JUMAPILI
YA 25 YA MWAKA-B
20/9/2015
Somo
I: Hek 2:12, 17-20
Zab:
53:3-6, 8
Somo
II: Yak 3:16-4:3
Injili:
Mk 9:30-37
Nukuu:
“Haya na tuone kama
maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake;
tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake,” Hek 2:17
“Na tumhakikishe kwa
jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake
akidhulumiwa,” Hek 2:19
“Maana hapo palipo
wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya,” Yak 3:16
“Lakini hekima itokayo
juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya
watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki,” Yak 3:17
“Na tunda la haki
hupandwa katika amani na wale wafanyao amani,” Yak 3:18
“Mwatamani, wala hamna
kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata,” Yak 4:2a
“Hata mwaomba, wala
hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yah 4:3
“Akaketi chini,
akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa
mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk 9:35
“Mtu akimpokea mtoto
mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi,
humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma,” Mk 9:37
TAFAKARI:
“Mwisho wa ubaya ni aibu; ila tunda la haki hupandwa katika amani na wale
wafanyao amani.”
Wapendwa wana wa Mungu,
karibuni na tutafakari pamoja na Mama Kanisa Dominika hii ya 25 ya Mwaka “B” wa
Kanisa. Ni kweli kwamba mwisho wa ubaya ni aibu; ila tunda la haki hupandwa
katika amani na wale wafanyao amani. Ndugu zangu, wapo wanaoshikilia maumivu
(machungu) bila kuyaacha. Badala ya kutoka katika maumivu kwa kusamehe,
wanaendelea kuyakumbuka katika mawazo yao tena na tena. Baadhi ya watu
wanaongozwa na chuki kutunza ndani uchungu wao, na wengine huwalipukia watu
wengine. Hali zote hizi si nzuri na hazisaidii maishani. Chuki mara nyingi
huleta maumivu kwako kuliko yule unayemchukia. Mtu aliyekukosea anaweza kuwa
amesahau lile kosa na anaendelea na maisha yake vizuri, wewe unaendelea kuumia
na kuhangaika na yaliyopita.
Sikiliza ndugu yangu:
Wale waliokuumiza wakati uliopita hawawezi kuendelea kufanya hivyo sasa
"isipokuwa" kama utaendelea kutunza uchungu. Yaliyopita yamepita!
Hakuna kitakachoyabadilisha. Unajiumiza tu na uchungu wako. Kwa ajili yako,
jifunze kutokana na hilo na kisha achana nalo. Maandiko matakatifu
yanatukumbusha kuwa, "kwani hasira humwua mtu mpumbavu, nao wivu humwua
mjinga." Ayu 5:2. Kuwa na hofu
kiasi cha kufa kwa sababu ya uchungu ni upumbavu, ni kitu kipumbavu kukifanya.
Wenye chuki na wivu hufurahia katika haya, “Haya na tuone kama maneno yake ni
kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; tufanye kujaribu
yatakayompata wakati wa mwisho wake,” Hek 2:17. Wenye wivu na majingu faida yao
ni kupoteza muda na kuwa vivuli vya wengine. “Maana
hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya,” Yak
3:16. Je, wapata faida gani kwa haya yote?
Wapendwa wana wa Mungu,
kuongozwa na msukumo huo katika maisha ni sawa na kuhangaika kuibomoa nyumba ya
jirani yake ilhali wewe mwenyewe hauna nyumba ya kuishi huku ukitegemea hifadhi
kwa jirani yako huyo. Ni kuishi katika falsafa ya “sote tukose!” “Na
tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha
saburi yake akidhulumiwa,” Hek 2:19. Wapo wengi miongoni mwetu hujisikia furaha
wakati wenzao wanateseka. Hii siyo hekima ya Mungu hata kidogo. “Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya
amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda
mema, haina fitina, haina unafiki,” Yak 3:17. Mimi ninayeishi leo na kesho
yanipasa kujua ukweli huu kwamba dunia hii si mahali pangu kwa kudumu. Nipo
katika ulimwengu huu kama sehemu ya maandalizi yangu ya maisha ya umilele. Kwa
hiyo hatma yangu ya umilele inategemea sana ninavyoishi leo, yaani, mahusiano
yangu na Mungu, wenzangu, na mazingira ninayoyaishi. Ni kuishi katika ukweli
huu nikijua kwamba, “tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao
amani,” Yak 3:18.
Wapendwa
wana wa Mungu, tusipoitafuta Amani katika haki hata yale tuyaombayo Mungu
hawezi akatupa kwa sababu hayatatufaidia sisi na wenzetu. Tutakuwa tunaomba kwa
ajili ya faida yetu binafsi kwa gharama za wengine. Mungu aliye Haki, Upendo,
Msamaha, na Amani hawezi kuruhusu jambo hilo hata kidogo. Mungu atakacho kupa
wewe hakiwezi kuwa madhara kwa mwingine kwa sababu kila mmoja wetu yupo hapa
duniani kwa sababu yake mwenyewe Mungu, na amemuumba kwa sura na mfano wake.
Hivyo tunapomwendea Mungu katika hali hii hawezi tutupatia kile tumwombacho.
Kwa sababu hiyo, “hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili
mvitumie kwa tamaa zenu,” Yah 4:3.7
Ndugu
yangu uliyefika jumapili hii ya leo elewa kwamba nafasi yako na hadhi yako
mbele ya Mungu haijengwi kwa wingi wa ufahamu wa ulimwengu huu aliouumba Mungu,
bali kwa kujinyenyekesha mbele zake ili yeye Mungu abaki kuwa mwalimu wako
maisha yako yote. Tendo hili la kujishusha halimaanishi tusijifunze na kutoka
kwenye wimbi la ujinga, bali kujifunza kwetu siyo mwisho wa ukweli ule
tunaoufahamu na ambao Mungu angependa kutufunulia kadiri ya mapenzi yake. Kwa
maana, “kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, wote wafanyao hayo wana akili
njema, sifa zake zakaa milele.” Zab 111:10. Hivyo hakuna namna yo yote kwa
mwanadamu kupata neema na baraka kutoka kwa Mungu kusiko kujisalimisha kwake
kwa Mungu. Kujisalimisha kwa Mungu ndiyo njia pekee ya kufunuliwa neema na
baraka za Mungu. Hivyo Yesu anawaambia Tenashara wake, akisema, “mtu atakaye
kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk 9:35
Wale wote wenye kumcha Bwana katika uelewa
huu, Yesu anawafananisha na watoto wachanga. Kumcha Bwana huku ni kuwa tayari
kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu pasipo shaka yoyote. Mtoto humwamini mzazi
wake kupita vitu vyote. Hivyo Yesu anawaambia wanafunzi wake, “mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea
mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma,” Mk
9:37. Ndugu yangu, ukuu wetu upo katika unyenyekevu wetu na kuwa tayari
kutumika kwa ajili ya manufaa ya wengi.
Andrea na
Yosefu walikuwa marafiki na wafanya biashara. Hata hivyo hawakufanikiwa sana
katika biashara zao licha ya kwamba walionekana kufanya bidii sana katika
biashara zao. Ndugu hawa walikuwa ni watu wa sala na hivyo kila siku walipenda
kusali misa ya asubuhi na baadaye kuwahi kwenye biashara zao.
Andrea na
Yosefu walikuwa na maduka ya kuuza
bidhaa mbalimbali, yaliyokuwa yakiongozana katika mtaa wa changamkeni katika
mji wao. Mungu baada ya kuona taabu zao na maombi yao kila siku ya misa za
asubuhi, alimtuma malaika Gabrieli kwenda kwa Andrea na kumuuliza swali hili:
“Omba cho chote kile utakacho Mungu atakupa kitu hicho, ila mwanzako, yaani,
Josefu Mungu atampa mara mbili zaidi.”
Baada ya
kupata ujumbe huu mzito, Andrea alimjibu Malaika Gabrieli na kumwambia, “nipe
siku tatu za kufikiri nami nitakupa jibu.” Siku tatu zilikwenda, na malaika
akamjia Andrea na kumwambia, “Je, umepata jibu?” Andrea akamjibu, “naomba niwe
chongo.”
Wapendwa
wana wa Mungu, Andrea alitafakari sana na kujiuliza kiasi cho chote cha pesa
angalikiomba mwenzake Josefu angepata mara mbili zaidi. Hivyo kwa kuongozwa na
chuki, aliamua kuomba awe chongo ili mwenzake awe kipofu, na kushindwa kuona
kabisa.
Hivi
ndivyo maombi yetu yalivyo. Mungu hawezi kamwe kutufungulia baraka na neema kwa
mtindo huu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU NIJALIE MOYO SAFI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario