JUMATATU WIKI YA 13 YA MWAKA-B
29/6/2015
Somo: Mwa 18:16-33
Zab: 102:1-2, 3-4, 8-9, 10-11
Injili: Mt 8:18-22
Nukuu:
“Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki
pamoja na mwovu?” Mwa 18:23
“Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini
mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao,” Mwa 18:26
“Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu,
Huenda wakaonekana huko kumi?” Mwa 18:32a
"Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi,” Mwa 18:32b
“Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake;
Ibrahimu naye akarudi mahali pake,”Mwa 18:33
“Mwandishi mmoja akamwendea,
akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako,” Mt 8:19
“Yesu akamwambia,
Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa
kulaza kichwa chake,” Mt 8:20
“Mwingine katika
wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba
yangu,” Mt 8:21
“Lakini Yesu
akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao,” Mt 8:22
TAFAKARI: “Okoa nafsi yako na
wenzako kwa kuishi kadiri impendezavyo Mungu.”
Wapendwa
wana wa Taifa la Mungu, ni kweli kwamba hatupo ulimwenguni humu kwa bahati
mbaya. Tupo ulimwenguni humu kwa malengo ya Mungu kila mmoja kadiri ya wito
wake. Pamoja na malengo hayo mazuri ya Mungu, uwepo wetu hapa duniani ni
mwendelezo wa ukombozi wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake binafsi, na kwa upande
wa pili kila mmoja wetu kwa ukombozi wa wingine. Hivyo kwa lengo hili la pili,
Mtume Paulo anasema, “Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie
mambo ya wengine,” Flp 2:4. Somo la leo linatuelekeza kuyatafakari makuu haya.
Wokovu si tendo tu lenye kubeba maana ya mtu mmoja aliye mwema, bali kwa yule
mwema mmoja katikati ya waovu Mungu huwa na huruma kwa kundi HILO. Hapa ndipo kulipobeba maana ya swali ya
Ibrahimu na jibu la Mungu. “Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki
pamoja na mwovu?” Mwa 18:23. Mungu anamjibu
Ibrahimu na kusema, “Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini,
nitapaacha mahali pote kwa ajili yao,” Mwa 18:26.
Ukweli ni kwamba Mungu hututakia mema kila siku na hapendi
tuangamie kwa jambo lolote. Tumepewa uhuru wa kufanya lililo jema, na hata
kwenda kinyume cha yale yasiyompendeza Mungu. Ni kwa uhuru huo huo tunaweza
kumrudia Mungu kwa toba na majuto. Mungu anatujua jinsi tulivyo na yupo tayari
kutupokea jinsi tulivyo. Ibrahimu anazidi kumdadisi Mungu na kupima uwezo wake
wa kusamehe. Mungu anaonyesha hana kigezo chochote cha kusamehe ilihali
muhusika yupo tayari kuiacha njia yake mabaya na kumfuata. Ibrahimu hachoki
mdadisi Mungu kuhusu huruma yake. Naye “akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu,
Huenda wakaonekana huko kumi?” Mwa 18:32a. Mungu anaweka msimamo wake wazi na
kumjibu Ibrahimu, “Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi,” Mwa 18:32b. Je, tunasababu yoyote kupata adhabu ya Mungu kwa
mwelekeo huu wa Mungu kuwa tayari kusamehe makosa yetu?
Sodoma na Gomora ni miji iliyosikika kwa
kutokuishi maadili mema. Kulikuwa na kila aina ya dhambi. Ukimya wa Mungu siyo
kwamba hakuona maovu hayo, bali Mungu anatuamini kwamba ukweli utatuweka huru
tunapogundua na kuacha njia zetu mbaya. "Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo
kweli itawaweka huru.” Yoh 8:32. Kweli hii ndiyo tunayoitafuta kila siku ya
maisha yetu kila mmoja na wito wake. Kwa “Kuwa” utawani, au maisha ya ndoa kama
yalivyo haitoshi, ila kuuishi ukweli wa maisha hayo kama yalivyo ndio kunakoleta
utofauti. Wapo tulioingia mifumo hiyo ya maisha kama yalivyo na mwisho wa siku
tumejikuta ni watupu kabisa. Kumbe yanipasa kila siku kuuutafuta ukweli juu ya
maisha hayo na kuuishi ukweli huo kila siku, na majira yote.
Hili ndilo analolizungumzia Yesu katika Injili
ya leo. Si swala la kumfuata popote Yesu aendapo, ila kujua nini maana ya
kumfuata Yesu, na matakwa yake. Kumfuata Yesu kadiri ya injili ya leo ni
“KUACHA” utaratibu na matamanio tuliyoyazoea. Kauli ya kutangaza nia ya
kumfuata Yesu ni rahisi sana kama anavyojinadi mwandishi huyu, na kusema, “Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako,” Mt 8:19. Akilijua hilo ni
jambo rahisi kutamka kama nia, Yesu anamjibu mwandishi huyu, “Mbweha wana
pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza
kichwa chake,” Mt 8:20. Kwa maana nyingine Yesu anataka kumwambia jambo hili:
je, upo tayari kuyaacha mazuri haya ya ulimwengu na ufahari wake wote, na kuwa tayari kutaabika na kudharauliwa kwa
sababu yangu? Hapa ndipo tunaposhindwa wengi. Ni sawa na kusema, “utawa
ninaupenda, ila ufukara siupendi.” Ni sawa na kusema, “maisha ya ndoa
nayapenda, ila uzazi siupendi.” Huu ni mkanganyiko wa hali ya juu.
Kumfuata
Yesu Kristo inamaanisha pia kujibadua kutoka katika mnaso wa mazoea, au
uhasilia. Hapa yatupasa kujipanga vizuri katika hatua hii. Wengi tumeshindwa
kujibabanua na kujibandua kutoka mnaso wa kiasili tuliokuwa nao kutokana na
uhasili wa maisha yetu kama binadamu. Hakuna kati yetu aliye kisiwa wala
aliyedondoka kama mana jangwani. Sote tumetoka katika familia, na familia hizo
zinaushawishi mkubwa kuhusu hatma ya maisha yetu ya kila siku. Ila leo Yesu
anasema JIMAMANUE NA JIBANDUE KUTOKA JELA HIYO.
Mnaso huu utupelekea kujiuliza moja ya maswali haya ya kifamilia
tunayoyaishi kila siku. “Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa
kwanza, niende nikamzike baba yangu,” Mt 8:21. Ni hekima na busara pia kwenda
kuwazika wazazi na hata kuwahudumia hadi siku ya mwisho ya maisha yao kadiri ya
amri ya nne, “waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza
yenye ahadi, upate heri, ukae siku
nyingi katika dunia,” Efe 6:2-3. Ila Yesu anatupa jibu la uhakika tunapoamua
kumfuata. Yesu anasema, “nifuate; waache wafu wazike wafu wao,” Mt 8:22.”
Hatukatazwi kuwazika wazazi wetu, bali tunaonywa kuwa “mkiongozwa na Roho,
hampo chini ya sheria,” Gal 5:18. Je, ndugu yangu wewe unaongwa na nini?
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU TUFUNULIE FUMBA LA MAISHA YA WAKFU KILA SIKU. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario