jueves, 15 de octubre de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 28 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 28 YA MWAKA-B

16/10/2015

Somo: Rum 4:1-8

Zab: 31:1-2, 5, 7

Injili: Lk 12:1-7

Nukuu:

“Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu,” Rum 4:2

“Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki,” Rum 4:3b

“Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao,” Rum 4:7

“Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi,” Rum 4:8

“Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki,” Lk 12:1b

“Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana,” Lk 12:2

“Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi,” Lk 12:4

“mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo,” Lk 12:5b

“Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi,” Lk 12:7

TAFAKARI: “Mungu ndiye mwenye kukuhesabia haki, na siyo mastahili tu ya  matendo yako.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni hulka ya binadamu kujipendelea na hata wakati mwingine kujihesabia haki na kujiridhisha kwa kile anachoona kwake kinamfaa. Kujijengea huku uhalali kwa mwanadamu kwaweza chukua mitindo mbalimbali ya kimaisha. Ni kweli kwamba kazi ya mtu humjengea utu mtu.  Ila kwa kielelezo hicho tu kama sehemu ya maisha ya mtu siyo uhalali kwa kupata mastahili mbele ya Mungu. Mtu ni zaidi ya kazi yake. Swali hapa ni kwamba, je, nisipoweza kufanya kazi kutokana na ulemavu fulani wa mwili wangu, utu wangu unaondolewa kama mwanadamu? Wapo pia watu wengine hujinasibu kwa kuwa na uwezo wa pekee kiakili. Na kwa hali hii wakajikuta kijihesabia haki katika mambo mbalimbali katika jamii na hata mbele za Mungu. Je, sisi tulio na akili za kawaida kabisa na hata wakati mwingine chini ya uwelewa wa kawaida “common sense,” ubinadamu wetu na utu wetu haujakamilika?

Ndugu yangu, upekee wako na hasa karama Mungu alizokupa si wakujinufaisha na kujisifia wewe tu, bali amekufanya hivyo kwa sababu ameamua uwe hivyo kwa mapenzi yake na kwa sababu yake. Na lengo kubwa hapa amekufanya hivyo kwa kufaidiana. “Hivyo, kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana,” 1Kor 12:7. Kuishi karama hizo kwa ajili ya kujikweza na kujihesabia haki ni “kama mawingu na upepo pasipo mvua; ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo,” Mit 25:14. Ni Mungu tu anayeweza kukuhesabia haki kwa sababu wewe kama ulivyo hauna kilicho chako zaidi ya dhambi zake. “Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu,” Rum 4:2. Ibrahimu anahesabiwa haki si kwa matendo yake, bali kwa Imani yake kwa Mungu. “Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki,” Rum 4:3b. Je, matendo yetu mema na ya kumcha Mungu hayana nafasi mbele za Mungu? La hasha! Mtume Yakobo anatuambia hivi,“Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu,” Yak 2:18. Hivyo matendo yetu yakibeba kile tunachoamini juu ya Mungu, na uhusiano wetu na naye, basi hatutakuwa mbali na ufalme wa Mungu. Hata hivyo ni Mungu peke yake mwenye kuona undani wa hayo matendo yetu, na kwa mantiki hiyo na kwa  matakwa yake ndiye atakaye tuhesabia haki.

Wapendwa wana wa Mungu, ninapojitazama mimi na kile nilicho katika mtazamo wa kibinadamu na sema wazi sina kilichokuwa changu kwa asilimia zote mia moja zaidi ya dhambi zangu. Hivyo kama mwanadamu ninahitaji neema na huruma ya Mungu kila wakati. Ninahitaji huruma ya Mungu kwa msamaha wa dhambi zangu ili niweze kupata neema hizo za kuishi Utakatifu ikiwa ndicho cheo chetu kwa aliye masikini au tajiri katika ulimwengu huu, kitupasacho kukipigania kila siku ya maisha yetu. Msamaha wa Mungu katika mwono wa dhambi ndiko kusitiriwa kwetu naye. Mtume Paulo analisema jambo hili hivi, “heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao,” Rum 4:7. Mungu ndiye anayetusitiri na kuturudishia hadhi yetu kama wanadamu na warithi wa ufalme wake pale tunapofanya toba ya kweli na majuto ya dhambi zetu. Mungu ni HURUMA katika maana halisi. Ni kwa maana hii kama Mungu angeamua kumshuhulikia kila mtu kadiri ya matendo yake hakika tusingekuwa na sehemu ya kujitetea wala kufichama. “Bwana, kama wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3. Ndugu yangu, sote tunaishi kwa neema tu za Mungu, kwa sababu anatupenda upeo. Hivyo usalama wangu na wako upo kwake Mungu na hasa tunapoishi katika hali ya kutokuwa na hatia. “Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi,” Rum 4:8. Kama Mungu anatupenda na kututakia mema siku zote, ni wajibu wetu kuishi katika neema hii ya utakaso. Furaha ya kweli hatuipata kutokana na vitu tulivyonavyo, bali ni amani ya ndani tuipatayo kwa kuishi bila hatia.

Wapendwa wana wa Mungu, tafsiri hii ya kuhesabiwa haki pasipo matendo yetu kama kielelezo cha kujiinua kwetu, ndiyo tahadhari anayotuambia leo Yesu katika Injili. Kujiinua kwa ubinafsi wetu ili tupate mastahili mbele za watu na Mungu ni chachu mbaya sana. Hivyo Yesu ananiambia mimi na wewe kwamba,“jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki,” Lk 12:1b. Unafiki ni kuishi kwa uhakika kile ambacho siyo wewe. Ni kuishi kwa kuwapendezesha watu kuwa wewe ni kitu fulani ilihali sivyo. Ndugu yangu tunayesafiri sote pamoja katika tafakari hii, ni ushauri wangu hata kama hauna maana kwako kwamba, ishi kile ulicho katika kweli na haki yake. Ni katika kweli hiyo na haki Mungu utunyanyua na kutupeleka pale alipo. Huku ndiko kuhesabiwa haki na  Mungu. Na kuishi katika kweli na haki ni kutambua kwanza kabisa mimi ni mwanadamu niliyeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu, na amependa niwe kama nilivyo na kuishi katika kweli hii. Hakuna haja ya kuogopa kuishi ukweli huu hata ikibidi kufa kwa ajili ya ukweli huu. Yesu ananiambia mimi na wewe kwamba, “nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi,” Lk 12:4. Ndugu yangu, kuuishi ubinadamu wako kwa mapaswa ya Mungu aliyetuumba si kazi rahisi. Wengi wetu hawapendi kujipokea kama walivyo ikiwa ndiyo sharti la kwanza kuuishi ubinadamu wako. Je, nina hoja nzito na ya kweli ya kutokujipokea? Ni nani basi ninayemwogoba? Je, ni nani yanipasa kumwagoba katika ubinadamu wangu?

Wapendwa wana wa Mungu, leo Yesu ananipatia jibu mimi na wewe ni nani tupasaye kumwogopa. Naye anasema, “mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo,” Lk 12:5b. Ni Mungu mwenye uwezo wa kuua na kumtupa mtu Jehanum. Hivyo wa kumwogopa ni MUNGU peke yake. Huyu ndiye tunayepaswa kuwa na hofu naye na si vinginevyo. Huyu ndiye anayejua kwenda na kutoka kwetu.  Wapendwa, ni Mungu wetu huyu kwamba “hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi,” Lk 12:7. Mungu wetu ndiye yote katika yote.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu.” 1Sam 2:6-7

No hay comentarios:

Publicar un comentario