JUMATANO
WIKI YA 11 YA MWAKA-B
17/6/2015
Somo: 2Kor 9:6-11
Zab: 111:1-2, 3-4, 9
Injili: Mt 6:1-6, 16-18
Nukuu:
“Lakini
nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa
ukarimu,” 2Kor 9:6
“Kila
mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa
lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” 2Kor 9:7
“Mkitajirishwa
katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi
yetu,” 2Kor 9:11
“Angalieni
msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya
kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 6:1
“Bali
wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa
kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na
Baba yako aonaye sirini atakujazi,” Mt 6:3b-4
“Bali
wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango
wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini
atakujazi,” Mt 6:6
“Bali
wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na
watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini
atakujazi,” Mt 6:17-18
TAFAKARI:
“Apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni siku nyingine tena ambapo Mungu hachoki kutukirimia neema zake, na wakati
mwingine twashangazwa kupatana neema na baraka nyingi kwa upendeleo mkubwa. Ila
leo kwa namna ya pekee tunakumbushwa neno hili, “apandaye kwa ukarimu atavuna
kwa ukarimu.” Neno ukarimu si geni masikioni mwetu. Neno hili linatumika sana
hasa pale tunapohamasishana kujitoa-sehemu ya mali yetu kwa wengine na hasa mahitaji mbalimbali ya Kanisa.
Ukarimu wa mtu ni moja
ya malezi ya mtu huyo. Hapa ndipo tunapotapa maana halisi ya msemo huu,
‘ukarimu huanzia nyumbani.’ Wapo baadhi miongoni mwetu msamiati huu “ukarimu”
si sehemu ya lugha yao. Walio wengi ni wakarimu kutokana na malezi yao toka
familia zao. Kwa maana hii, ukimwona rafiki yako si mkarimu jaribu kuchunguza
familia yake. Yawezekana kwenye familia yake ndiko kwenye chuo cha uchoyo.
Pamoja na uhalisia wa baadhi ya watu kuwa wachoyo kupindukia, ukweli unabakia
pale pale kwamba, “MOYO USIO NA SHUKRANI UKAUSHA MEMA YOTE.” Neno hili ndilo
analotufundisha leo Mtume Paulo kwamba, “apandaye haba atavuna haba; apandaye
kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu,” 2Kor 9:6
Wapendwa wana wa Mungu,
wengi hatufanikiwa katika kazi zetu licha ya kufanya kazi hizo usiku na mchana
kwa sababu tu tumeshindwa kuwa wakaribu, na hasa kumrudishia Mungu sehemu ya
mali yake. Yote tulivyonavyo si mali yetu. “Fedha
ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi,” Hag 2:8.
Wewe na mimi mali tuliyonayo halali ambayo ni yetu kwa asilimia mia moja ni dhambi
zetu. Vipaji ulivyo navyo, mali uliyonayo, vyote ni vya Mungu. Ni jambo la
busara ukafikiria vizuri mfumo wa maisha yako.
Ndugu tunayesafiri
pamoja katika tafakari hii, yatupasa kutafakari njia zetu kama kweli zinaendana
na matakwa yake Mungu. Je, ninaona furaha kutoa sehemu ya mali yangu kwa ajili
ya wahitaji, na hasa wanyonge? Kunafaida kubwa sana tunapowakumbuka wanyonge.
Bwana asema hivi, “Heri amkumbukaye myonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu,” Zab
41:1. Wengi hatufanikiwi kutoka na mifumo mibovu ya kimaisha. Mifumo isiyokuwa
na hofu ya Mungu ndani yake. Nabii Hagai anatupa sababu ya kutokupata baraka
mbele za Mungu. “Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini
njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa
lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na
yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko
uliotoboka-toboka,” Hag 1:5-6. Tunapata baraka na neema juu ya neema tunapotoa
kwa moyo sehemu ya mali yetu kwa wahitaji.
Mara
zote ona unawajibu wa kufanya wa kutoa kwa moyo na fanya hivyo. Hivyo, “kila mtu na atende kama
alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu
humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” 2Kor 9:7. Jaribu kufikiria fedha
unazotumia kwa matumizi kama haya yafuatayo; ulevi, vipodozi, waganga wa
kienyeji, kutoa rushwa na kupokea rushwa; na linganishe na fedha unazotoa kwa
ajili ya kuwasaidia wahitaji ikiwa ni pamoja na sadaka yako ya jumapili. Je
kuna uwiano mzuri?
Mungu hakatai wala
hapingi sisi kuwa matataji hata kidogo. Tendo la Neno kufanyika mwili na kukaa
kwetu ni tendo la kutukuza imani na kutuweka karibu na Mungu na upendo wake ili
tuweze kuuridhi ufalme wake. Katika tendo hili kunamanisha pia kwa umasikini wake
Kristo kuuchukua Mwili na kukaa kwetu, amejifanya masikini ili sisi tuwe
matajiri. Hivyo, “Maana mmejua neema ya
Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa
tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Kwa
mantiki hii, kadiri Mungu anavyokukirimia ni kwa namna hiyo hiyo unawajibishwa
kuwa mkarimu kwa kutambua upendo wa Mungu kwako. Ufahamu huu si tu kwa mali
zinazoshikika, bali pia kwa vipaji vyetu kwa ajili ya wenzetu tunavyojitoa kwa
utayari bila kujibakiza. Ni kwa namna hiyo, “mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa
na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu,” 2Kor 9:11. Je,
yanipasa kutumia njia gani katika tendo hili la
ukarimu?
Njili yetu leo inatupa
kinagaubaga namna ya kufanya na inavyompendeza Mungu. Leo tulio wengi
tunapowasaidia wahitaji na hasa; wazee, mayatima na wajane, tunatenda tendo
hili kwanza kwa kuwakusanya watu ili waona tunachokitoa, pili, tuna viita
vyombo vya habari ili wautangazie ulimwengu jinsi tunavyotoa. Tufanyapo tendo
hili kwa mfumo huu twajisikia raha nafsini mwetu, na kujipongeza kwa kufanya
kazi nzuri ya kichunguji. Je, kuwa Baba au Mama mwema na mkaribu kwa familia
yako unaitaji kuvaa au kubeba bango lenye maandishi kama haya; “Baba mwema na mkarimu,”
ili familia ijue ukweli huo? Nafikiri hapa kwa kiasi kikubwa tunakosea sana
tunavyofanya hivyo. Yesu anatoa onyo na angalisho pia, anavyosema, “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi
mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu
aliye mbinguni,” Mt 6:1. Tendo kama hili halina dhawabu yo yote machoni mwa
Mungu. Ni kweli watu watatusifia na kutuandika kwenye magazetu yao, ambayo
kesho yake magazeti hayo hayo yaliyopambwa jana kwa utoaji wetu yatafungia vitumbua
na historia yote inaishia hapo. Je, imani na matumaini yako ipo kwa watu? “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye
mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha
Bwana,” Yer 17:5. Bali, “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye
Bwana ni tumaini lake. Maana
atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto;
Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala
hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda,” Yer
17:7-8. Tunapowategemea wanadamu hasa kwa matendo yetu ili yawapendezeshe
hatuna tofauti na Mafarisayo nyakati zile za Yesu.
Yesu
leo anatupeleza mbali zaidi na hasa matendo yale tuyafanyayo ilikwa ni kumrudishia
Mungu sifa na shukrani, hatupaswi kuyafanya kama maonyesho mbele za watu ili
watuone. Matendo haya ni utoaji wa dadaka, sala, na kufunga. Anayetukirimia
neema na baraka katika matendo hayo ya kiroho ni Mungu mwenyewe. Hakuna maana
yo yote ya kuomba huruma kwa watu mara tuyafanyapo mambo haya. “Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue
ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka
yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi,” Mt 6:3b-4. Ni kweli
utoapo kwa siri, ndivyo hivyo Baba yako aonaye sirini atakujazi. Ila tusimwibie
Mungu au kumdanganya Mungu kwa kumpa kile kisicho halali. Mfano mdogo ni huu;
ukiangalia shilingi hamsini hadi mia mbili huwezi kukuta maneno haya, “Fedha
halali kwa malipo ya shilingi, mia tano, elfu moja au elfu kumi,” ambayo yapo
pia kwenye noti ya shilingi elfu mbili, na elfu tano. Je, unapotoa sadaka yako
jumapili shilingi hamsini, mia moja, au mia mbili, unatoa fedha halali
ukilinganisha kwa kipato chako cha mwezi? Kama kuna uwiyano hautakuwa umetenda
kosa, na hautakuwa umejifungia baraka na neema za Mungu. Kama unacho kingi na
unasema kwa matendo yako unachokidogo, Mungu atakipunguza kadiri ya matendo
yako. “Wakamkasirisha kwa matendo yao; tauni ikawashambulia,” Zab 106:29. Mungu
aweza kukufanya chochote kadiri na uchoyo wako.
Na
tusalipo yatupasa kuunganika na Mungu katika undani wetu na siyo kupayukapayuka
ili watu wajue tunasali. “Bali wewe
usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako,
usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi,”
Mt 6:6. Hatumpendezeshi yeyote tunaposali bali Mungu ambaye ni yote katika
yote, na tunauonja ukaribu wetu na Mungu, kwa njia ya kumshukuru, kumtukuza,
kumwomba na kumsifu.
Na
mwisho tunapofanya tendo la kufunga kuwe na malengo. Licha ya kuwa ni tendo la
kiroho, kufungu ni tendo la kiafya pia. Je, ninavyojinyima nafanya hivyo kwa
sababu gani hasa? Na kwa kufunga kwangu kumelenga maisha yangu ya kiroho? Je,
ninalenga hasa utakaso ndani mwangu, au nalifanya tendo hilo kwa vile imekuwa
mazoe kila kipindi fulani cha mwaka watu hufanya hivyo nami nafanya? Pili,
tendo hilo mwisho wa siku linawalenge watu gani kama shukrani kwa Mungu? Haya
ni maswali muhimu sana ya kujiuliza kabla ya kufanya zoezi hili la kiroho.
Maswali hayo yakipata majibu yake fanyi hivi, “wewe
ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na
Baba yako aonaye sirini atakujazi,” Mt 6:17-18. Kujipaka mafuta ni kutokuwavuta watu kujua
unachokifanya kwa sababu tendo hili ni la kiroho zaidi.
Tumsifu Yesu Kristo!
TUPANDE KWA UKARIMU
ILI TUVUNE KWA UKARIMU KILA WAKATI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario