domingo, 31 de mayo de 2015

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 9 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 9 YA MWAKA-B
1/6/2015
Somo: Tob 1:1a, 2; 2:1-9
Zab: 111:1-2, 3-4, 5-6
Injili: Mk 12-1-12
Nukuu:
            Lakini jirani zangu walinidhihaki, wakasema, “Mtu huyu bado haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hilo; ingawa alikimbia, na kumbe! Anazika maiti tena,” Tob 2:8
Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6
Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu,” Mk 12:7
“Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu,” Mk 12:8
TAFAKARI: “Upendo wa kweli ni kuwa tayari kuteseka kwa ajili ya wengine.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tulitafakari neno hili; “Upendo wa kweli ni kuwa tayari kuteseka kwa ajili ya wengine.” Ukomavu wa imani yetu unao endana na Ukristo wetu, hupimwa kwa kiwango cha upendo wetu kwa wenzetu na ule utayari wa kuteseka kwa ajili ya wenzetu. Utayari huu si ule wa kujianda kwa ajili ya kufanya kitu kizuri ya kuwasaidia wengine, bali ni kuwa tayari kwa lolote linalotokea na kujitosa kwenye jambo hilo kwa nguvu zako zote, uwezo wako wote, akili zako zote, na hata muda wako wote.
Tunaona utayari huu kutoka somo letu la kwanza, pale ambapo Tobiti anapotapa habari ya mtu kunyongwa na kutupwa sokoni. Tobiti anapata taarifa hii kupitia mtoto wake ambaye alimtuma kwa nia njema kwamba aende amtafute mtu masikini wa Taifa lao aje ashiriki naye chakula. Badala ya mtu masikini, anapata taarifa ya mtu aliyenyongwa hadi kufa na kutupwa sokoni. Binadamu hueshimiwa kutoka na utu wake, hivyo hata akifariki maiti yake huifadhiwa kwa heshima. Licha la ukweli huu, Tobiti anaenda mbali zaidi, na kufanya maiti huyu kuwa sehemu ya msiba wake. Hivyo kwa heshima zote anamzika na kukubali kuingia unajisi kutokana na upendo huu wa ajabu na kuwajibika. Majirani zake wanambeza kwa tendo hili, na kusema, “Mtu huyu bado haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hilo; ingawa alikimbia, na kumbe! Anazika maiti tena,” Tob 2:8.
Wapendwa wana wa Mungu, si mara moja tumekutana matukio kama haya, na wakati mwingine  na maiti zisizokuwa na ndugu wa karibu. Wapo kati yetu ambao mara tusikiapo habari kama hizi huguswa na kuwajibika kadiri ya uwezo wetu. Wapo wengine wanapokutana na matukio kama haya ujisemea mioyoni mwao, “jambo hili halinihusu, kila mtu na mzigo wake.” Labda nikukumbushe ukweli wa jambo hili. Hakuna binadamu yeyote aliyejizika mwenyewe. Unaweza kufanya maandalizi ya awali, mfano; kuchimba kaburi na kulipamba unavyotaka, kununua sanda, kuchonga jeneza, na mambo mengine katika hatua ya awali ya maandalizi, ila hutoweza kujibeba na kulifunika kaburini ukiwa maiti. Watu wengine lazima wakuhifadhi.
Kwa maana nyingine, tatizo lolote lile linalomkumba binadamu mwenzangu laweza kwa namna hiyo hiyo kunipata mimi mwenyewe. Hivyo hata siku moja usilipige kisogo tatizo la mwenzako. Fanya chochote kile unachoweza kukifanya, na mara nyingine saidia mapema kabla mambo hayajaharibika. Kama ni mgonjwa hangaikia kwa bidii zako zote matibabu yake, na usingoje akifa ndiyo uonyeshe upendo kwa kujitoa. Tunaona maigizo mengi sana ya wakristo ambao uthamini sana maiti kuliko uhai wa mtu. Tupo tayari kujitoa sana kwenye msiba kuliko wakati mtu huyu alipokuwa akiitaji huduma za matibabu. Haya ni maigizo ya upendo.
Katika somo letu la Injili, Yesu anatoa simulizi la historia nzima ya wokovu wetu, na kufunua  mioyoni kwa Wayahudi hitimisho la historia hiyo kwa kifo chake ambacho wao Wayahudi watakitekeleza kutokana na mioyo yao kuwa migumu kwa kutokupokea upendo wa Mungu na kuuishi.
Mungu katika kumkomboa mwanadamu alitumia njia mbalimbali na watu mbalimbali hatua kwa hatua. Lakini hapa mwishoni amemtuma mwanaye mpendwa Yesu Kristo akiamini kuwa huyu tutamsikiliza.Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6 Kinyume chake, tumejitwalia na tunaendelea kujitwalia mambo ya Mungu mwenyewe na kutaka kuwa wamiliki wa kitu ambacho kwa uhalisia na silika yetu hatuwezi.
Njia iliyorahisi mara nyingi kwa mtu mwovu ni kuchukua nafasi ya yule anayemwona kuwa ni kipingamizi chake. Kristo kwa upande wa Wayahudi na sisi sote tusiopenda kupokea na kuuishi upendo wa Mungu ni wapinzani wa ukweli huu. Kuchukua nafasi ya mpenzani wako katika maani niliyoisema ni pamoja na kumfifisha mpinzani wako, ambako mara nyingi huchukua mwelekea wa kukatisha uhali wa mtu yule. Kwa maana, ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti,” Yak 1:15. Hivyo Yesu Kristo anatabiri kifo chake na kuwaambia Wayahudi kwa mfano ule wa wakulima, wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu,” Mk 12:7. Nao wakafanya kadiri ya dhamiri zao mbovu. Ila pamoja na hila hizi za kibinadamu na za uovu, hatuwezi kufifisha upendo wa Mungu. Kristo ndiye mpango mzima wa Mungu. Hivyo, Kristo ni, “Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni,” Mk 12:10.
Wapendwa wana wa Mungu, kamwe usimtendee binadamu mwenzako ubaya. Binadamu huyu ambaye hujua familia yake, ukoo wake, kabila lake, na taifa lake anachapa ya Mungu ndani yake. Ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kutomtendea wema na haki ni kutomtendea Mungu wema na haki hiyo ambayo ni yake, na kwa kufanya hivyo uku ukijiita mwana shirika fulani la kitume, wana kikundi fulani parokia, mwana maombi, nk, ubakia kuwa upendo wa maigizo ambao mara nyingi wewe na mimi ni waigizaji maarufu.

Tumsifu Yesu Krito!


EE YESU TUJALILE UPENDO WA KWELI, NA TUWE TAYARI KUTESEKA KWA AJILI YA WENGINE. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario