jueves, 1 de octubre de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 26 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 26 YA MWAKA-B
2/10/2015
Somo: Bar 1:15-22
Zab: 78:1-5, 8-9
Injili: Mt 18:1-5, 10, 12-14
Nukuu:
“Tumemwasi, wala hatukuitii sauti ya Bwana Mungu wetu, kwenda katika sheria zake alizoziweka mbele yetu,” Bar 1:18

“bali tulikwenda kila mtu katika mawazo ya moyo wake mbaya, kutumikia miungu ya kigeni na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana Mungu wetu,” Bar 1:22

akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3

Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4

 Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 18:10

“Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee,” Mt 18:14

TAFAKARI: “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu,” Mit 11:2

Wapendwa wana wa Mungu, unyenyekevu ni msingi wa fadhila zote. Unyenyekevu unatulazimu kuujua ukweli ulivyo ndani ya nafsi zetu na kujua ukweli wa udhaifu wetu. Hatua kiroho hii utupa nguvu ya kuishi kile tulicho kadiri ya mapenzi ya Mungu. Hakika unyenyekevu wa mtu ni furaha kubwa sana ya Mungu. Ni furaha ya Mungu kwa sababu tunakuwa binadamu kweli katika sura na mfano wake Mungu. Hivyo, “Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli,” Isa 29:19. Mtu asiye mnyenyekevu hujikweza na kujiinua pasipo mastahili yake. Asiye mnyenyekevu ni vigumu sana kujishusha kunako elekea kujifunza. Asiye mnyenyekevu ni mpumbavu anayeshupalia ujinga hata kama kesha eleweshwa ukweli wa mambo. Kinyume chake wanyenyekevu hujaliwa neema ya Mungu. Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu,” Yab 4:6.

Wapendwa wana wa Mungu, mnyenyekevu husimamia haki katika kweli kwa sababu msingi wa fadhila zote ni unyenyekevu. Mnyenyekevu hawezi kudongoka katika laana ya uovu wo wote. Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki. Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema,” Mit 3:33-34. Unyenyekevu hutujengea nidhamu ya hali ya juu. Unyenyekevu utupelekea kupokeana kama tulivyo na kusaidiana kufikia malengo tarajiwa ya kila mmoja wetu. Unyenyekevu utufikirisha kabla ya kutenda jambo lo lote katika maisha. Unyenyekevu hutufanye kuwa watii na wapole hata pale mantiki ya ufahamu wetu inaposhindwa kukubaliana na ukweli kama ulivyo hasa katika joto la ujana wetu. Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5. Unyenyekevu wa mtu ni ukweli wa Mungu ndani ya mtu huyo.

Wapendwa wana wa Mungu, ni katika mtizamo huu tunaweza kuona pale ambapo hapana unyenyekevu binadamu alijifanyia yake, na Mungu alijiweka pembeni. Kiburi cha binadamu ni chukizo kubwa sana kwa Mungu. Kuishi katika kiburi siyo makusudio ya uumbaji wetu. Wana wa Israeli wanatambua tatizo hili na kwa vinywa vyao wanasema,  “Tumemwasi, wala hatukuitii sauti ya Bwana Mungu wetu, kwenda katika sheria zake alizoziweka mbele yetu. Bali tulikwenda kila mtu katika mawazo ya moyo wake mbaya, kutumikia miungu ya kigeni na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana Mungu wetu,” Bar 1: 18, 22. Hakuna neema na baraka pale tunapotawaliwa na kiburi. Mwenye kiburi ni vigumu sana kujipokea na kupokea ukweli ambao hauendani na mfumo mzima wa kufikiri kwake.

Katika Injili ya leo, Yesu anamfananisha mtu mwenye unyenyekevu kama mtoto. Mtoto mdogo hana cha kujikuza zaidi ya kuyaona yote na katika yote kwa wazazi wake. Mtoto huweka uaminifu mkubwa sana kwa wazazi wake. Wazazi wake huwa kila kitu kwake. Ni katika mtazamo huu Mungu wetu ni kila kitu kwetu. Hatuna cha kujikweza mbele zake “kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu,” 1Kor 1:25. Ni katika ukweli huu Yesu anawaambia wanafunzi wake maneno haya mazito, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3. Tusipojivua kujua kwetu kusikokuwa na maana yo yote zaidi ya mbwembe tu, hatutaweza kufunuliwa siri za mbinguni.

Unyenyekevu wenye mfano wa utoto ndio huo unaotufanya wakubwa mbele ya uso wa Mungu. Ukubwa huo siyo ule wa kufanya tutakayo sisi na kuzirithisha nafsi zetu, bali kuyafanya yote kadiri ya mpango wa Mungu. Kuujua mpango wa Mungu ni pale tu tunapokuwa tayari kujinyenyekeza mbele zake. Hivyo, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4. Katika ufalme huu wa mbinguni hakuna maguvu ya kutalawa au kutawaliwa, bali nguvu ya UPENDO wa kweli.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, wanyenyekevu wana sauti kubwa sana mbele za Mungu. Mtu ye yote anayemdharau mtu mnyenyekevu kwa vile anayafanya yote hayo kwa kujishusha yu na hatia kubwa sana mbele za Mungu. Yesu anatuambia,  Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 18:10. Hivyo tujiadhari sana na jeuri yetu ya pesa, madaraka, umaarifu na kutambulika kwetu katika jamii. Haya yote mwisho wa siku hayana msaada wo wote katika umilele wetu. “Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee,” Mt 18:14. Hivyo basi, kwa utajiri nilio nao, kwa madaraka niliyo nayo, kwa umaarufu nilio nao, na kwa kutambulika kwangu katika jamii, yanipasa kuwa sauti ya wasio na sauti.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU, TUJALIE HEKIMA YA KUONA UKWELI KAMA ULIVYO, FADHILA YA UNYENYEKEVU KUJIONA KAMA TULIVYO, NA NEEMA YA MSAMAHA TUISHI PASIPO HATIA KWETU NA KWA WENZETU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario