sábado, 3 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 27 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 27 YA MWAKA-B
4/10/2015
Somo I: Mwa 2:18-24
Zab: 127:1-5
Somo II: Ebr 2:9-11
Injili: Mk 10:2-16
Nukuu:
Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake,” Mwa 2:21 

na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu,” Mwa 2:22

Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume,” Mwa 2:23 

Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja,” Mwa 2:24

Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso,” Ebr 2:10 

Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake,” Ebr 2:11 

Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii,” Mk 10:5

Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke,”Mk 10:6 

Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja,” Mk 10:7-8 

TAFAKARI: “Yesu Kristo haoni haya kutuita ndugu zake hata kama tunaishi kinyume cha maagano yetu kimaisha kwa sababu kwa neema ya Mungu ameonja mauti kwa ajili ya kila mtu.”

Wapendwa sana wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 27 ya mwaka “B” wa Kanisa. Kwa namna ya pekee Mama Kanisa kupitia masomo yote matatu ya leo anatutaka tuonje upendo wa Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo, hasa kwenye maagano yetu ya Maisha, hususani Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Sakramenti ya ndoa Takatifu ina upekee wake kwa mtazamo huu: ni Sakramenti ambayo wahusika wote wawili ndiyo wakufunzi wa ndoa hiyo. Ni maajabu ya Mungu katika upendo na makusudio yake kwamba muunganiko huu wafanywa imara licha ya tofauti za kimalezi na makuzi ya kila mwanandoa.

Siri na fumbo la sakramenti hii Takatifu ipo kwenye makusudio ya uumbaji wa mwanaume na mwanamke. Mungu baada ya kuumba vitu vyote na katika uzuri wake, aliona bado kuna kitu ambacho si sawa. Hivyo kwa upendo wa ajabu wa Mungu Baba anayafanya haya; Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake,” Mwa 2:21. Kilichotolewa kwa Adamu, yaani upavu, ndiyo uwepo wa Mwanamke. Kwa maana hiyo mwanamke ni kile kilichotoka wa Adamu. Tendo hili ndilo linalowaweka pamoja na kuwa mwili mmoja. Hivyo,  na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu,” Mwa 2:22. Wataalamu wa hesabu wanatuambia kwamba moja jumlisha na moja ni mbili, ila kwa hesabu hii, Mungu katika fumbo hili ya ndoa, anatufundisha kwamba moja jumlisha moja ni moja. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja,” Mk 10:7-8. Umoja huu ni wa ajabu sana unaotuelekeza kutafakari upendo wa Mungu katika Sakramenti hii na fumbo zima la Sakramenti ya ndoa.

Katika dunia hii walitokea watunzi wazuri sana wa tenzi mbalimbali hata leo bado wapo watunzi wa tenzi hizi, ila haijatokea mtuzi mzuri wa tenzi za rohoni kama Adamu. Fumbo hili la mwanamke kutoka kwa mwanaume lina ibua hisia za ndani za Adamu na yeye bila kujizuia anayasema haya ya moyoni: “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume,” Mwa 2:23. Hakuna neno lingine zaidi ya maneno haya ya Adamu yanayoweza kuonyesha furaha aliyokuwa nayo Adamu baada ya kupewa msaidizi wake. Kama huu ni ukweli, iweje basi tunaona leo ndoa hazidumu? Kwa nini basi ndoa zimekuwa za majaribio? Nafasi ya Baba na Mama katika ndoa leo ipo wapi? Mbona tunaona kila mmoja akijifanyia mambo yake hata kama ndoa hiyo bado yaesabika kuwepo?

Wapendwa tatizo kubwa leo katika ndoa ni kwamba NDOA halichukuliwi katika UTAKATIFU wake bali kama mazoea na mfumo wa kawaida wa kijamii, kwamba muda ukifika na jamii ikiona inafaa basi yanipasa kuona kuwa na mke, au kuolewa kuwa na mume. Mambo yamekuwa ya KIMWILI zaidi kuliko KIROHO. Ndoa nyingi leo zinapofungwa Makanisani au sehemu nyingine kwenye vyombo vya sheria kama mahakamani,  zimekuwa maigizo makubwa. Ni maigizo makubwa katika mtazamo huu wa kiroho: anayefunga ndoa, yaani kuoa au kuolewa unakuta kesha kuwa na mahusiano hayo kimkataba na wanaume wengi au wanawake wengi. Huyu anayefunga naye ndoa sasa ndiye anayejulikana rasmi katika jamii kwa sababu kaamua kujulikana hivyo kutokana na matakwa ya jamii husika na siyo maisha ya ndani ya kiroho. Ndoa hii haiwezi kudumu kwa sababu inaingia katika mgogoro wa kimahusiano kiroho uliokwishwa kufanywa awali na wanaume au wanawake wengi. Madhara ya kufanya uzinifu kabla ya ndoa kama Sakramenti ni tatizo kubwa kwa maisha ya ndoa husika.

UZINZI ni:-Kufanya tendo la ndoa kabla ya ndoa na nje ya ndoa baada ya ndoa au ni kufanya ngono na mtu asiyekuwa mke au mume wako. Unapozini ni sawa na kuuchukua mwili wako na kuunganisha na mwili wa mtu mwingine “nao watakuwa mwili mmoja” (Mwa. 2:24b). Kwa hiyo kadri unapozini na watu wengi ndivyo unavyozidi kuugawa mwili wako na unajijeruhi zaidi. Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja,” 1Kor 6:16. Hiki ni chanzo kikubwa sana cha maumivu ya ndani kwa wanandoa.

Hivyo aliye zini kabla ya kuoa au kuolewa, katika ulimwengu wa kiroho anakuwa ameugawa mwili wake kwa hao aliozini nao. Na hivyo ndani ya mwili wake anakuwa amebeba miili ya watu wengine. Sasa wakati mtu huyu anapooa au kuolewa, ndoa yake inakuwa ya shida na ugomvi mwingi kwa sababu anakuwa si mkamilifu kimwili na anakuwa tayari amejigawa sehemu mbalimbali na amebeba miili ya watu wengine. Hapa ndipo tunaposhangaa na kuona mwanamme anamwacha mke wake mzuri na wa kuvutia na kutembea na vigaragosi vya ajabu. Vile vile hapa ndipo tunaposhangaa kumwona mwanamke anatoka kwenye ndoa yake na kutembea na vibaka wa ajabu kusimuliwa. Je hatujui kwamba, “kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini?”

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na mapungufu hayo kibinadamu bado tunao uponyaji tunapojisalimisha ndani na katika Kristo. Kama vitu vyote vimekuwepo kupitia Kristo ni kwa njia yake vitu hivyo hutakaswa kupita yeye mwenyewe. Hivyo uponyaji wetu upo kwa Kristo peke yake. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso,” Ebr 2:10. Je, tupo tayari kuona ukweli huo ndani yetu ili tuponwe na Kristo? Mara nyingi kinachozuia uponyaji wetu ni pale tunapoona aibu kujipokea kama tulivyo. Hakuna maana yoyote kuendelea kujipulizia uturi ili hali ndani yetu kuna ufundo wa harufu kali sana. Yesu pamoja na kubeba aibu yetu, haoni haya kutuita ndugu zake. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake,” Ebr 2:11. Waswahili wana sema hivi, “msificha uchi hazai.”

John na Mary walikuwa na wakati mzuri sana na ndoa yao ya miaka minne. Hakika Mary alijiona mwanamke aliyependwa sana na mme wake na kubarikiwa sana na Mungu. Hivyo siku moja  alitaka kumfanyia “surprise” mume wake. Aliamua kununua “line” nyingine tofauti ya simu ili akiwa nyumbani ampigie mume wake.

Kama ilivyokuwa kawaida, Mume wake, yaani John baada ya kurudi kazini njioni huwa sebuleni akitazama mpira au tamthilia huku mkewe Mary akiwa jikoni anaandaa chakula cha jioni.
Mara Mary akampigia mmewe siku kwa namba ile mpya. “Hello Mpenzi wa moyo wangu. Mbona leo upo kimya sana? Kulikoni?” Mary aliongea kwa sauti nyororo kupita kiasi. “Ok, nimekuelewa Darling. Nipo nyumbani na “Asha Ngedere” kanibana mbaya sana. Nitakutafuta baadaye honey wangu.” John alikata simu haraka kwa woga kwamba mke wake aliyekuwa jikoni angesikia mazungumzo yale.

Mary hakuamini masikio yake, hivyo alimtumia ujumbe wa maneno, “Message,” nao ulikuwa hivi, “MBONA SIKUELEWI?” Mara John akajibu, “nimekuwambia nipo na mke wangu kanibana kama mpira wa kona. Nitakutafuta baadaye baby.”

Basi, baada ya kula na wakiwa kitandani, wote wakiwa simu zao zipo “silence,” John alimtumia ujumbe yule aliye mpigia na kumtumia ujumbe. “Bila shaka naongea na Monica. Mbona tulishamalizana ile “issue” ya gari? Please baby, usiniharibie ndoa yangu. Nipo naye kitandani. Kesho jioni tutaonana pale pale Corner Bar,” John alituma ujumbe.

Mara baada ya dakika tano hivi, Mary mkewe John, aliamka kitandani na kuwasha taa. John alishtuka kwa sababau haikuwa kawaida ya Mary kufanya hivyo. “Embu niambie mume wangu mpenzi, huyu Monica ni nani?” Mary alitaka kujua ukweli wa huyo Monica huku akimuonyesha mumewe zile “message.”

John macho yalimtoka kama mjusi aliyebanwa na mlango! Kisha John alimdondokea miguuni mke wake na kumwomba msamaha huku akisema, “hapa sina cha kujitetea mke wangu. Kama kukamatwa umenikamata vizuri. Naomba unisamehe na kesho nitakuonyesha huyo Monica na baada ya hapo ndio utakuwa mwisho wa mimi na Monica,” Mary akamjibu, “Basi tulale mme wangu ila sina furaha nawe kwa sana!”

Wapendwa wana wa Mungu, ndoa ni fumbo na yawapasa wana ndoa kusomana tabia kila siku hadi mwisho wa maisha yenu. Na msamehane kweli pale mmoja wenu anapokiri udhaifu wake. Msaidie kweli mwenzako wa ndoa kuwa imara unapoona ni dhaifu katika mambo fulani ndani ya ndoa yenu. Mpe moyo mwenzako wa ndoa kufanya vizuri zaidi pale anaposhindwa kufikia malengo yake sawa sawa.

Tumsifu Yesu Kristo! 


“Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” Ebr 13:4

No hay comentarios:

Publicar un comentario