martes, 23 de junio de 2015

TAFAKARI: KUZALIWA KWA YOHANE MBATIZAJI

KUZALIWA KWA YOHANE MBATIZAJI
24/6/2015
Somo I: Isa 49:1-6
Zab: 138
Somo II: Mdo 13:22-26
Injili: Lk 1:57-66, 80
Nukuu:                                             
Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu,” Isa 49:1

akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa,” Isa 49:3

naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia,” Isa 49:6

Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake,” Mdo 13:24 

Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake,” Mdo 13:25

Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye,” Lk 1:66

Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli,” Lk 1:80

TAFAKARI: “Wewe si bahati mbaya.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha siku ya kuzaliwa kwake Yohane Mbatizaji. Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji kunajidhihirisha kama utangulizi wa yale atakayoyafanya Kristo kama hatua ya mwisho ya kumkomboa mwanadamu. Kwa maana nyingine, Yohane anatambulika katika Kanisa na hasa katika fumbo zima la historia ya ukombozi wa mwanadamu kama msafishaji njia, mwandaaji njia, mtoaji taarifa wa kile ambacho kitatokea. Yohane Mbatizaji anawaandaa watu kwa kumpokea Masiha na Mwokozi wa wanadamu. Hivyo basi, tafakari yetu leo utaongozwa na neno hili; “Wewe si bahati mbaya.”

Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji ni fumbo na muujiza wa pekee wa Mungu kwa wale wamtumainio. Familia ya Zakaria na Elizabeth ilihuzunishwa sana kwa kukosa mtoto kwa muda mrefu. Ila wakati ulipotimia Mungu aliyafanya yote kadiri ya mpango mzima kwa ajili ya watu wake wote. Hivyo tendo hili la kuzaliwa kwake Yohane Mbatizaji linadhihirisha maneno haya kwamba ‘hakuna aishiye ulimwengu huu kwa bahati mbaya.’ Kama umezaliwa jua wewe ni wa pekee, na Mungu anampango mkubwa sana juu yako, na ukombozi wa watu wake. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia,” Rum 14:7-9. Ni mara ngapi twajisikia vibaya wakati tunapopigwa na hali ngumu ya maisha hata tunamtusi Mungu na kumuasi? Wewe si bahati mbaya!

Somo letu la kwanza linaelezea umuhimu wa uwepo wetu katika dunia hii, na malengo yake. Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu,” Isa 49:1. Ndugu yangu, ungali bado hujazaliwa Mungu kesha fahamu jina lako na makusudi yake. Tendo hili linajitokeza wakati wa kumpatia jina Mtoto aliyezaliwa na Elizabeth. Jambo la ajabu wote wawili yaani Elizabeth na Zakaria wanapendekeza jina “Yohane” licha ya kwamba hawakuwa na mawasiliano kabla yake. Jina Yohane maana yake ni, “Mungu ndiye mwenye Neema.” Ndugu yangu, Mtume Paulo anasema, Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10. Hatuna cha kujivunia kwa kile tulicho. Kwa sababu hiyo, yapo mambo makuu matatu yatupasa kufahamu ili kujua makusudi ya Mungu katika maisha yetu hapa duniani. Jambo la kwanza ni hili; kwa hali yo yote nitakayokuwa nayo lazima nijipokee kwanza, na kwa namna hiyo ndivyo neema za Mungu zitafanya kazi ndani yangu.

Pili, Mungu hutupa majukumu ya kufanya hapa duniani. Hatupo hapa kushangaa shangaa na kujiingiza katika mambo ya watu wengine. Mtume Paulo anatoa onyo: “Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema,” 2The 3:11-13. Tupo katika ulimwengu huu wa malengo maalumu, na kupitia malengo hayo kazi ya Mungu hutendeka.  Mungu anawaambia Waisraeli na anakuambia wewe na mimi pia, “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa,” Isa 49:3. Mungu hutukuzwa tufanyapo vyema yale tunayoyaishi kadiri ya wito wetu. Wakati mwingine hatutambui wajibu huu mkubwa mbele ya Mungu kwa kuwajibika vilivyo kwenye tumishi zetu ndogondogo na wakati mwingine zile zisizo julikana rasmi na jamii.

Mfano Mama lishe anayewahudumia wachimba mifereji pembezoni mwa jiji. Yawezekana hakuna mwenye kuguswa na huduma hii hata kidogo. Ila angalia wamama lishe hawa wanavyojituma na kudamka usiku wa manane kuandaa watakavyovihudumu kwa siku. Faida waipatayo ni ndogo sana ukiliganisha na muda wanaoutumia kuwahudumia vibarua hawa walio wanyonge kama wao. Hii ni neema ya Mungu! Katika jambo hili Mungu anasema, “Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia,” Isa 49:6. Ndugu yangu, yale tujitoayo bila kujibakiza katika utume wetu, ni nuru kwa watu wa Mungu, na kwetu ni wokovu wa milele.

Ni kwa namna hii ya pekee, wakati ulipotimia Mungu anatupatia Yohane Mbatizaji kama mwaandaaji wa yule atakaye hitimisha lengo la kuukomboa ulimwengu huu kutoka utumwa wa dhambi. Huyu anayeandaliwa ni neno aliyefanyika Mwili akakaa kwetu. Huyu ndiye Kristo. Yohane Mbatizaji anawaandaa watu kwa kuwahubiria habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake,” Mdo 13:25. Je, twaweza kuwa wanyenyekevu kama Yohane Mbatizaji? Je, tupo tayari kuwaandalia wengine mazingira mazuri ya utendaji? Ni mara ngapi tunapokabidhiwa kazi twataka kuharibu vyote tulivyovikuta na wakati mwingine tuondokapo twaharibu yote tuliyoyafanya ili anayekuja asikute chochote? Je, hii ndiyo sababu ya uwepo wako katika dunia hii? Wakati mwingine tuyafanyayo hayaendani na maisha na wito wetu, na matendo hayo wakati mwingine ni heri yale ya kipagani kuliko sisi tunayemjua Kristo.

Tatu, tunapoishi hapa duniani maisha yetu yawe barua za kusomwa na wengine, na kwa kupitia barua hizo wengi wapate wokovu. Maisha yetu yaamshe mvuto wa kumfahamu Mungu na kupenda kuishi naye. Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji na maisha yake ni kielelezo cha makusudio ya Mungu kwa watu wake. Hivyo, Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye,” Lk 1:66. Je, maisha unayoishi kuna viashiria vyovyote vya mkono wa Mungu? Kama hamna ni vyema ukachunguza ukamilifu na uaminifu wa maisha unayoishi kadiri ya wito wako. Kwa Yohane Mbatizaji jambo hilo lipo wazi kwa sababu tunaambiwa hivi: Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli,” Lk 1:80. Ni vyema nijiulize swali hili: Je, hapa nilipo kadiri ya wito wangu, ninakua, naongezeka nguvu rohoni, ninamatumaini ya kukutana na Mungu kwa sadaka yangu hiyo niitoayo kila siku (katika jangwa hilo la Maisha)?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE MUNGU TWASEMA ASANTE KWA KUTUPA SABABU YA UWEPO WETU HATA DUNIANI. HATUPO KWA BAHATI MBAYA. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario