JUMANNE WIKI YA 11 YA MWAKA-B
16/6/2015
Somo: 2Kor 8:1-9
Zab: 145:2,5-6, 7, 8-9a
Injili: Mt 5:43-48
Nukuu:
“Maana
walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao
uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao,” 2Cor 8:2
“Tena
walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa
Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu,” 2Kor 8:5
“Lakini
kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote,
na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia,” 2Kor
8:7
“Maana
mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili
yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini
wake,” 2Kor 8:9
“Wapendeni
adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili
mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake
waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki,” Mt 5:44-45
“Basi
ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48
TAFAKARI:
“Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu
aliye mbinguni.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni jambo la kawaidi kutokuwa na mawasiliano mazuri na adui yako kutokana na
vitendo vyake visivyo vizuri. Injili ya leo inatuhimiza kuwapenda adui zetu.
Je, kuna sababu yeyote ya kumpenda adui yangu? Kama ninamwamini Kristo na
sadaka yake pale Msalabani, sinabudi kumpenda adui yangu. Kama natambua kuwa
Mungu ni UPENDO, na ameniumba kwa sura na mfano wake, sinabudi kumpenda adui
yangu. Kama ninaamini katika fumbo hili la uumbaji, Mungu aliniumba kwa sura na
mfano wake, sinabudi kumpenda adui yangu. Kama ninaamini pia katika fumbo hilo
la uumbaji Mungu alimwumba adui yangu kwa sura na mfano wake, sina budi
kumpenda adui yangu. Iwaje sasa nimchukie yule mwenye sura na mfano wa Mungu? Hapa
ndipo kwenye changamoto kubwa kwangu kama mfuasi wa Kristo. Je, nifanye nini
ili niweze kumpenda adui yangu?
Mpendwa unayesafiri
nami katika tafakari hii, njia pekee ya kumpenda adui yako ni kumwombea. Kwa
vile nataka nimpende, siwezi kumwombea mabaya. Ombi langu kwa Mungu kuhusu adui
yangu lapaswa liwe hivi “Ee Mungu uliyenipenda upeo na kuniumba kwa sura na
mfano wako, na kwa namna hiyo hiyo umemwumba mtesi wangu kwa sura na mfano
wako, kwa kupitia uwezo wako huo wa ajabu wa kutenda yote mema kwa wema na
waovu, mbadili mtesi wangu aendane sawa sawa na makusudi yako katika uumbaji
wako. Nasadiki na kutambua Wewe ni Upendo, Msamaha na Furahi yetu. Amina.” Je,
adui yangu anaweza kuwa sababu ya kukomaa kwangu katika Imani?
Mpendwa katika Kristo,
wakati mwingine yatupasa kuyapima mateso tuyapatayo kutoka kwa adui zetu. Jambo
la kwanza la kujiuliza ni hili, je, mimi nimechangia kwa kiasi gani kwenye
mateso hayo? Kama hakuna lolote nililolifanya zaidi ya wema wangu kwake na
badala yake ni chuki, wivi, hasira na hata kunidhuri, basi teso hilo lina neema
na baraka kwangu. Teso hilo ni sehemu ya kukua kwangu kiroho. Teso hilo
linalenga ukamilifu wa kweli wa Mungu. “Basi
ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt
5:48. Je, kama nimechangia katika teso hilo kuna njia ya kutokea?
Mpendwa
kama unajitambua umechangia katika teso hilo, njia ya kutokea ni kujirudi.
Fanya toba ya kweli kuliko kutafuta ushindi ulipokwisha shindwa tayari. Katika
hali hii yanipasa kukivua kiburi changu na kuuvaa unyenyekevu ili niweze kuuona
mlango wenye nuru na kutoka kwenye giza hilo nene. Wengi wetu katika hali hii
tunajitutumua na kuona ni heri kufa na tai yangu shingoni kuliko kujishusha na
kujifunga kikoi. Wengi wetu neno “nisamehe nimekosa,” ni neno gumu sana
kulitamka. Ni afadhali kulia na kutokwa na machozi kuliko kusema “nisamehe
nimekukosea.” Kuomba msamaha kwa kutamka neno ni uponyaji kwako na kwa yule
uliyemwumiza. Tamka neno kwani kwa neno Mungu aliumba kutoka utupu na kuwa
kitu. Je, nifanye nini ili niwe macho muda wote katika kuishi yale yanayomcha
Mungu?
Somo
letu la leo, Mtume Paulo anatufundisha namna na kuishi na wenzetu ikiwa ni
pamoja na kuyasadifu yale yote tunayotendewa na wenzetu. Kwanza kabisa
hatupaswi kutokuwa wakarimu hata kama tunajaribiwa au kuishi katika dhiki.
Ukweli ni kwamba hupokea kadiri unavyotoa. Katika jambo hili Mtume Paulo
anatuambia, “Maana
walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa
mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao,” 2Cor 8:2. Wengi tunaokutana nao na
wanajitoa bila kujibakiza, ni watu wa kawaida sana, na mara nyingine hujinyima
sana. Mtume Paulo anatuambia hivi, “Tena
walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa
Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu,” 2Kor 8:5
Wapendwa wana wa Mungu,
ni kwa namna tunavyojitoa kwa wenzetu ndivyo tunavyokirimiwa neema na baraka za
Mungu. Na hii ndiyo moja ya sababu ya kuumbwa kwetu, yaani kumtumikia Mungu
kupitia viumbe vyake, na kwa namna ya pekee wale aliowaumba kwa sura na mfano
wake. “Kama mlivyo na wingi wa mambo yote;
imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo
hivyo mpate wingi wa neema hii pia,” 2Kor 8:7. Hakuna aliyetoa kitu kwa ajili
ya Mungu akawa masikini. “Maana mmejua
neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu,
ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,”
2Kor 8:9. Basi ndugu yangu, mpende adui yako na tenda wema kwa kila unayekutana
naye.
Tumsifu Yesu Kristo!
No hay comentarios:
Publicar un comentario