martes, 20 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 29 YA MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 29 YA MWAKA-B
21/10/2015
Somo: Rum 6:12-18
Zab: 124:1b-3, 4-6, 7-8
Injili: Lk 12:39-48
Nukuu:
Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake,” Rum 6:12

Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema,” Rum 6:14

Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki,” Rum 6:16

na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa haki,” Rum 6:18 
Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu,” Lk 12:40

“Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo,” Lk 12:43
“Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana,” Lk 12:47 

Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo,” Lk 12:48a

“Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi,” Lk 12:48b 

TAFAKARI: “Jiwekeni tayari, kesheni mkiyatenda mapenzi ya Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, injili yetu ya leo inakazia sana kuwa tayari muda wote kwa sababu hatujui siku ya kutoka kwenye ulimwengu huu. Hivyo kuwa katika mikono salama ni kukesha katika utumishi wa haki katika kutenda mapenzi ya Mungu.Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu,” Lk 12:40. Jambo la msingi kupita yote katika kesha letu ni kuishi katika hali ya neema, yaani, kutokuwa na hatia juu ya dhambi. Mtume Paulo anakazia sana swala hili ikiwa ndiyo njia pekee ya kupata kibali mbele ya Mungu na kuhesabiwa haki. Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake,” Rum 6:12. Maisha ya mtu wakati mwingine huongozwa na tamaa za mwili wake pale nafsi yake inapoegemea zaidi katika mwili.

Wapendwa wana wa Mungu, nafsi inapoegemea mwenye mwili mtu huyo huongozwa na matendo ya mwili. Matendo hayo ya mwili hayampi mtu fursa ya kuurithi ufalme wa Mungu. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Hata hivyo mtu huwa kwenye mikono salama pale nafsi yake inapoegemea katika Roho. Tunda la Roho hakuna sheria katika maana ya kufuata mambo yetu ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na mila na desturi zetu zisizokuwa njema. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria,” Gal 5:22-23. Tuelewe kwamba mtu mzima ni mwili, nafsi, na roho.

 Wapendwa katika Kristo, mwili ni nyumba ya nafsi na roho. Kwenye nafsi ndipo penye magonjwa yenyewe kwani ni katikati ya Roho na Mwili. Ni kwenye nafsi mtu hudumu katika madhara ya dhambi na kuendelea kuhifadhi moyoni. Hapa ndipo kwenye hifadhi ya matukio mabaya yanayomsononesha mtu. Kwenye nafsi ndipo kunapomfanya mtu kutosamehe kwa muda mrefu. Nafsi hupata maumivu kutoka roho, hasa dhambi. Nafsi pia hutawaliwa na; Hofu, Chuki, Hasira, Kujihukumu, Kujikataa, Kukosa furaha, Kukosa upendo, na Kukosa amani.

Ili uisalimishe nafsi yako yakupasa kuishi katika hali ya neema, yaani, kuishi katika hali ya utakaso kila wakati. Mtume Paulo anawasihi watu wake na hasa kuwaonya juu ya matendo ya sheria. Matendo ya sheria ni uhalali waliojiwekea baada ya kuishakachua Torati na hivyo kuishi kutokana na tafsiri ya torati na mapokea ya mababu zao. Kwa namna nyingine walichokuwa wanakishikilia kilikuwa ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Hiki ndicho kile kilichojulikana kama TALMUD. Kwa mantiki hii, mtu hawezi kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria. Hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki,” Gal 2:16. Tuelewe kwamba Mtume Paulo hasemi kwamba kwa kumwamini Kristo Yesu hakuna haja ya sheria katika maana ya Torati. Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye,” Gal 3:10.  Kinachopingwa hapa ni kile nilichokisema juu ya ukweli wa TALMUD. Hapa waliyafanya tu yale yaliyozipendezesha nafsi zao na kuacha yale yaliyozisuta dhamiri zao.

Mtu akiwa chini ya Neema, yaani hali ya utakaso, hawezi kutawaliwa na dhambi. Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema,” Rum 6:14. Tunazipata neema hizo tunapojijengea uhusiano mzuri na Kristo Yesu aliyeshinda dhambi kwa sadaka yake pale msalabani. Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii,” Rum 6:16a.  Sisi tu watumwa wa Kristo kwa sababu utumishi wa utii unaleta haki. “Ni utumishi wa utii uletao haki,” Rum 6:16c. Yesu ndiye njia, kweli na uzima, Yoh 14:6. Ila mauti uletwa na utumishi wa dhambi. “Ni kweli kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti,” Rum 6:16b.

Injili inakazia jambo hili la kuwa watumwa katika utumishi wa utii uletao haki. Yesu anasema heri ya mtumwa huyu anayekesha kwa utumishi wa utii na kufanya mapenzi ya Mungu. “Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo,” Lk 12:43. Kwa kuiongoza nafsi katika kweli na neema tuipatayo kwa sakramenti ya upatanisho, ndipo tunapoiokoa na kuhesabiwa haki kadiri ya mapenzi yake Mungu. Kwa kutokufanya mapenzi ya Mungu huku ukijua ukweli huo, itakupasa kipigo kutoka kwa Mungu. “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana,” Lk 12:47. Ni kwa namna hiyo hiyo kwamba, Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo,” Lk 12:48a. Hivyo maisha yetu hapa duniani na fursa tulizojaliwa na Mungu vinatualika kuwa mawakili wazuri na waaminifu. Mwisho wa siku itakupasa kutoa hesabu yake kwa namna ulivyotumia fursa hizo. “Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi,” Lk 12:48b. Ni wakati wa kila mmoja wetu kujitazama vyema ili usije anguka katika mtego huu wa kutokukesha katika utumishi wa haki uliotukUKA katika kuyafanya mapenzi ya Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!


Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe; bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu,” 2Kor 6:3-4a

No hay comentarios:

Publicar un comentario