viernes, 23 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 30 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 30 YA MWAKA-B
25/10/2015
Somo I: Yer 31:7-9
Zab: 126:1-2, 2-3, 4.6, 6
Somo II: Ebr 5:1-6
Injili: Mk 10:46-52
Nukuu:
Maana Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli,” Yer 31:7

Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu,” Yer 31:9

Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:1

awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu,” Ebr 5:2 

na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:3

Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni,” Ebr 5:4 

“Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu,” Mk 10:47

Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita,” Mk 10:49

Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona,” Mk 10:51 

Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani,” Mk 10:52

TAFAKARI: “Mungu huwaridhia watu wake nyakati zitimiapo. Msife Moyo.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, karibuni kwa pamoja leo Dominika ya 30 ya mwaka “B” wa Kanisa tulitafakari neno hili, “Mungu huwaridhia watu wake nyakati zitimiapo. Msife Moyo.” Dominika hii ya 30 ya mwaka “B,” masomo yote matatu yanalenga kwenye dhana hii ya Mungu; Huruma, Upendo, na Haki kwa watu wake walioonewa. Mungu wetu siyo kama mtengeneza saa ya ufungua, na baada ya tendo hilo huiacha saa hiyo ijiendeshe yenyewe. Ukimya wa Mungu katika mahangaiko ya mwanadamu siyo kwamba hamjali mwanadamu, bali husubiri nyakati zifaazo ili alitendapo jambo hilo alitende katika ukamilifu na utimilifu wake mwenyewe. Ukimya wa Mungu kwetu katika mahangaiko ni nafasi pia kwetu ya kuyatafakari kwa kina yatupatayo ili nyakati zikitimia tufanye uamuzi sahihi kwa kile apendacho Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna uovu wowote ule utakao dumu milele. Wema na Upendo wa Mungu ndivyo vitakavyodumu milele. Imani na matumaini yetu yatafikia kikomo chake. “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13. Mungu hawezi kamwe kufuta mahusiano na mwanadamu aliyechagua kumuumba kwa sura na mfano wake. Ni kwa namna hii ya ajabu, Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu,” Mdo 17:26-27. Mahangaiko na mateso ya watu kwa namna yoyote ile, iwe utumwani au kwenye inchi yao wenyewe, Mungu hawezi kuyafumbia macho. Hakuna mwanadamu yeyote juu ya uso huu wa dunia ambaye yupo kwa sababu yake au kwa bahati mbaya. Kila mmoja wetu yupo kama alivyo kwa sababu ya upendo wa Mungu na furaha ya Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, kilio cha muda mrefu cha wana wa Israeli kinasikika mbele ya Mungu, naye Mungu wakati ulipotimia alisema basi inatosha. Mungu asemapo inatosha, kweli inatosha kwa sababu,  kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu,” Mhu 3:1. Ni kwa kusudi hilo na kuridhia kwake Mungu na watu wake anatuma ujumbe wa furaha kwa Yakobo kupitia Nambii Yeremia na kusema, “Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli,” Yer 31:7. Mungu analitenda jambo hili kwa wakati ulipotia. Tukiwa na Mungu hatuna sababu ya kuwa na hofu wala Mashaka licha ya vitisho vingi vitakavyo uzunguka ukweli huo. Kama sote tuliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hakuna binadamu mwenye haki zaidi ya mwingine, wala mwenye haki zaidi za umiliki kuliko mwingine.

 Ni kwa maana hiyo hiyo kwamba hakuna kikundi chochote kinachoweza kujihesabia haki katika umiliki wowote ule. Kwa kufanya hivyo kwa nguvu na mabavu ni kujaribu kuchukua haki na kibali ya Mungu iliyopo ndani ya kila mmoja wetu. Hili ni kosa kubwa sana binadamu kulifanya. Kisicho kibali na haki ya wengi kwa maridhiano hasa katika swala zima la utawala ni haramu, na hapo Mungu hawezi kuwepo. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao,” Mt 18:20. Sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Kuipuuza sauti ya wengi iliyosima katika haki na kweli ni kumpuuza Mungu, na katika hali hiyo Mungu hawezi kufumba macho yake. Mtume Paulo anasema, bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu,” 1The 2:4. Lolote lile lisilokuwa na hofu ya Mungu ndani yake halina uhalali wa kuwepo na mwisho wake ni majanga makubwa. Mzaburi anasema, Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure,” Zab 127:1

Wapendwa wana wa Mungu, vita ya kweli na haki hasa pale mwanadamu anapojaribu kujimilikisha haki za watu, kuuondoa utawala huo wa uovu si jambo rahisi kwa binadamu fanya kwa nguvu zake mwenyewe. Tunahitaji nguvu ya sala pamoja na maharifa aliyotujalia Mungu. Hata leo katika Taifa letu kama ilivyokuwa Taifa la wana wa Israeli tunahitaji sala na uwezo wa Mungu ili kuvuka vita hivi vya haki dhidi ya uovu. Naye Mungu anasema nasi leo, mtakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hamtajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu,” Yer 31:9. Leo Taifa letu la Tanzania lipo katika hali hii ya wana wa Israeli. Mungu peke yake ndiye wa kutuvusha katika mtego huu wa haki dhidi ya uovu. Tumwamini Mungu pasipo shaka kwa sababu Mungu hawezi kuumba jiwe kubwa ambalo mwisho wa siku akashindwa kulinyanyua. Mungu aliyetuumba kwa kutuchagua na kutupenda kwa namna ya pekee hatoshindwa kututoa kwenye mkwamo huu wa leo.

Mungu kwa nafasi yake atamtumia mmoja wetu kutimiza nia na matamanio yetu. Mpango wa Mungu kwetu ni wa ajabu sana kuuelewa. Ila historia ya wokovu wetu inatuonyesha wazi ukweli huu kwamba, Mungu hutumia vile vilivyo dhaifu kufifisha vile vinavyojionyesha na kujipendekeza kuwa shupavu na hodari. Mama Bikiria Maria alipohesabiwa haki mbele ya Mungu anatuambia ukweli huu kwa kusema, Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:51-52. Huyu ndiye Mungu anayesimama kutetea haki za wangonye na kuwa sauti kwa wale wasio na sauti katika jamii. Kwa kutimiza jambo hili Mungu huchagua kile kinachoonekana dhaifu machoni mwa watu hasa upande ule unaojihesabia haki. Jambo la ajabu licha ya udhaifu wetu kibinadamu, kwa sakramenti ya ubatizo, Mungu anatushirikisha mambo makuu matatu; Ukuhani wake, Unabii, na Ufalme. Ni kwa namna hii ya ajabu kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:1. Hivyo yote tuyafanyayo si kwa mastahili yetu binafsi, bali yale yanayomhusu Mungu na Taifa lake.

Wapendwa katika Kristo, Mungu anayempenda na kumchagua  ayafanye yale anayoyataka ana sifa hizi tatu kadiri ya somo letu la pili leo: Kwanza kabisa, awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu,” Ebr 5:2. Mungu hatuambii mtu huyo lazima awe Mtakatifu kama Yeye alivyo, bali mtu huyo aweza kutumika vyema kwa sababu naye ana hali ya udhaifu kama atakao wahudumia. Waswahili wanasema, ‘zimwi likujualo halikuli likakwisha.’ Sifa ya pili ni kuwajali wale atakao watumikia licha ya udhaifu wake. Na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:3. Ni kwa kupitia wajibu huu aliopewa ndipo atakapo tumia dhamana hiyo aliyopewa ya juu kabisa kujisahihisha makosa yake, na kujitakasa dhambi zake kwa sadaka ya utumishi wake na huruma ya Mungu. Na sifa ya mwisho mtarajiwa huyo asiwe mtu wa kujikweza na kujihesabia haki, bali Mungu awe hofu yake. Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni,” Ebr 5:4. Sifa hizo tatu kadiri ya somo letu la pili leo zituongoze katika ufahamu wa kweli kutambua ni yupi anayetufaa kuwa kiongozi wetu. Tumwombe Mungu kwa namna ya pekee atuongoze vyema katika chaguzi hii ya viongozi wenye kuhesabiwa haki na kupewa kibali mbele zake Mungu.

Injili yetu ya leo inakazia swala lile lile la Mungu kuwaridhia watu wake nyakati zitimiapo. Jambo la pekee katika Injili ya leo ni hili la uponyaji wa Bartimayo  mwana wa Timayo. Nyakati za kuponywa kwake zinatimia pale alipopaza sauti yake na kusema inatosha Bwana, niondoe katika mahangaiko na shida hii niliyokuwa nayo kwa muda mrefu. Kumbe neema na baraka hazikufuati kama haupo tayari kujifungua na kujiweza wazi kuzipokea neema na baraka hizo. Ndiyo yako ya kutoka ndani, ndiyo pona yako kutoka mateso yako. Bartimayo ambaye alikuwa mwombaji kipofu anapomsikia Yesu anapita anasema kwa sauti kuu, “Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu,” Mk 10:47. Ni ukweli mwamba Bartimayo alichoshwa na hali yake ya kuomba omba, na umasikini uliokuwa unamzunguka. Bartimayo alichoshwa na kutokuona kwake, hivyo alipenda kuona ‘kweli’ na ‘haki’ zikitendeka. Sehemu kubwa ya Watanzania leo hawana tofauti na hali aliyokuwa nayo Bartimayo. Wengi tu masikini wa kutupwa na ombaomba ilhali Mungu katupatia kila kitu kama Taifa. Yesu anamjibu Bartimayo, mimi na wewe, “Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona,” Mk 10:51. Bartimayo ametoa jibu sahihi juu ya mahangaiko na mateso yake. Je, wewe na mimi tunajibu gani juu ya hatima ya maisha yetu na Taifa letu? Baada ya Bartimayo kutoa ombi lake, Yesu analitimiza kwa kusema, “Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani,” Mk 10:52. Je, una imani ya kutosha ili upate uponyaji? Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii usipoteze nafasi uliyopewa leo kufanya maamuzi sahihi ya maisha yako na Taifa lako kwa vizazi vingi vijavyo.

Napenda nikuache na maswali haya yafuatayo yakusaidie:
1.      Masomo ya leo yanasema chochote kuhusu Tanzania yako ya kesho?
2.      Somo la pili leo kutoka waraka kwa Waebrania linasema chochote kuhusu wagombea nafasi mbalimbali za uongozi hasa kwa Rais umtakaye?
3.      Kama somo hilo la Waebrania lina sema kitu kuhusu swali hilo la pili, bado umebaki na uelewa ule ule wa mwanzo uliojikita kwenye ushabiki?
4.      Mwisho, somo la kwanza na Injili linasema chochote kuhusu ukomo wa mahangaiko na mateso yako wewe, na Taifa kwa ujumla?

Tumsifu Yesu Kristo!


“Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu,” Zab 27:9

No hay comentarios:

Publicar un comentario