JUMANNE
WIKI YA 12 YA MWAKA-B
23/6/2015
Somo:
Mwa 13:2, 5-18
Zab:
14:2-3a, 3bc-4ab, 5
Injili:
Mt 7:6, 12-14
Nukuu:
“Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na
kwa dhahabu,” Mwa 13:1
“Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na
wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa
katika nchi,” Mwa 13:7
“Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati
ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi
tu ndugu,” Mwa 13:8
“Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya
nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua,” Mt
7:6
“Basi yo
yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo
torati na manabii,” Mt 7:12
“Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni
mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango
huo,” Mt 7:13
“Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao
waionao ni wachache,” Mt 7:14
TAFAKARI:
“Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni
vivyo hivyo.”
Wapendewa wana wa
Mungu, ni mtu yule tu asiyejua maana ya furaha atakuwa tayari kusababisha uzuni
kwa mwenzake. Ni mtu yule tu aliyejua maana ya mateso na karaha zake atakuwa
tayari kuyasababisha na kumtendea mwenzake mateso hayo. Ila kama tunajua vizuri
namna ya kuwa na furaha ya kweli na namna ya kuwa na uchungu, mara zote
tutawatendea wenzetu yale yaliyo heri kwetu. Ukweli huu wa maisha tunaanza
kuupata katika shule ya awali kabisa, ambayo ni familia. Hatua hii muhumu
katika maisha ya binadamu ikikosewa tu, maisha yote ya mtu huwa kituko katika
jamii. Mahusiano yetu na watu na namna tunavyowachukulia ni tunda la malezi ya
familia zetu.
Kunapotokea sintofahamu
baina ya ndugu, ni afadhali tofauti hizo zirekebishwe mapema kabla ya jambo
lile kuota mizizi na kukomaa. Familia iliyolelewa vizuri katika misingi ya utu
wema ni vigumu kudondoka katika mtego wa mafarakano. Mara zote watatafuta njia
ya kutatua matatizo yao. Mara nyingi tofauti ndani ya familia iliyolelewa
katika misingi ya utu wema hutoka nje ya familia ile. Yatokayo nje ya familia
yaweza kuwa mali au utajiri, mahusiano na familia nyingine yanayotokana na kuoa
au kuolewa, watu wale tunaowachukua ili watusaidie kazi zetu-wafanyakazi. Kama
ndugu yawapasa mara zote kuliangalia jambo hili kwa makini sana. Zipo familia
ziliofarakana kwa sababu ya mali, wake waliowaoa, na wakati mwingine
wafanyakazi waliowaamini kupita ndugu aliyezaliwa naye.
Ni kweli kabisa kila
tunayeishi naye lazima tumpe mastahili yake yaendanayo na utu wake kama binadamu.
Tatizo kama hili linaonekana katika familia ya Abramu na Lutu. Hii ndiyo hali
aliyokuwa nayo Abramu na nduguye Lutu. “Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na
kwa dhahabu,” Mwa 13:1. Mali na utajiri tulionao isiwe sababu ya kututenganisha
na upendo wa Mungu, ndugu, na jirani. Hata hivyo, “kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na
wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa
katika nchi,” Mwa 13:7. Linapotokea jambo kama hili la kutokuelewana ndugu, ni
lazima ndugu mkae na kutafuta suluhu la jambo hilo. Kwanza kabisa yawapasa
kuelewa kwamba mlikuwa ndugu kabla ya mali hizo, na mtaendelea kuwa ndugu hata
baada ya kutokuwa na mali hizo. Huo ndiyo msingi wa mambo yote. Kama ugomvi
utanendelea ni afadhali mtafute njia ya kuepusha ugomvi huo, kwa kutengana
kijeografia, ila kuwa karibu kimawasiliano. Hiki ndicho alichokifanya Abramu na
ndugu yake Lutu. “Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo
ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na
wachungaji wako; maana sisi tu ndugu,” Mwa 13:8. Hakuna duka lolote hapa
nduniani linalouza undungu. Ni vyema kuheshimiana na kutaabikiana pale mambo
yanapokwenda ndivyo sivyo. Undugu huu siyo tu undugu wa damu, bali hata undugu
ule tunaoujenga kutokana na maisha yetu ya maagano: Sakramenti ya ndoa, Daraja
Takatifu, na maisha ya Wakfu.
Bwana wetu Yesu Kristo anatupatia suluhu lenye upana uliozidi
mipaka ya kifamilia. Suluhu hilo ni kuwa macho muda wote katika kujali na
kuwajibika tukifanya jambo hili la msingi, yaani, “yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo
hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12. Maana yake ni kwamba,
jambo lililo jema ni jema tu siyo kwako ila na hata kwa mwenzako. Basi litende
kama lililovyo na vizuri zaidi litende kama lako. Hufanyavyo hivyo, jua ndiyo
Mungu apendavyo liwe hivyo kwani hiyo ndiyo hamu ya moyo wake, ambayo kwetu ni
sheria. Sheria hii ya “upendo,”
twaifanya si kwakushurutishwa, bali ndicho kiini cha maisha yetu, na hofu yetu
kwa Mungu.
Ndugu
yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, jambo hilo hapo juu tusipolifanya,
na hasa kwa ndugu na wale wote wanaotuzunguka, bado hatujajua thamani ya utu
wetu, na upendo wa Mungu Baba kwetu. Hapa tunapewa angalisho: “Msiwape
mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije
wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua,” Mt 7:6. Mara nyingi
tunavipa vitu heshima kuliko utu wa mtu. Leo na hasa ulaya, mbwa au paka
anaweza kugaramiwa na kupewa upendo wa hali ya juu kuliko ombaomba aliye
mlangoni mwa Kanisa siku nzima. Mbwa huvalishwa nguo za joto wakati wa baridi,
ila masikini huyu hana hata koti kuufunika mwili wake. Binadamu na utu wake
atabakia kuwa hivyo hata kama mfumo wa maisha yake utakuwa mbovu au
kutokuridhisha. Mbwa au Nguruwe atabakia kuwa nguruwe hata kama tutajaribu
kumpandisha na kuwa na hali kama sisi. Sababu ni kwamba yale tuwafanyiayo yenye
mastahili ya kibinadamu kwao hayana maana na hayana thamani yoyote kwao.
Wanyama wapewe stahiki za wanyama, na binadamu apewe heshima yake kama binadamu
licha ya umaskini wake.
Hapa
ndipo penye mtihani mkubwa wa maisha, na tafsiri nzima ya maisha ya umilele
ikiwa ni pamoja na hukumu yake. Yesu Kristo anatupatia njia ya kufuata
tusijepigwa na mshangao siku ya mwisho. “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni
mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango
huo,” Mt 7:13. Uzuri wa njia pana ni kwamba
kunauwezekano mkubwa wa kubeba kila kitu, yaani ponda mali kadiri ya uwezo
wako, ila usisahau kifo kwani huja kwa mtindo huo huo. Na hapo ndipo penye
ubaya wa njia pana. Njia nyembamba hutukataza baadhi ya mambo kutokuchukuliana
nayo. Wembamba wa njia hutunyenyekesha namna ya kutembea katika njia ile ili
tufike kwa usalama mwisho wa safari. Njia nyembamba inatuadhabisha namna ya
kuenenda kwa faida yetu wenyewe. “Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao
waionao ni wachache,” Mt 7:14. Waionao njia hii ni wachache kwa sababu hulka ya
binadamu si kupata mateso. Ndugu yangu, elewa hakuna utukufu pasipo msalaba.
Hivyo njia nyembamba ndiyo njia sahihi kuelekea uzima wa milele.
Tumsifu
Yesu Kristo!
BINADAMU
APEWE HESHIMA YAKE NA UTU WAKE LICHA YA UMASIKINI WAKE. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario