatma ya
mahangaiko yetu. Hatma ya mahangaiko yetu ni uponyaji wa kweli. Tunaposukumwa
na majibu tu ya yale yanayotusumbua, tunaishia kwanye ufahamu wa haraka na usio
na uweledi wa kiimani. Hapa ndipo wakristo wengi hudondoka. Tupo kati yetu
tunaoamini kwanza majibu ya waganga wa kienyeji kabla ya kupeleka kesi hiyo
mbele ya hakimu mwenye haki na mamlaka yote, Yesu Kristo. Pamoja na utayari wa
yule akida juu ya Imani aliyokuwa nayo kuhusu Yesu, haoni sababu ya Yesu
kufanya safari na kuleta uponyaji huo ili hali uzima upo ndani na katika
Kristo. Hivyo anaonyeshesha imani yake isiyo na shaka kwa Yesu na kusema,
“Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na
mtumishi wangu atapona,” Mt 8:8. Ndugu yangu, hiki ni kikomo cha hali ya juu
kwa kile tukiaminicho.
Yesu alifumbii jambo
hili macho bila kulisemelea. Hapa ndipo mahali Yesu anapotuonyesha nini maana
ya Imani ya kweli. Pamoja na mamlaka aliyokuwa nayo yule Akida, alitambua
mamlaka aliyokuwa nayo Yesu. Kujishusha kwa Akida huyu ndipo kunapo muhesabia
haki. Hivyo “Yesu aliposikia hayo,
alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani
kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10. Je, ni wangapi tulio
tayari kuuvua ubwana wetu na kuuvaa utwana?
Ndugu yangu, katika
Imani ya kweli ndipo penye uponyaji wa kweli. Uponyaji wa kweli ndani yetu
tunatembea nao ila hatujua ni wapo kwa kushika. Hili linajidhihirisha kwa
maneno ya Yesu mwenyewe. Naye anamwambia yule Akida, “Nenda
zako; na iwe kwako kama ulivyoamini,” Mt 8:13. Ndugu yangu, bila shaka upo
wakati unafanya maombi kwa nia mbalimbali. Leo ngoja nikumegee siri ya
kufanikiwa katika maombi yako. Kwanza, kuwa na imani kwa kile unachokiomba
kwamba umeshakipata tayari. Pili, kila neno ulitamkalo kwa imani hiyo nena
maneno haya, “nani nasimama katika neno hili nililolitamka bila shaka.” Hapa
ndipo Mungu ulitimiza lile tuliombalo kadiri tulivyoliamini.
Kristo mara zote
anatutakia uhai, tena uhai wa kweli. Ni kwa namna hii, “ili
litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa
udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu,” Mt 8:17. Yesu anamponya mama mkwe
wa Petro na mama huyu anawahudumia. Kristo mara zote anatwaa udhaifu wetu na
kuyachukua magonjwa yetu. Ndugu yangu, magonjwa yako wayapeleka wapi?
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU
TUKARIMIE MAISHANI MWETU UKARIMU KWA KILA TUNAYEKUTANA NAYE. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario