jueves, 18 de junio de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 11 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 11 YA MWAKA-B
19/6/2015
Somo: 2Kor 11:18, 21b-30
Zab: 33:2-3, 3-4, 6-7
Injili: Mt 6:19-23
Nukuu:
Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi,” 2Kor 11:23

katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi,” 2Kor 11:27

Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu,” 2Kor 11:30

19 Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba,” Mt 6:19

Bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi,” Mt 6:20

Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako,” Mt 6:21
Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru,” Mt 6:22

Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza,” Mt 6:23 

TAFAKARI: Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.”

Wapendwa wana wa Mungu, hali ya kujifu kwa kile tulicho na yale yatutambulishayo (mali, umaarufu, cheo, elimu) katika jamii ni silika ya binadamu. Ni hali ya kibinadamu pia kusifu na kusifiwa. Tendo la kusifu na kusifiwa kwa walio wengi hutawala furaha yao. Je, ni kweli kuwa furaha yetu msingi wake ni haya tuyapatayo leo na kesho kutoweka? Wengi wetu leo hujulikana kwa utajiri uliojijenga katika umiliki wa mali. Hali hii bila shaka ni furaha kwao. Wapo wengine furaha yao imejijenga katika kazi zao wazifanyazo na mahusiano yao kwa wale wanaowahudumia, si kwa upendo bali kwa nguvu itokanayo na cheo na mamlaka waliyo nayo. Mfano Mgambo wa jiji hujisikia raha kuvuruga na kunyang’anya kwa nguvu mali za wachuuzi. Mtu huyu hupenda atambulike kwa cheo chake hata kama kwa upande wa jamii inayomzunguka ni kero kutokana na utendaji wake uliowekwa kwa taratibu mbovu za utawala mbovu.

Yawezekana pia kizazi kijacho ambacho ni matokea ya kizazi hiki chetu kikashabikia sana maisha ya kifisadi kutoka na baadhi yetu kuachwa na mara nyingine kutetewa kwa tendo hili la kufisidi mali za umma. Watu hawa wenye kufanya vitendo hivi yawezekana pasipo shaka yo yote furaha yao imejikita katika mali zilizo za wizi na dhuluma. Je, furaha ya kweli imejengwa katika misingi ipi?

Ndugu yangu tunayesafari pamoja, jambo la msingi kabisa kuelewa ni kwamba furaha ya kweli haijengwi katika vitu, ila vitu hutumika tu kama namna ya kuwezesha furaha ile ya kweli. Ni kweli kwamba unaweza kuwa na vyakula vizuri na vitamu sana, ila kama hauna hamu ya kula chakula kile kwa wakati ule, chakula hicho hakina maana yo yote. Furaha ya kweli hujengwa kwa kuanza kutazama yale yaliyomapungufu ndani yako, ambayo kwa kuyaelewa hufungua matamanio ya kuwa mzuri zaidi katika kuona, kutenda, na kuishi. Usipoona madhaifu haya ndani yako, na kuanza kuchukua hatua ya mabadiliko kuelekea kuliko kuzuri na kukamilifu, hata yale uyapatayo yangekuwa mazuri kwa namna gani hayatakuwa na maana yo yote. Furaha itokanayo na mambo hayo huwa ya muda mfupi tu, na mara zote huenda kwa wakati na mitindo ya kimaisha.

Mtazamo huu wa kujitazama mapungufu yetu ili tusonge mbele katika uzuri, wema na ukamilifu ndani mwetu, ndiyo sababu ya maneno haya ya Mtume Paulo:Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu,” 2Kor 11:30. Ni pale tu ninapojua udhaifu wangu vyema ninakuwa makini katika kuongea, kutenda, kushauri, kukaripia na hata kuhukumu kuliko haki. Huu ni msingi muhumu sana wa furaha ya kweli. Msingi huu ukiwa imara, furaha yake haitegemei kwa yale yatakayojengwa juu ya msingi huu. Kwa kuwa imara na kuyaona madhaifu yako na kuchukua hatua ya kubadilika kuelekea ukamilifu, wingi wa vitu na uzuri wake haviwezi kuwa sababu ya furaha yake.

Mtizamo huu uliojengwa katika msingi wa kweli wa furaha humfanya mtu kutokuogopa mateso, madharau, kutengwa na hata kusemwa vibaya ikiwa jambo lile alifanyalo kwalo lenyewe limesimama katika kweli. Hali hii ndiyo inayopelekea Mtume Paulo kusema “ananena kiwazimu” yale yote ya ugusao ukweli wa furaha yake ambaye ni Kristo mwenyewe. Kristo ni kioo kituwezeshacho kuyaona madhaifu yetu kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kioo hiki ni njia ya kusafisha madoa yetu kuelekea ukamilifu. Hivyo katika aina zote za magumu kimaisha tutakuwa “zaidi” kwa sababu tunajua ni nani tunayemfuata na kumtumikia kupitia wale ambao Mungu kawaumba. Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi,” 2Kor 11:23. Huku ndiko kuwa na furaha ya kweli hata katika mateso.

Mateso haya huwa na nuru kwa sababu mbele yake upo utukufu. Mateso bila utukufu ni kupotea muda bure. Kristo kama kielelezo chetu ameyashinda mateso na kutupatia utukufu. Hivyo tunapoteseka kwa sababu ya Kristo, twapata furaha tukijua pasipo shaka kwamba baada ya mateso hayo tunao utukufu. Kristo huyapa maana mateso yetu. Hivyo hatuogopi chochote katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi,” 2Kor 11:27. Hatuogopi kwa sababu tunaye jemedari wa vita na mateso ambaye aliushinda ubaya kwa wema. Je, vitu na mali tunazozitafuta mchana na usiku zina sehemu gani katika furaha yetu?

Kama nilivyokwisha kusema hapo mwanzo, vitu na mali tulivyokuwa navyo huwa na maana tu kama furaha yetu imejengwa kwa kuyaona madhaifu yetu, na kuishi kuelekea ukamilifu. Kwa hiyo vitu hivi havitakuwa ndio mwisho wa mahangaiko yetu kwa uwepo wake kwa vyenyewe. Vitu hivi huwa uwezekano tu wa kutufikisha katika ile furaha ya kweli. Yesu anatoa onyo na angalisho kuhusu mali tuzifanyazo ndio kwisho wa kila kiti. Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba,” Mt 6:19. Mfano mzuri kwa hiki akisemacho Yesu, tazama wakati wanapofariki matajiri na kuzikwa. Je, uzikwa na mali zao ambazo ndizo zilizokuwa sababu ya furaha yao? Matajiri wengine hupendekeza kuzikwa na baadhi ya mali zao, na hata wengine uenda mbali zaidi na kupendekeza kuzikwa na “vizima moto.” Je, mateso na moto wa jehenam twaweza kuuzima kwa kutumia vizima moto hivi? Tunachopaswa kufanya muda wote tuishipo hapa duniani ni kuwekeza katika uzima wa milele.

Kuwekeza katika uzima wa milele ni kujitahidi kila siku ya maisha yetu kuishi katika ukamilifu hata kama udhaifu upo. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Mt 5:48. Ukamilifu huu ni kuishi katika saburi ya kweli. Ni kuishi maisha yampendezayo Mungu, licha ya udhaifu wetu kibinadamu. Mungu katuumba wanadamu, na katika uwanadamu wetu ndivyo atakavyo tukomboa. “Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno,” Yak 1:4. Ndugu yangu unawekeza katika benki ipi hadi sasa?

Wapendwa nawashauri sote tuwekeze katika “BUM,” yaani Benki ya Uzima wa Milele. Benki hii ina usalama kuliko benk zote hapa duniani unaoweza kuufikiria. Benki hii ndiyo anayoisema leo Bwana wetu Yesu Kristo, jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi,” Mt 6:20. Je, ipo benki hapa duniani yenye usalama kupita BUM?

Mt. Agustino anasema, “Mioyo yetu haitulii mpaka itakapo tulia kwako Ee, Bwana.” Ni kwa namna hiyo basi tunapowekeza ndipo unapokuwa mtima wetu. Ndipo ulipo moyo wetu na mahangaiko yake. Ndipo palipo na hitimisho la yote tuyatarajiayo katika safari hii iliyosongwa na giza nene mbele yetu. Hivyo, hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako,” Mt 6:21. Ndugu yangu, chunguza mwenendo wako mzima wa maisha. Chunguza vizuri na wala usijipendelee kwa lolote kama kweli unataka kuenenda katika njia iliyo salama. Mungu ametupa sote UFAHAMU na UHURU wa kumrudia au kumkana, na kuifuata njia iliyo salama. Ufahamu na uhuru huu ndiyo taa ya mwili. Ufahamu na uhuru wetu ndilo jicho la kutazama na kubaini mema na mabaya. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru,” Mt 6:22.

Ufahamu na uhuru huu Mungu aliotupa tusipoutumia vyema hakika tunaangamia mchana kweupe. Ufahamu na uhuru huu ni kama kisu. Twaweza kutumia kisu kukata mkate, na twaweza kutumia kisu kwa kujiua au kuwadhuru wengine. Yesu anasema ni kwa namna hiyo, jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza,” Mt 6:23. Je, wataka kutembea katika kiza hili la umauti milele yote?

Tumsifu Yesu Kristo


EE YESU, NIONGOZE KATIKA NJIA ILIYO KWELI SIKU ZOTE ZA MAISHA YANGU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario