viernes, 12 de junio de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 10 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 10 YA MWAKA-B
13/6/2015
Somo: 2Kor 5:14-21
Zab: 102: 1-2, 3-4, 8-9, 11-12
Injili: Mt 5:33-37
Nukuu:
Tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao,”  2Kor 5:15

Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya,” 2Kor 5:17

Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye,” 2Kor 5:21

 “lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;  wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu,” Mt 5:34-35

Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu,” Mt 5:37

TAFAKARI: “Thamani ya Ukristo wako.”

Wapendwa wana wa Mungu, ‘ng’ombe hauthamini mkia wake hadi hapo utakapokatwa.’ Msemo huu unamaana sana katika maisha yetu ya wafuasi wa Kristo. Ni kweli pia wengi hatuoni thamani ya ukristo wetu kutokana na kutokupata misingi halisi na imara ya kiini cha imani yetu. Yawezekana pia mtindo wa maisha tunayoyaishi umetupelekea kutokuona umaana wa ufuasi wetu. Wapo wale waliozaliwa kwenye familia za kikristo na wakajikuta taratibu zote za kuwa mkristo zinafuatwa kama zilivyo bila kuyagisa maisha halisi ya ukristo. Hapa ninamaanisha ulizaliwa, ukabatizwa, kukapata Ekaristi Takatifu, ukaimarishwa, na mwisho wa siku ukabahatika kufunga ndoa, na leo upo kama ulivyo. Unaishi maisha ya ukristo pasipo kuguswa au kukutana na Kristo.

Kwa mtindo huo wa maisha huwezi kuona thamani yake, na mwisho wa siku hatutashangaa ukabadili dini na kuwa kitu kingine. Watu wa mtindo huu ni wale mara zote utawasikia wakitoa sentensi za jumla jumla: “Mungu ni yule yule hakuna utofauti kati ya mpagani na Mkristo.” Watu hawa ni hatari sana. Lengo lao kuu ni kujitahidi kila siku kupatana na ulimwengu na mambo yake, ila siyo kweli ya Mungu na ufalme wake. Ukweli ni kwamba tutamfuata Kristo katika kweli kama tutajua ukweli kuhusu Kristo. Kujua kweli kuhusu Kristo ni kujua sababu ya kuja wake na kifo chake. Katika somo la leo tunapewa sababu ya kifo chake. Tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao,”  2Kor 5:15.

Sababu ya kifo cha Yesu inatoa taswira mpya ya ufuasi wake. Uhai wa mkristo baada ya kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni uhai unaopinga umimi, ila hukumbatia umoja wa kindugu. Ni maisha mapya ndani na katika Kristo. Ni maisha yasiyo na kipimo cha upendo: kifamilia, kiukoo, kikabila, kitaifa au kibara. Ni maisha ya kumwona Kristo kwa kila binadamu tunayekutana naye. Ni katika ukweli huu, hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya,” 2Kor 5:17. Ni maisha yenye kujali na kuwajibika kwa ajili ya upendo usio na kipimo. Maisha haya tunapoyaishi katika mtazamo huu, ututhaminisha mbele ya Mungu na kuhesabiwa haki na Kristo kwa sababu, Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye,” 2Kor 5:21. Ni maisha yenye thamani kubwa sana.

Yawezekana nisiifahamu falsafa vizuri na hata tahuidi/teología. Ila katika hili sina shaka nalo; kwamba, wote waliokuja na kuanzisha mifumo fulani ya maisha walivuma kwa wakati wao na mwisho walikufa.  Kristo alikuja kwa wakati maalumu, na kufanya yote kwa wakati maalumu, na kufa. Ila baada ya siku tatu alifufuka kutoka wafu. Jambo hili ni kielelezo tosha cha thamani yangu kama Mkristo na mfuasi wa Kristo. Je, ukweli huu umeuona katika dini ipi isipopokuwa dini ya Kikristo, na wale wamwaminio KRISTO? Je, tunapofahamu ukweli huu tunasababu ya kuishi kama wapagani ili hali tunamjua Kristo? Kama twamjua Kristo na tunaye  katika maisha yetu kila siku, hatupaswa “kuapa kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;  wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu,” Mt 5:34-35. Je, tufanyaje?

Wapendwa, maisha ya ufuasi wa Kristo ni maisha yasiyoongwa na hofu ya kibinadamu wala mashaka yake. Hatupaswi kumwendea Kristo kwa mashaka mashaka, au kubahatisha bahatisha. Kwa mateso, kifo na kufufuka kwake ametuondolea mashaka yote kuhusu yeye. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu,” Mt 5:37. Kwa mang’amuzi yangu ya muda niliokaa parokiani niligundua wapo baadhi ya wakristo wangu waaminifu kweli kuhudhuri misa za kila siku, na dominika bila kukosa. Ila nilishangazwa kuwaona baadhi yao kila jumapili mchana baada ya kutoka Kanisani huenda pia kwenye nyumba za sala zilizojaa ushawishi wa miujiza. Huku walionekana wachangamfu kupindukia na hata matoleo yao kwenye nyumba hizi zenye kauli mbiu ya miujiza yalikuwa mara dufu.

Ndugu yangu, imani yetu na ufuasi wetu katika Kristo siyo ya undumilakuwili. Huwezi sema ndiyo hapa kwa asilimia mia moja na kunako fanana na hapo kwa asilimia hizo hizo mia. Miujiza siyo kielelezo cha Imani, bali miujiza utumika kuwasaidia wale wasiokuwa wamekomaa Kiimani. Kama namwamini Kristo siitaji miuji ili inisadikishe kuamini kwangu. Ila kwa kuamini kwambu, Kristo aweza kunitumia kuzitenda kazi zake kadiri ya matakwa yake. Kristo aweza kunitumia kama chombo chake katika kutenda alama hizo ili kuwasadikisha wale walio na imani haba. Hivyo ni muhimu kutafakati kuhusu Imani yako.

Tumsifu Yesu Kristo!


UKRISTO WANGU NI THAMANI KUBWA KWANI NIMEKOMBOLEWA KWA DAMU YA YESU YENYE THAMANI KUBWA. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario