JUMATANO WIKI YA 9 YA MWAKA-B
3/6/2015
Somo: Tob 3:1-11a,
16-17a
Zab: 24:2-3a,
4-5b, 6-7bc, 8-9
Injili: Mk:
12:18-27
Nukuu:
“Sasa
unifanye utakavyo. Uitoe roho yangu, nitoweke hapa duniani,
mwili wangu na uwe tena udongo. Kwangu afadhali kufa kuliko
kuishi, maana nashutumiwa bila makosa; nimekata tamaa kabisa. Bwana, upende basi kuniondoa kwenye msiba huu, unipeleke kwenye pumziko la milele. Usinikatalie
ombi langu.” Tob 3:6
“Sitajiua
mwenyewe, hasha; nitamwomba Bwana achukue roho yangu, nisisikie tena matusi
kama yale! 11Kisha Sara alisimama dirishani, akainua mikono yake na kusali: “Utukuzwe, ee Bwana Mungu wangu; liheshimiwe milele jina lako
takatifu” Tob 3:10e-11
“Basi, maombi ya Tobiti na Sara yakakubalika mbele yake Mungu
mwenyewe, naye akamtuma malaika Rafaeli
kuwasaidia. Alitumwa kuondoa
vile vigamba vyeupe machoni mwa Tobiti ili aweze kuona tena, na kufanya mipango
ya ndoa kati ya Sara na Tobia, mwana wa Tobiti; Tobia alikuwa binamu ya Sara,
na hivi alikuwa na haki ya kumwoa Sara. Rafaeli aliagizwa pia kuliondoa lile
jini Asmodeo, lililokuwa limempagaa Sara,” Tob 3:16-17
“Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa
kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?”
Mk 12:24
“Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi,
bali huwa kama malaika walioko mbinguni,” Mk 12:25
“Yeye
si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana,” Mk 12:27
TAFAKARI: “Yeye si Mungu wa wafu,
bali wa walio hai. Mungu huwajibu wale wanaomtumainia.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, wale tu walio hai ndio wenye uhusiano wa moja kwa moja na Mungu huyu
tunayemwamini. Uhai unaosemwa hapa ni uhai wa Imani usiotia shaka kabisa juu ya
Mungu huyu tunaye mwamini, mtukuza, msifu, mwabudu na kuziimba sifa zake.
Tunayafanya haya yote si kwa mazoea, bali kwa kutambua upendo wake kwetu na
mshikamano wake kwetu usionakikomo. Hata hivyo siyo wote tunaoishi uhasilia na
ukweli huu. Kufikia hatua hii ni ukomavu wa kiroho. Wengine twaweza kufikia
hatua hii bila tatizo lolote na hata kutokutoka jasho. Wengine hufikia hatua
hii ya kuunganika na Mungu pasiposhaka baada ya kuyapitia majaribu mengi katika
maisha. Hivyo, chuma imara ni kile kilichofuliwa kwa moto mkali sana.
Ukweli huu wa maisha ya
kiroho tunaouona leo tunapotafakari juu ya majaribu ya Tobiti na Sara binamu
yake. Jana tuliziangalia zile hatua tano za kifo. Leo tuitazame kwa undani
hatua ile ya tano, yaani KUJISALIMISHA. Tunapojisalimisha vyema bila manung’uniko,
Mungu hutujibu mahangaiko yetu na huzuni zetu. Kadiri ya matatizo ya Tobiti,
licha ya kukata tamaa, ikiwa ni hatua ya nne ya kifo, tunaona kujirudi kwake
kwa kufanya toba na kuomba msamaha wa dhambi zake, na hivyo kujisalimisha vyema
kwa Mungu. Tobiti anajisalimisha kwa maneno haya; “Sasa
unifanye utakavyo. Uitoe roho yangu, nitoweke hapa duniani,
mwili wangu na uwe tena udongo. Kwangu afadhali kufa kuliko
kuishi, maana nashutumiwa bila makosa; nimekata tamaa kabisa. Bwana, upende basi kuniondoa kwenye msiba huu, unipeleke kwenye pumziko la milele. Usinikatalie
ombi langu.” Tob 3:6. Ni vizuri kujirudi pale tunapotambua kumejikwaa kwa
kumkufuru Mungu. Kujirudi huku kama Wakristo ni kuijongea sakramenti ya
kitubio, ikiwa ni ndiyo njia mahususi ya kurudisha uhusiano wetu na Mungu ambao
hubomolewa kwa dhambi.
Naye
Sara, binamu yake Tobiti, alikuwa na majaribu yafuatayo; Katika maisha yake
aliolewa mara saba, na mara zote hizo waume wake wote walifariki. Sababu ya
vifo vya waume zake hayo ilitokana na kumilikiwa wa jini Asmodeo, ambalo
liliwauwa wanaume wote walioishi naye. Leo tukio kama hili twaweza kuliongelea
kwa namna mbalimbali. Wapo wengine mara zote wanaolewa na kuachika kwa kipindi
kifupi tu bila sababu za msingi. Yawezekana kwa hali hii umeshachanja mbuga za
kutosha kwa waganga wa kienji bila mafanikio.
Wapo
wengine hawajajaliwa watoto, na kwa sababu hiyo hujiona kutokukamilika kama
wazazi. Haya ni mateso makubwa sana hasa kwa mila na desturi zetu waafrika.
Mwanamke aliye tasa ni aibu sana ukwenini. Husemwa na kunyanyaswa sana. Kwa
kweli ni karaha sana. Pamoja na mahangaiko na majaribu haya, Sara
anajisalimisha kwa Mungu, baada ya kuona hakuna sababu ya kuutoa uhai wake.
Naye anajisalimisha hivi; “Sitajiua mwenyewe, hasha; nitamwomba Bwana achukue
roho yangu, nisisikie tena matusi kama yale! Kisha Sara alisimama dirishani,
akainua mikono yake na kusali: “Utukuzwe, ee Bwana Mungu wangu; liheshimiwe milele jina lako takatifu” Tob 3:10e-11.
Wapendwa
wana wa Mungu, tunapojisalimisha kwa Mungu kikamilifu, tunajiweka mahali salama
zaidi, na kumwachia Mungu atende kadiri ya mapenzi yake. Hapa ndipo Mungu
huonyesha Mamlaka yake ambayo kwetu ni upendo usiokipimo. Mungu kamwe hawezi
kutuacha tukaangamia hasa pale tunapomtegemea yeye kuliko vitu vyote. Hawezi
kuacha tutaabike tunapokuwa hai Kiimani. Mungu wetu ni Mungu wa walio hai. Hapa
ndipo yale maneno ya Yesu hutimia, “Nami
nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi
mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye
atafunguliwa,” Lk 11:9-10.
Ni katika hali hii ya kujisalimisha pasipo shaka kwa Mungu,
Tobiti na Sara wanajibiwa mahangaiko yao. “Basi, maombi ya Tobiti na Sara yakakubalika mbele yake Mungu
mwenyewe, naye akamtuma malaika Rafaeli kuwasaidia. Alitumwa kuondoa vile vigamba vyeupe machoni mwa Tobiti ili
aweze kuona tena, na kufanya mipango ya ndoa kati ya Sara na Tobia, mwana wa
Tobiti; Tobia alikuwa binamu ya Sara, na hivi alikuwa na haki ya kumwoa Sara.
Rafaeli aliagizwa pia kuliondoa lile jini Asmodeo, lililokuwa limempagaa Sara,”
Tob 3:16-17. Tobiti anapata kuona tena, na si kuona tu, bali pia kumwona mwenzi
wa maisha yake. Sara anapewa mwanamme aliyemaliza chuo cha majaribu. Hivyo ndoa
hii itadumu nyakati zote kwa sababu wote wawili wamekwisha andaliwa na Mwalimu
mwenye viwango vyote, naye ndiye Mungu wa walio hai.
Injili yetu ya leo inakazia kipengele hiki cha kwisho, na
imebeba habari yote nzima ya tafakari yetu, kwamba, “Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Mungu
huwajibu wale wanaomtumainia.” Na zaidi ya hapo, Yesu anatufunulia uhalisia wa
maisha ya ufufuko. Tutakapofufuliwa na kuishi mbinguni naye Mungu, katika miili
yetu ya utukufu, hatutahitaji haya ya duniani; mfano kuoa au kuolewa, kula,
kulala, nk. Haya ni mahitaji ya miili hii ambayo bado haijatakatifuzwa. Hivyo
Yesu anasema, “Kwa maana
watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika
walioko mbinguni,” Mk 12:25. Ndugu yangu
umeipata hiyo?
Tumsifu Yesu Kristo!
EE MUNGU NIIMARISHE
IMANI KATIKA MAJARIBU YANGU. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario