miércoles, 1 de julio de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 13 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 13 YA MWAKA-B
2/7/2015
Somo: Mwa 22:1-19
Zab: 114:1-2, 3-4, 5-6, 8-9
Injili: Mt 9:1-8
Nukuu:
Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,” Mwa 22:12

Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,  katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;  na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu,” Mwa 22:15-18

Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako,” Mt 9:2

Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako,” Mt 9:6

Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii,” Mt 9:8

TAFAKARI: “Yote yawezekana kwa Mungu, kuwa na Imani.”

Wapendwa wana wa Mungu, kwa kutambua ubinadamu wetu tunatambua mwisho wa yote ndani mwetu, na mwanzo mpya wa safari yetu kiimani. Ufahamu tuupatao kutokana na vilema na mapungufu yetu utuimarisha na kutufanya tutafute jalizo la pale kulipopungua na kudumu katika hali hiyo ya ukamilisho hadi mwisho. Maisha yetu ya kila siku ni tendo la kiimani. Mtakatifu Agustino anasema, “kuamini ili kuelewa, na kuelewa ili kuamini.” Hatua ya kwanza twaanza kwa kuamini hicho kitu, na kadiri tuendeleavyo katika imani ya kitu kile, ndivyo tunavyozidi kuelewa kile tukiaminicho. Na kadiri tuelewavyo kiti hicho, ndivyo tunavyozidi kuamini kitu hicho.

Imani anayoonyesha Ibrahimu kwa uthubutu wake wa kumtoa mwanaye wa pekee kama sadaka ya kuteketezwa, ni mwendelezo kwa uelewa wa Imani yake ambayo Mungu alianza kumfunulia tangu alipomwamuru kuiacha nchi yake na kwenda ugenini. Ufahamu huu wa Imani ndiyo unaompa Ibrahimu uthabiti zaidi wa kile anachokiamini kuhusu Mungu. Ibrahimu hana shaka kabisa na ujumbe wote wote kutoka kwa Mungu. Mungu anamwamuru Ibarahimu, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.” Mwa 22:2. Baada ya kusikia ujumbe huu, Ibrahimu anachukua hatua mara moja.

Tuelewa kwamba Ibrahimu analifanya jambo hili ingawa Isaka ni mtoto wa Uzee wake na anajua wazi kwa umri aliokuwa nao ni ndoto kwa njia ya kawaida kuwa na uwezo wa kuzaa tena. Bila shaka Ibrahimu anajua vyote alivyonavyo ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu kwake. Tulivyonavyo tumekopeshwa kwa muda tu. Sisi ni waangalizi wa mali ya Mungu. Na baada ya muda mchache tutaviacha na kuwakabidhi wengine kama tulivyovikuta. Jambo lingine tunaloliona kutoka kwa Ibrahimu ni hili; kamwe Ibrahimu hakuwahi kujifananisha na mali alizokuwa nazo. Watu wanaojifananisha na mali zao ni vigumu sana kujisalimisha kwa Mungu.

Tazama wakiwa njiani kuelekea sehamu ya kutolea sadaka, Isaka akiwa amebeba kuni za kujikaangia, anamwuliza Baba yake mbona hatuna mwanakondoo ingawa vyote tumekamilisha? Jibu la Ibrahimu linaonyesha kwa kiasi gani Mzee huyu alivyokuwa amejawa Imani. Naye anamjibu mwanaye, “Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu,” Jibu hili linathibitisha ni kwa kiasi gani Ibrahimu alikuwa anayaishi maneno yake. Maneno ayatamkayo yamebeba uzito wa Imani aliyokuwa nayo.

Maandalizi yalipotimia alimchukua mtoto wake Isaka na kumlaza juu ya kuni na kuchomoa kisu chake kumchinja. Ndipo iliposikika sauti kutoka mbinguni, “Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,” Mwa 22:12. Tendo hili la ujasiri ndilo linalomwesabia haki Ibrahimu. Kuhesabiwa haki kwa Ibrahimu ni kupata baraka kutoka kwa Mungu iliyotukuka. Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,  katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;  na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu,” Mwa 22:15-18. Tujitoapa kwa Mungu pasipo shaka na pasipo kujibakiza, naye ufungua neema zake bila kikomo. Mungu utubariki kupita uwezo wetu kwa sababu tumekuwa waaminifu kwa kile kidogo alichotupa. “Bwana wake akamwambia, vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako,” Mt 25:23.

Yesu katika Injili ya leo analetewa mgojwa aliyepooza katika kitanda mzegamzega.  Yesu kuona imani ya watu wale walivyokuwa wakimtaabikia ndugu yao mgonjwa akamwambia yule aliyepoonza, “Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako,” Mt 9:2. Maneno haya ya Yesu ni maneno yenye kubeba ubaba na umama ndani yake. Maneno haya ya Yesu siyo tu ya uponyaji, bali ya kuumba  na kuleta uzima mpya. Tendo hili linawachukiza baadhi ya waandishi kwani walilitafsiri kama ni kukufuru Mungu. Watu hawa hawaoni Umungu ndani ya Yesu. Kuwakata kimbelembele chao, Yesu analiweka wazi jambo hili machoni mwao na kusema, Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako,” Mt 9:6. Kwa maneno na msimamo huu wa Yesu mbele ya waandishi hawa anadhihirisha mamlaka yake kamili, kwamba, Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3.

Wapendwa tendo alilolifanya Yesu la uponyaji linakuwa kikolezo cha Imani, na ule mkutano unafunuliwa juu ya Mambo makuu ya Mungu. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii,” Mt 9:8. Je, wewe ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, umefunuliwa jambo gani ambalo waweza kumsifu Mungu?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUONGEZEE IMANI. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario