JUMANNE WIKI YA 27 YA MWAKA-B
6/10/2015
Somo: Yon
3:1-10
Zab:
129:1-4, 7-8
Injili:
Lk 10:38-42
Nukuu:
“Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari
nitakayokuamuru,” Yon 3:2
“Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti
yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa,” Yon 3:4
“Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga,
wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo,” Yon 3:5
“Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti
chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika
majivu,” Yon 3:6
“Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe,
wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia,
mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila
mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake,” Yon 3:7b-8
“Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya.
Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende,”
Yon 3:10
“Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na
kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi,” Lk 10:41
“lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu
amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa,” Lk 10:42
TAFAKARI: “Usalama wa maisha yetu baada ya kukengeuka ni kufanya toba ya
kweli.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kukengeuka kiimani ni kuiacha njia ya Mungu, kuacha mafundisho
na miongozo ya maisha ya kiroho. Ni maisha ambayo mtu anajichagulia na
kujifanya yeye kuwa yote katika yote. Kwa maneno mengine ni kuasi Imani yako.
Kuasi au kugeukia njia mbaya kiimani, mtu anaweza kufanya kwa kujua kabisa na
kuliko wazi, yaani kuikana imani yake hiyo hadharani, au kwa kutokujua na pole
pole kujidhihirisha katika matendo na namna yake ya kuishi. Kwa kuishi kwake
mtu huyu siyo tu haamini, bali hataki hata kusikia habari hizo.
Hivyo katika
somo letu leo kutoka Nabii Yona tunaona ni kwa namna gani watu wa Ninawi
walivyokengeuka na kuishi visivyompendeza Mungu. Yona anatumwa kwa watu hawa
kufikisha ujumbe wa Mungu. “Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari
nitakayokuamuru,” Yon 3:2. Habari yenyewe ni kuacha njia zao mbaya na kumrudia
Mungu. Mara nyingi binadamu anapokataa uwepowa Mungu katika maisha yake, mwisho
wa usalama wake unakuwa matatani. Yapo mambo mengi binadamu kafichwa kuhusu
uhai na maisha yake kwa ujumla. Mfano; ukweli kuhusu kifo, ukweli kuhusu
sintofahamu ya maisha yake hata kwa sekunde moja ijayo, ukweli kuhusu matukio
ya kutisha yanayotokana na nguvu za asili “Nature,” nk. Pasipo na shaka yoyote
ile hali hii inataka kutuambia kitu kuhusu nguvu fulani iliyopo nje ya uwezo wa
mwanadamu na yale yote yanayomzunguka. Hapana shaka pia kwa jicho la Imani,
nguvu hii ni uwepo wa Mungu anayeyaratibisha yote kadiri ya uwezo ma mamlaka
yake.
Kujirudi au kurudi kutoka njia mbaya ni kufanya ukiri wa
kweli. Kujitambua huku kiimani ni kufanya toba ya kweli. Kwa kufanya tendo hili
Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, ambayo tangia mwanza ni kuwa na uhusiano
mzuri na viumbe vyake. “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani
kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote
wafikilie toba,” 2Pet 3:9. Baada ya kuupokea ujumbe wa Yona, watu wa Ninawi
waliifanya toba yao kama ifuatavyo, “Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga,
wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo,” Yon 3:5.
Ishara zote zinazobeba tendo hili la toba zinatuelekeza kwenye huruma ya Mungu
baada ya ukiri wa ndani wa yale yaliyopelekea kuvunjika uhusiano wetu na Mungu.
Kilio cha toba licha ya kwamba chaweza kufanywa na yeyote kwa
kujifahamu baada ya kufuata njia zake na hasara zake, tendo hili linapofanywa
na jamii nzima linakuwa na nguvu sana. “Kwa kuwa walipo wawili watatu
wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao,” Mt 18:20. Kwa
uzito wa jambo hili, Mfalme wa Ninawi anahamasika na kutoka katika kiti chake
cha ufalme. “Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti
chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika
majivu,” Yon 3:6. Kama kiongozi kujitoa
katika kiti cha enzi ni kukubali mabadiliko yanayopelekea usalama wa wale
unaowaongoza. Ni kukubali kama kiongozi umechangia tatizo, na upo tayari kuanza
upya na watu wako katika yale yaliyomema na kwa manufaa mapana ya Taifia lako.
Ni
viongozi wachache sana wanaojitambua hasa pale wanapoambiwa mambo hayapo sawa,
na watu wanateseka. Kwa upande wa nchi zetu za Afrika bado hatuna utaratibu wa
viongozi kukubali kuchoka kwao na kuwa sababu ya mateso ya watu wao. Wapo
tayari kufa na tai zao shingoni, yaani, kutokuachia madaraka, licha ya kwamba
hali ni mbaya sana kwa kila nyanja. Hawa ni viongozi wanaochukua nafasi ya
Mungu na kuwa sababu ya mateso na dhiki kwa wananchi wao. Mfalme wa Ninawi
aliposikia ujumbe ule wa Mungu kupitia Nabii wake Yona, alitoa tamko kwa watu
wake: “Mwanadamu asionje
kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala
wasinywe maji; bali na wafunikwe
nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam,
na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake,”
Yon 3:7b-8. Huku ndiko kuwa na maarifa kama kiongozi wa watu. Kukosa maarifa
kumewatesa wengi sana, hata sasa watu wa Mungu wanateseka kwa viongozi wao na
wale wanaongozwa kukosa maarifa. Naye Mungu anasema, “kwa sababu hiyo watu
wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo
wana njaa, na wengi wao waona kiu sana,” Isa 5:13. Kujielewa ni hatua muhimu
sana kuelekea njia iliyo njema na salama. Ni pale tu wana wa Ninawi
walipojielewa Mungu akaurudisha uhusino wake nao uliovunjika kutokana na
kukengeuka kwao. “Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya.
Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende,”
Yon 3:10. Huku ndiko kujisalimisha kwa kujielewa. Hapa ndipo iliposalama yetu
inayojengwa na ufahamu wetu wa kweli wa Mungu yule tunayemtumikia.
Katika somo la Injili ya leo, Mariamu ndugu yake Martha
anajielewa na kumfahamu yule anayemtumikia aliye kweli katika yote, na mwisho
anajisalimisha kwake. Yawezekana mimi na wewe tumeyapa maisha yetu kipaumbele
chake cha kwanza katika kujishughulisha katika mambo mengi yasiyo na mwelekeo.
Maisha yetu hayajengwi kwa wingi wa vitu tunavyofanya, bali uelewa wa yale
tunayoyafanya, na kwa nini tunafanya kama tunavyoyafanya. Martha kama tulivyo
wengi anajilinganisha na yale anayofanya na kukosa muda wa kujua chanzo ya yale
yote tunayoyafanya na kwa nini tunayafanya kwa namna hiyo, na ni nani
anayeyaratibisha. Martha anamlalamikia Yesu kwa nini Mariaumu ndugu yake hamsaidii.
Yesu anamkumbusha Martha jambo la muhimu na kusema, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa
ajili ya vitu vingi,” Lk 10:41. Furaha yetu haitokani na vitu tunavyofanya.
Kujishughulisha huku katika maana ya kufanya hivyo tu, kutatuletea mfadhaiko
mkubwa sana.
Maisha yetu yanamaana kwanza kabisa tunapojitambua na
mwisho kujisalimisha muda wote kwa yule atupaye uzima wa milele. Huyu ndiye
chanzo cha furaha yetu na umilele wa maisha yetu. Kwake yatupasa kutumia muda
mwingi naye. Huyu ndiye Kristo; njia, ukweli, na uzima wetu, Yoh 14:6. Kuwa na
Kristo ni kuchagua fungu lililo jema ambalo kwalo hatuwezi ondolewa. Ukweli huu
ndio Yesu anaomwambia Martha na sisi leo kwamba pamoja na yote tuyafanyayo, “lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu
amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa,” Lk 10:42. Kukaa chini ya
miguu ya Yesu ni ule utayari wa kulishwa neno la uzima, na kujazwa ufahamu na
kufunuliwa siri ya uzima wa milele. Tumeumbwa tuishi Milele.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE BWANA TUFUNULIE KWELI YAKO KILA SIKU. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario