viernes, 2 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 26 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 26 YA MWAKA-B
3/10/2015
Somo: Bar 4:5-12, 27-29
Zab: 68:33-37
Injili: Lk 10:17-24
Nukuu:
“Jipeni moyo, watu wangu, Israeli mnaokumbukwa! Mliuzwa kwa mataifa, lakini hamkuangamia, kwa kuwa mlimtia Mungu ghadhabu mlitolewa kwa adui zenu,” Bar 4:5-6

“Kwa sababu ya dhambi za wanangu nimeachwa ukiwa, kwa kuwa walikengeuka na kuiacha sheria ya Mungu,” Bar 4:12b

“Jipeni moyo, wanangu, mlilieni Mungu! Maana Yeye aliyewapatiliza mambo haya atawakumbuka,” Bar 4:27

Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme,” Lk 10:18 

Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na n’nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru,” Lk 10:19 

Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni,” Lk 10:20

“Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21b 

TAFAKARI: “Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka binadamu yeyote yule katika mahangaiko yake ya kila siku anaitafuta furaha na anataka kuwa na furaha. Furaha hii ambayo ndiyo kielelezo cha yote ayafanyayo mwanadamu kwa bahati mbaya au nzuri furaha hiyo hukatishwa na yeye mwenyewe, mazingira anayoyaishi, au na watu wengine. Pamoja na mazingira hayo iliyosema, maisha ya mtu yasiyo na malengo ni chanzo kikubwa sana cha kutokuwa na furaha ya kweli. Malengo ya mtu ndiyo dira ya kuyafikia yale anayoyatamani. Maisha yenye malengo hubeba mafiga manne: wewe mwenyewe, uhusiano wako na Mungu, uhusiano wako na jamii inayokuzunguka,  na uhusiano wako na mazingira yanayokuzunguka. Maisha ya mtu hujengwa na kulindwa na mafiga hayo. Moja ya mafiga haya yasipozingatiwa, binadamu huyu aweza kuwa utumwani au akawa hatarini kuwa utumwani.

Utumwa kwa namna nyingine ni hali yo yote ile isiyokuwa huru au uwezo wa kufanya chochote hata kama uwezo huo, yaani  wewe mwenyewe binafsi, jamii, na Taifa upo. Utumwa huu ni hali ili ya kujisalimisha pasipo hiari yako. Vile vile kutokujielewa na kukosa ufahamu wa mambo yaliyo ya kawaida kabisa ni utumwa mbaya sana kuliko ule wa kutumikishwa. Ni kwa namna hii wewe mwenyewe unaweza kuwa mtumwa. Uhusiano wako na wengine au jamii inayokuzunguka usio na uwiano sawa, kweli, na haki waweza kukufanya wewe mtumwa, au Taifa kama dola huru likawa utumwani hata kama kijeografia wapo pale pale. Utumwa wa namna hii tunauona sana katika mataifa mengi ya Afrika na Tanzania ikiwemo. Uhusiano wako na Mungu katika hali ya uasi wakufanya kuwa mtumwa wa dhambi. Tunakuwa watumwa wa dhambi kwa kukataa waziwazi upendo wa Mungu na kujifanyia yetu, kusiko haki, upendo, kweli, na Amani. Na mwisho, uhusiano wako na mazingira yako ukiwa mbovu mwisho wa siku unakuwa mtumwa katika mazingira yako. Mfano, tunahitaji hewa safi na maji yenye usalama kwa afya zetu. Tunapoyaharibu mazingira yanayotuzunguka tunajiweka hatari kuwa watumwa wa afya zetu, na mwisho wa siku ni janga kubwa la maisha.

Wapendwa wana wa Mungu, katika hali hizo, binadamu hawezi kuwa na furaha hata kama kwa asili binadamu hutafuta furaha hiyo. Wana wa Israeli wanajikuta hatiani kwa vile tu hawakuwa na uhusiano mzuri na Mungu. Hivyo kutokuwa na furaha kama taifa na kujikuta wakiwa utumwani kunatokana na kutozishika sheria za Mungu.  Hivyo, “Kwa sababu ya dhambi za wanangu nimeachwa ukiwa, kwa kuwa walikengeuka na kuiacha sheria ya Mungu,” Bar 4:12b. Utumwa wa mtindo huu, binadamu anaweza kujinasua tu kwa kujijengea ufahamu wa kutosha. Kuwa tayari kuzisoma alama za nyakati na kuzitafsiri kadiri ya wakati. Mungu hawezi kumwacha mja wake katika hatua hii muhimu ya kujitoa kwenye mkwamo huu. “Jipeni moyo, watu wangu, Israeli mnaokumbukwa! Mliuzwa kwa mataifa, lakini hamkuangamia, kwa kuwa mlimtia Mungu ghadhabu mlitolewa kwa adui zenu,” Bar 4:5-6

Je, hali hii ya wana wa Israeli inasema nini kuhusu Taifa letu leo? Je sisi leo tunapoangalia uhusiano wetu na mataifa yanayotuzunguka hata ng’ambo ya bara letu tupo salama? Kijeografia bado tupo kwenye ardhi yetu. Je, kiuchumi, kijamii, kisiasa, utamaduni bado tupo salama? Bila shaka kwa hali ilivyo leo jibu utakua nalo. Hata hivyo hatuna sababu ya kukata tamaa. Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi endapo tutaisikiliza sauti ya Mungu ndani mwetu, na yale yote Mungu anayotufunulia kupitia watu mbali mbali. “Jipeni moyo, wanangu, mlilieni Mungu! Maana Yeye aliyewapatiliza mambo haya atawakumbuka,” Bar 4:27. Ni wakati wa kujipa moyo kwamba tunaweza na ni wakati wa kufanya maamuzi magumu kwa manufaa mapana ya taifa letu na  vizazi vijavyo. Mtindo wa kufanya mambo kwa mazoezi hauna nafasi tena katika maisha ya leo.

Wanafunzi wa Yesu wale sabini, wanarudi katika utume wao na kustajabia mambo makuu ya Mungu aliowatendea. Uhusiano wetu mzuri na Mungu ni chanzo kikubwa sana cha furaha yetu ya kweli. Lakini Yesu anawaambia wasiwe na furaha tu kwa sababu walimwana shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme, bali ndani yao Mungu aweza kufanya mambo makubwa zaidi ya hayo. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na n’nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru,” Lk 10:19. Huu ndio msingi wa furaha ya kweli kwa wale wote wenye hofu ya Mungu. Mahusiano mazuri na Mungu, hutujengea uwezo mkubwa sana wa kupambana na uovu.

Mara tuyaonapo haya makuu yakifanyika ndani mwetu tusibweteke. Dunia hii tunapoishi pomoja na uzuri wake na mambo yake, siyo mahali petu pa kudumu. Hapa ni mahali tu pa maandalizi ya umilele. Ni jukumu la kila mmoja wetu kupafanya hapa duniani kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi huku tukijua siyo sehemu ya mwisho na ya umilele. Maandalizi mazuri ya hapa duniani ndiyo jibu la uhakika wa maisha hayo ya umilele. Hivyo furaha yetu kwa yote tutakayoyapata hapa duniani itupe taswira halisi ya maisha baada ya haya. Kuhusu ukweli huu Yesu anawaonya wanafunzi wake nasi pia kwa kusema, Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni,” Lk 10:20. Furaha yetu isiwe tu ya leo na kesho, bali furahi hii ipewe kibali na Mungu Baba wa Mbinguni. Tufurahi na Mungu milele mbinguni.

Wapendwa wana wa Mungu, ufahamu wa siri na ukweli huu,  Mungu anautoa wa wanyenyekevu wake wa moyo. Wanyenyekevu wa moyo hufunuliwa siri za Mungu kwa sababu wapo tayari kusikia, kufanya, na kuishi kadiri ya mpango wa Mungu. Hivyo Yesu anamshukuru Mungu kwa niaba ya wanyenyekevu wote wa Moyo na kusema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21b. Ni uchanga wetu kama watoto tupo tayariwa kujifunza, kusikiliza, kufanya, na kuishi kadiri ya matakwa ya Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!


Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili,” Rum 12:16

No hay comentarios:

Publicar un comentario