viernes, 30 de octubre de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 30 YA MWAKA.B

IJUMAA WIKI YA 30 YA MWAKA-B
30/10/2015
Somo: Rum 9:1-5
Zab: 147:12-13, 14-15, 19-20
Injili: Lk 14:1-6
Nukuu:
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu,” Rum 9:1-2

Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo?” Lk 14:3

Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato?” Lk 14:5

TAFAKARI: “Binadamu na uhai wake una thamani kubwa sana mbele ya Mungu.”

Wapendwa wana Mungu, tunapotafakari uumbaji wa ulimwengu huu na historia ya wokovu wetu hatuwezi kukwepa ukweli huu; kwanza, Sababu ya kuumbwa kwa ulimwengu huu kulimpa nafasi ya kwanza na ya juu mwanadamu. Mungu alichagua kwa utukufu wake na furaha yake kumuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake, Mwa 1:26-27. Jambo la pili, Uhai wa mwanadamu una thamani kubwa sana mbele ya Mungu. Uhai huu ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu kwetu. Ni jukumu la mtu binafsi na jamii inayomzunguka kuulinda uhai huu kwa gharama zote. Katika jitihada hizi Mungu hatotuacha “Kwa sababu Bwana atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka,” Mit 22:23. Je, tunayosababu ya kuhuzunika pale tunapokandamizwa haki zetu na kunyanyaswa kwa uhai wetu? Lazima kuhuzunika kwa sababu siyo mpango wa Mungu bali ni mpango wa mwanadamu anayechukuwa nafasi ya Mungu. Ni hali yetu ya kibinadamu kama asemavyo Mtume Paulo, Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu,” Rum 9:1-2. Pamoja na hali hii bado tunayo matumaini makubwa sana kwa sababu Mungu wetu yu hai na huyaona mateso yote. Ni wakati tu utakapotimia atasimama katika kweli na haki.

Kipindi cha Yesu, Wayahudi kwa kuishika sabato yao, walikubali kuona mtu anatesaka hata kufa kuliko kuivunja sabato. Yesu anazihoji dhamiri zao, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo?” Lk 14:3. Maandiko Matakatifu yanatuambia kwamba wao wote walinyamaza. Yesu akalitenda lile lililo jema na lenye kumpendeza Mungu. Ukimya wa watu hawa unadhihirisha ni kwa namna gani haki za watu zinavyokanyagwa ili tu kulinda maslahi binafsi kwa wachache kupitia mgongo wa sheria ambazo ni kandamizi.

Kwa mara nyingine tena, Yesu anahoji dhamiri zao na matendo yao kwa kwenda ndani kabisa kwa yale wanayoyafanya kinyume na sheria zile kandamizi wanazoziamini na kuzishika. Yesu Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato?” Lk 14:5. Jambo hili walilifanya licha ya kuwa vinara wa kushika sabato kwa nguvu zote. Yesu anawathibitishia tena upofu wao juu ya sheria na amri za Mungu. Yesu anawathibitishia pia ukatili wao na uovu wao juu ya mapendo kwa jirani. Je, leo tunafanya tofauti tunapolitazama Taifa letu. Ni mara ngapi wenye haki hushutumiwa na mwisho kuhukumiwa wauaji, na wauaji kuwa huru? Ni mara ngapi tunashuhudia uovu uliokithiri na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa na watawala wenye dhamana ya mali na haki za raia zake?

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, na kama mmoja wa jamii ya watu wa Mungu na Taifa kwa ujumla wake, bado tunayo safari ndefu kuelekea mwanga kamili wa kweli na haki. Safari hii itakuwa fupi tu tukifanya mambo makubwa yafuatayo; Kwanza kabisa tumwogope Mungu na kuwa na hofu ya Mungu, na kwamwe tusichukue nafasi ya Mungu kwani hatutafanikiwa. Pili, kutoka moyoni mwetu tuikatae hali hii ya ukandamizaji kwa mawazo, maneno, na vitendo. Tatu, kila mmoja wetu atimize wajibu wake kwa haki na kweli. Na nne, tujali umoja wetu na uzalendo wetu kama Taifa.

Tumsifu Yesu Kristo!


Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure,” Zab 127:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario