ALHAMISI WIKI YA 27 YA MWAKA-B
8/10/2015
Somo: Mal 3:13-4:2a
Zab: 1:1-4, 6
Injili: Lk 11:5-13
Nukuu:
“Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na
waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia,” Mal 3:18
“Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru;
na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile
inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala
tawi,” Mal 4:1
“Lakini kwenu ninyi mnaolicha
jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake,” Mal 4:2
“Nami nawaambia,
Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa,” Lk
11:9
“Kwa kuwa kila aombaye
hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa,” Lk 11:10
“Basi, ikiwa ninyi
mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni
hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” Lk 11:13
TAFAKARI: ““Kwa kuwa kila aombaye
hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.”
Wapendwa wana wa Mungu, maneno haya ya
Yesu kwetu leo ni uzima kwani yeye ndiye njia, kweli na uzima wetu. Naye
anasema, “kwa kuwa kila aombaye
hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa,” Lk 11.10. Lakini
mara nyingi hatuyapati yale tuyaombayo si kwa sababu Mungu hasikii maombi yetu,
bali Yeye mwenyewe anajua ni wakati gani ufao kutupatie kile tuombacho. Kwa
hiyo yatupasa kudumu katika maombi bila kukata tamaa. Kwa upende mwingine hatuyapati
yale tuyaombayo kwa sababu hatujui kuomba vizuri. Mtume Yakoba anatuambia hivi;
“Hata mwaomba,
wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3.
Kuomba kwetu tusilenge tu katika ubinafsi wetu. Sala uombayo ilenge pia makundi
mengine yenye mahitaji kama yako.
Kutokuwa na msimamo katika sala ni
tatizo kubwa sana katika kufunguliwa kwetu kwa yale tuyaombayo. Uvumilivu katia
sala ni muhimu sana wa. Tunapokosa utulivu wa ndani ni rahisi kubebwa na kila
wimbi au upepe. Mtu yeyote anayeruhusu hali hii maombi yake huwa ya majaribio
na kumfanya kuhama kutoka Kanisa moja kwenda lingine. Hali inapoota mizizi
humfanya pia kutoka imani moja kwenda nyingine. Mtu huyu anachotafuta ni upako
kwa kubahatisha bahatisha. Mungu wetu sio wa kubahatisha.
Mwisho wa siku mtu mwenye mwelekeo huu
wa Imani huishia kutokuamini kabisa. Hukosa imani kabisa na Mungu aliyekuwa
anamwamini mwanzo na kuishia kuwa asiyeamini chochote. Hali hii ndiyo
tunayoiona katika somo letu la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Malaki. Hata
katika hali hii, Mungu ubaki kuwa Mungu wa huruma, upendo, kweli, haki, na
amani. Yakupasa kumrudia na kujisalimisha kwake. Mungu wetu mara zote hupenda
kuanza upya nasi pale tunapojisalimisha kwake. Tunapojisalimisha
kwake Mungu wetu hashikamani na historia yetu ya zamani. Ingekuwa hivyo basi
hakuna yeyote kati yetu angeweza kusimama mbele yake. Kama anavyotukumbusha
Mzaburi kuhusu huruma na upendo wa Mungu, “Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3. Kumbe kufanikiwa katika maombi ni
kujisalimisha bila kujibakiza. Ni kumrudia Mungu kusikokuwa na shaka yo yote. “Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya
wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia,”
Mal 3:18. Kumrudia Mungu huku kusiwe kwa maneno tu, bali kwa matendo yakibeba
mfumo mzima wa maisha yetu.
Je, kuna usalama wo wote wa kutomrudia Mungu na kujisalimisha
kwake? Kwa jeuri na kiburi cha mwanadamu aweza kudumu nacho kwa muda mfupi tu
wa maisha yake. Mwisho wa kiburi cha mwanadamu ni kihama. Kwa nini basi
usitumie muda na dakika zilizobaki kumtafuta Mungu wa kweli na kujisalimisha
kwake? “Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka
kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa
makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata
haitawaachia shina wala tawi,” Mal 4:1. Hakika Mungu atalifanya zoezi hili kwa
kweli na haki. Hakuna ye yote kati yetu atakaye sema hakupewa muda, wala
kaonewa.
Je, wenye hofu ya Mungu wana nafasi gani kwa kujisalimisha
kwao? Hakika Mungu hataacha kamwe kuwanyeshea mvua ya neema na baraka wenye
hofu ya Mungu. Wenye hofu ya Mungu kwa kuishi kwao kuliko kweli na haki
watasitawi katika haki na kweli ya Mungu. Mungu humwelekea mwenye hofu naye kwa
sababu ndani yake kuna unyofu wa moyo.
Huku ndiko kusitawi mbele za Mungu kuliko haki. Hivyo, “mwenye haki
atasitawi kama mtende, atakua kama mwerezi wa Lebanoni,” Zab 92:12. Mungu
hawezi kukaa kimya kwa wonyofu wa moyo. Hakuna alichaye jina la Mungu, naye Mungu
akaziba masikio ya kilio chake. “Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki
litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake,” Mal 4:2. Yatupasa kudumu katika
sala na maombi yetu tukiwa na matumaini kwamba tumekwisha pata kile tuombacho.
Somo letu la Injili linafafanua vizuri dhana nzima ya wanyofu
wa moyo na kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Hawa ndio waliomfanya Mungu kuwa
kimbilio lao. Hawa ndio wale wasiokuwa na mbadala wa maisha yao zaidi ya Mungu
katika shida zao. Hawa ndio Yesu anaowaambia, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni,
nanyi mtafunguliwa,” Lk 11:9. Huu ndio uhusiano wa Mungu na aliyemnyofu wa
moyo. Mungu kamwe hatosita kutokumhesabia haki katika kweli. “Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye
huona; naye abishaye atafunguliwa,” Lk 11:10. Ni kweli hata aliyekatili aweza
kutoa bila upendo kwa yule anayemsumbua, lakini mwenye kupenda hawezi kuacha
kutoa. Mungu wetu ni upendo na anajua mahitaji yetu yote. Naye Yesu anaufunua
upendo huu wa Mungu kwetu kwa kusema, “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu
vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao
wamwombao?” Lk 11:13. Ndugu yangu tuliosafiri
wote katika tafakari hii, jisalimishe
kwake aliye Mungu wa kweli, upendo, haki na amani.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Lakini
mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 24:13
No hay comentarios:
Publicar un comentario