sábado, 10 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 28 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 28 YA MWAKA-B
11/10/2015
Somo I: Hek 7:7-11
Zab: 89:12-17
Somo II: Ebr 4:12-13
Injili: Mk 10:17-30
Nukuu:
            “Naliichagua kuliko fimbo za enzi na vitu vya enzi, wala mali sikuifananisha na kitu cha thamani; mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo,” Hek 7:8-9

Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo,” Ebr 4:12

Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu,” Mk 10:18 

Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate,” Mk 10:21

Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi,” Mk 10:22 

Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mk 10:25

Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu,” Mk 10:27

Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30

TAFAKARI: “Kwa maana kuishi kwetu ni Kristo, na kufa  kwetu ni faida kwa wengine.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 28 ya mwaka “B” wa Kanisa. Dominika hii Mama Kanisa anatualika sote tutafakari juu ya sababu ya maisha yetu hapa duniani na msingi unayobeba maisha yote. Napenda tutafakari maneno ya Mtume Paulo ambayo yanafanana na ujumbe wetu wa leo, yaani, “kwa maana kuishi kwangu ni Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21. Kama tumeumbwa kwa sababu na lengo mahususi la Mungu, ni kwa maana hiyo hiyo tupo hapa duniani kwa sababu maalumu ya Mungu. Ni kweli isiyotia shaka kwamba uumbaji wetu umelenga katika ukombozi wa ulimwengu mzima. Hivyo uwepo wako hauna maana yoyote kama hauna uhusiano na mwingine aliyeumbwa kwa mfano wake Mungu. Tupo hapa duniani kwa kufaidiana na kutaabikiana.

Jambo la msingi kupita yote ni kulijua neno la Mungu na kulishika kikamilifu. Hii ndiyo hekima ya kwanza kabisa inayolenga sababu ya kuumbwa kwetu na kuwa katika ulimwengu huu. Uzima huu tunaupata katika neno la Mungu. Neno la Mungu ndiyo kirutubisha na kijenga kinga ya mwili na roho. Tukikosa kirutubisho hiki, hakika afya yetu itakuwa katika mashaka na tuupatapa ugonjwa wowote ule hatutakuwa salama kwa sababu hatuna kinga. Hivyo kulichagua neno la Mungu ni muhimu kuliko fimbo za enzi na vitu vya enzi, wala mali sikuifananisha na kitu cha thamani; mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo,” Hek 7:8-9. Katika neno vyote vilikuwa kama Mungu alivyoamuru. Mungu aliumba kwa neno na vyo vilifanyika kama tunavyoviona. Hivyo Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo,” Ebr 4:12. Wapendwa wana wa Mungu, je tunashiriki neno hili kikamilifu katika jumuiya zetu? Mbona leo jumuiya zetu zimekuwa za kina mama na watoto tu? Vijana wa kike na wakiume mpo wapi?

Neno hili ambalo ni uzima na uhai ndani kwetu, ndiye Kristo mwenyewe. Yesu leo anakutana na kijana aliyejaa shauku ya uzima wa milele huku akikabiliwa na changamoto ya mali na malimwengu. Uzima wa milele upo kwa kila mmoja wetu, ila yatupasa kuwa tayari na matakwa yake. Kijana huyu anajinasibu mbele ya Yesu kwa mbwembwe nyingi na hata kumwita Yesu MWEMA. Kwa mbwembwe hizi Yesu anampa somo la kwanza na kumweka sawa.

Yesu anatoa angalisho mapema kabisa kwa kusema, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu,” Mk 10:18. Wema katika maana halisi ya neno hilo u na Mungu. Kama wema u na Mungu, yote tuyafanyayo hayawezi lingana na wema wa Mungu.

Ndugu zangu katika Kristo, yapo mambo mengi yanayotutia matumaini na heri hapa duniani. Ila kwa mambo hayo hatuwezi kufananisha na uzuri na wema wa Mungu. Tukirejea falsafa ya Plato, twaweza kusema kwamba, yote tuliyonayo yanaakisi tu wema na uzuri halisi alionao Mungu peke yake. Ni katika hali hii, Yesu anampa changamoto kijana yule aliyejiona mkamilifu na hasa amri za Mungu. Jambo hili kwake halikuwa matatizo kabisa kwani amri hizi alizishika vizuri tangu utoto wake. Hivyo Yesu anamwambia baada ya kumkazia macho na kumpenda, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate,” Mk 10:21.

Ndugu yangu, yawezekana hauna mali katika maana ya vitu vya kuonekana na kushikika, ila umejaliwa mali za kiroho kama; akili nzuri, uwezo wa kusikiliza na kutatua matatizo yaani busara na hekima, na hata maisha ya ukaribu na watu. Haya pia Yesu anatuambia tuenende tukayauze na kuwapa maskini. Kuyauza haya hasa katika maana ya utajiri wa Kiroho, ni kutoshikamanana nayo na kujifananisha nayo kama kielelezo cha utu wetu mbele za watu na kujitofautisha mbele za wengine na haya yanayoonekana pekee mbele za watu. Kuwapa maskini kunamaanisha kwamba haya yote tumepewa ili tuyatoe kwa wahitaji. Kila mmoja wetu hapa duniani ni mwitaji. Hivyo kila mmoja wetu ni masikini katika hali ya kuhitaji kile asichokua nacho. Hivyo kuishi kwetu hapa duniani kama wana wa Mungu na wenye hofu ya Mungu, ni kuishi katika kufaidiana kuliko kwa kweli, yaani niwe kwaajili ya mwingine.

Wapendwa wana wa Mungu, kuyaona maisha katika mtazamo huu ni sawa na kujikana mwenyewe. Hivyo hatuoni ajabu kwa kijana yule kuondoka mbele ya Yesu baada ya kupewa maana ya pili ya sababu ya maisha yake hapa duniani. Kwa maana hiyo, yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi,” Mk 10:22. Kwa maana nyingine kijana huyu alikuwa na vipaji vingi, au uwezekano mwingi kimaisha. Jambo hili linamtia hofu ya kuishi kwa sababu aliishi kwa ajili yake tu. Kuishi kwetu hapa duniani si kwaa ajili yako tu. Ubinadamu wetu, kama ulivyo katika kitabu cha mwanzo juu ya uumbaji, tumepewa mamlaka ya uumbaji shirikishi na Mungu. Hivyo tupo hapa duniani kwa ajili ya wengine pia waone na kutambua uso wa Mungu. Ukweli huu juu ya uumbaji wetu na sababu zake, tusipoutilia maanani hatutaona wajibu wa kuwa matajiri. Hii ndiyo sababu ya Yesu kusema hivi juu ya matajiri wasiojua wajibu huo katika dhana nzima ya kufaidiana, Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mk 10:25. Ndugu yangu, chunguza utajiri wako.

Jambo hili si rahisi kulifanya kwa sababu sote kama binadamu tunayo silika ya umimi. Ila Mtu kuwa huru na kuishi katika umilele yampasa kuushinda umimi wake. Kinachohitajika hapa ni utashi wa kweli wa kufanya yaliyo mema na yenye mtazamo wa kimungu kila siku. Tukiwa katika mwelekeo huu kimaisha, hakuna cha kutushinda. Hivyo Yesu anasema katika hali hii ya kibinadamu; Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu,” Mk 10:27. Ndugu yangu, kwa Mungu yote yanawezekana. Chukua hatua. Hivyo kinga hii yatupasa kuichangua

Mzee Mathayo na Mamsoro walibariki ndoa yao wakiwa tayari wana watoto wanne. Mzee Mathayo alikuwa mfanya biashara mzuri sana. Hakupata muda wa kusali na wana jumuiya wenzake kila siku ya jumamosi asubuhi, kwani alidamka mapema sana kwenda kwenye biashara zake. Kitendo hiki kilimkera sana mke wake na familia nzima. Kila mara alipoulizwa na mke wake kwa nini hatengi muda wake na kusali nao kwenye jumuiya, Mzee Mathayo alimjibu mkewe na kusema, “Mke wangu haujua tulipofunga ndoa tumekuwa kitu kimoja? Unapokwenda wewe kwenye jumuiya nami nipo. Shida yako nini? Somo hili hata Paroko analijua.” Mzee Mathayo alijitetea kila mara kwa maneno haya.

Kwa upende mwingine kwa michango ya Kanisa na mengineyo kama harambee, Mzee Mathayo alikuwa mstari wa mbele kabisa. Kwa tendo hili alijulikana sana Parokiani mwake. Miaka ilipita na wote wawili yaani, Mzee Mathayo na Mama Mamsoro walifariki. Je siku ya ufufuo ilikuaje?

Mungu hakuchelewa kuliona jina la Mamroso, na tendo lilifuata ni kumfufua kama alivyobatizwa, yaani, ‘Mamroso nakufufua kwa jina langu (Mungu), na la mwana (Yesu Kristo) na la Roho Mtakatifu.’ Mamroso aliposhtuka akajikuta yupo peponi na Watakatifu wote, Malaika na Mungu. “Je, Mume wangu yupo wapi,?” Mamsoro alimwiliza Mungu. “Niliwaunganisha kwa sakramenti ya ndoa ili msaidiane wote kuwa wakamilifu ila mumeo alikataa kwa nafsi yake mwenyewe licha ya wewe kumshauri kila siku hasa kulisikia neno langu kupitia jumuiya. Hivyo hapa kalabrasha lake halipo. Na kama halipo hakuna ufufuo kwake,” Mungu alimjibu. “Mbona tuliambiwa tumekuwa kitu kimoja katika sakramenti ya ndoa?” Mamroso alimuuliza Mungu. “Sakramenti hiyo mmeunganishwa ili msindikizane na kusaidiana katika utakatifu na mwisho wa siku kila mmoja wetu atafufuliwa kwa jina lake kama ilivyokuwa siku ya ubatizo wetu. Wewe ulifanya nafasi yako vyema. Yeye alichagua fungu lake na kwa hilo anastahili kuwa pale alipo, yaani motoni,” Mungu alimjibu.

Wapendwa wana wa Mungu, tutakuwa pale tulipojiandalia. Ni vyema tukawa makini kwa kile tulicho leo katika hali zetu zote. Kuishi kwetu kuna maana tukiwa na Kristo na kufa kwetu ni faida kwa wengine.
Tumsifu Yesu Kristo!


“Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario