JUMAPILI,
NOVEMBA 1 2015
Sikukuu
ya Watakatifu Wote
Somo
I: Ufu 7:2-4, 9-14
Zab:
24:1bc-2, 3-4ab, 5-6
Somo
II: 1Yoh 3:1-3
Injili:
Mt 5:1-12a
Nukuu:
“Na malaika wote
walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za
wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi,
wakamsujudu Mungu,” Ufu 7:11
“Hao ndio
wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe
katika damu ya Mwana-Kondoo,” Ufu 7:14b
“Tazameni, ni pendo la
namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa
sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye,” 1Yoh 3:1
“Na kila mwenye
matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3
“Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila
neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini,
na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni,” Mt 5:11-12
TAFAKARI: “Utakatifu ndiyo Cheo chako.”
Wapendwa katika Kristo, leo Mama Kanisa kwa furaha
kubwa anaadhimisha sikukuu ya Watakatifu wote. Kwa namna ya pekee kabisa mimi
na wewe leo tunakumbushwa kwamba ‘Utakatifu ndiyo Cheo chetu.’ Malengo
ya Mbatizwa yeyote ni kuwa mkamilifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo
mkamilifu. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama
Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Huu ndio wito wa kila
mbatizwa ili kulifikia taji lile la Utakatifu ambalo ndilo cheo chetu. Ni kuwa
na matumaini na Mungu na kila siku kujitakasa na kuepuka kuishi katika hatia. “Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa,
kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3
Ndugu yangu, tungali hapa dunia wengi wetu hupenda
kujipambambanua na ubora wa familia zao, koo zao, makabila yao, itikadi zao za
kisiasa na kidini na hata utaifa wao. Tukiishi katika ngazi hii tu bado
hatujajua hatma ya uwepo wetu hapa duniani. Huko Mbinguni hatutajulikana kwa
hayo niliyoyataja, bali tutajulikana kwa
usafi wetu uliotokana na UTAKATIFU wetu tuliouishi hapa duniani ikiwa ni
mahali tu pa maandalizi na kupita.
Kila mmoja wetu aweza kuwa Mtakatifu. Utakatifu wako ni
matokeo ya kuwa mwaminifu kwa mambo madogo madogo ya kila siku, na kuyafanya
hayo kwa ukamilifu wake. Ni kuwa tayari kumpa Kristo nafasi ndani ya moyo wako
ili atende kazi nawe kwa yale yanayompendeza Mungu na jirani yako. Utakatifu
wako ni tokeo pia la kufungua milango kwa wote wenye uhitaji bila kujali
historia zao na mapungufu yao. Ni kujaribu kufanana na Yesu katika kuwaza,
kutathmini na kutenda. Tunapokuwa karibu na Kristo ndivyo tunavyofunuliwa siri
za Baba yetu wa mbinguni na ufalme wake.
Ukaribu huu niliousema, utufanya kuwa watoto wapendwa wa
Mungu katika utii usio shuruti. Tunatii kwa sababu Mungu anatupenda na
anatutakia mema katika ukamilifu wake. Ndugu yangu, “Tazameni, ni pendo la
namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa
sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye,” 1Yoh 3:1. Maisha
haya ya utakatifu yatatudai kila siku kusimama katika kweli na haki, na wakati
mwingine tutapimwa Imani yetu.
Kupimwa
huku kwa Imani kwa weza pia kutuondolea uhai wetu. Basi hili litakapotokea
yatupasa kuyasema maneno haya pasipo shaka yoyote, “kwangu mimi kuishi ni
Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21. Ni kuyaona yote yaliyofaida kwako ni
hasara kwa ajili ya Kristo, Flp 3:7. Tunapoyaachia maisha yetu katika kiwango
hiki, Kristo kamwe hawezi kutuacha katika taabu hizo. Kristo hubaki kuwa faraja
kubwa kwetu katika dhiki na taabu hizo. Naye anatuambia nyakati kama hizo tuwe
watu wa kufurahi kwa sababu tunamruhusu Mungu kutenda mambo katika hali yetu ya
uduni na Mateso. “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila
neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini,
na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni,” Mt 5:11-12. Je,
wayafurahia mateso yako?
Mtawa mmoja wa kiume katika Monasteri fulani alijijengea
ukaribu sana na Yesu wa Ekaristi Takatifu. Mtawa huyu alikuwa mpishi wa muda
mrefu katika Monasteri hiyo. Aliipenda sana kazi yake na kwake ilikuwa moja ya
kumtukuza Mungu kupitia huduma hii kwa wanajumuiya wenzake. Kamwe hakuwahi
kunung’unika hata pale ambapo kazi zilikuwa nyingi.
Kila asubuhi Mtawa huyu mara baada ya masifu ya asubuhi na
Misa Takatifu, huenda bustanini kuchuma mboga na vitu vingine kama maandalizi
ya chakula cha Mchana na jioni. Bustani ile ilikuwa baada ya kulipita Kanisa.
Hivyo alijiweka ahadi ya kuongea na Yesu wa Ekaristi Takatifu kila siku kabla
ya kufika bustanini.
Siku moja akiwa na kikapu chake na kisu aliingia Kanisani
na kuanza kusali na kutafari mbele ya ‘Terbenakulo,’ Sehemu zinapohifadhiwa
Hostia Takatifu. Mara alishtushwa na sauti ya kengele ya Malaika wa Bwana,
iliyoashiria pia ni muda wa chakula cha mchana. Mtawa huyu aliingiwa na hofu
kubwa sana kwani alikuwa bado hata bustanini hakuwa amefika.
Mtawa huyu aliondoka kwa haraka ili awahi kuomba msamaha
kwa watawa wenzake kwa kutokuandaa chakula kile cha mchana. Maajabu ni kwamba
alipofika tu eneo la jikoni alikaribishwa na harufu nzuri sana ya chakula na
kusikia watawa wenzake wakimsifu kwa chakula kitamu alichoandaa. Kila mmoja
alitaka kuongea naye na kumpa asante kwa kazi nzuri aliyofanya.
Akiwa ameshika kikapu chake na kisu ndani yake, alionekana
akitokwa na machozi ya furaha huku akisema “asante Yesu kwa kuniona na
kuniondolea aibu hii.” Watawa wote walibaki midomo wazi! Ndugu huyu alisimulia
yote yaliyotokea. Jumuiya yote ilijawa na furaha na kumtukuza Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu, tunapokuwa karibu na Mungu, kamwe
hawezi kutuacha. Mungu atatupigania hadi mwisho. Hivyo tuwe waaminifu na
kufanya yote kwa ukamilifu tukimtanguliza Mungu kwa kila kitu. Mtume Yakobo
anatuambia siri hii kwa kusema, “Mkaribieni Mungu,
naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na
kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili,” Yak 4:8. Haya ndiyo maandalizi ya
cheo chako, yaani, Utakatifu wako.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Hao ndio wanatoka
katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika
damu ya Mwana-Kondoo,” Ufu 7:14b
No hay comentarios:
Publicar un comentario