martes, 13 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 28 YA MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 28 YA MWAKA-B
14/10/2015
Somo: Rum 2:1-11
Zab: 61:2-3, 6-7, 9
Injili: Lk 11:42-46
Nukuu:
Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale,” Rum 2:1

Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu?” Rum 2:3

kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu,” Rum 2:11

 Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo,” Lk 11:44 

Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu,” Lk 11:46 
TAFAKARI: “Hakuna upendeleo kwa Mungu."

Wapendwa wana wa Mungu, masomo yetu ya leo yanagusa maisha yetu ya kila siku. Jambo la msingi kabisa kabla ya kuzama katika tafakari hii, yatupasa kujua kila mmoja wetu katika ulimwengu huu hayupo hapa kwa bahati mbaya. Sote tupa katika ulimwengu huu kwa sababu ya upendo wa Mungu. Mungu alipenda tuwepo katika ulimwengu huu akizingatia muda, katika maana ya  lini tuwepo, tuishi katika ulimwengu huu kwa muda gani, na kwa namna ipi. Uwepo wako wa leo na sasa ni uratibishaji wa Mungu mwenyewe. Ingawa kuna wazazi haramu, hakuna watoto haramu. Yawezekana hawakuwa katika mpango wa wazazi wako lakini si kwamba hukupangwa na  Mungu. Kusudi la Mungu huweza pitia katika kosa au hata dhambi ya watu.

Uwepo wetu ni kusudi la Mungu na tokeo ya upendo wake. Mungu aliumba ulimwengu huu kwa sababu ya mimi na wewe tuishi. Mimi na wewe ni makusudio makubwa sana katika umbaji wa dunia hii. Hivyo, kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo,” Efe 1:4. Ukweli huu unathibitisha asili ya Mungu, yaani yeye ni UPENDO. Kwa mantiki hii hatuwezi kamwe kusema kwamba Mungu anaupendo, bali asili ya Mungu ni UPENDO.  Ndugu yangu,  “yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo,” 1Yoh 4:8. Ndugu yangu, kama kunaupendeleo ni huu ambao Mungu aliompa mwanadamu. Uwepo wako na mimi katika duniani hii ni waajabu na wa kupita viumbe vyote alivyo viumba. Tuna kila sababu ya kuona fahari hii ndani mwetu na kumsifu Mungu kila dakika ya pumzi yetu. Mungu, kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake,” Yak 1:18. Ndugu yangu unataka Mungu afanye nini zaidi kwako?

Je, una habari kwamba hata namna ya kuonekana kama ulivyo ni mpango kazi wa Mungu? Kwa nini basi wachukua muda mwingi kurekebisa kazi ya Mungu? Kwa nini basi wa mkosoa Mungu kwa kujibadili kile Mungu alichokifanya katika mwono na maumbile yako? Wengi miongoni mwetu hatuna furaha kwa sababu hatutaki kujipokea kama tulivyo na badala yake tunaishi maisha linganishi kila siku. Tunapenda kuwa kila wetu wanachotaka tuwe, mfano; wembamba kupita kiasi, au kuwa na nywele ndefu na zenye kuvutia. Ndugu yangu, elewa jambo hili, mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi,” Zab 139:15. Kile ulicho ni ufundi wa Mungu na kazi ya mikono yake mwenyewe.

Je, una habari kwamba Mungu alikuwa na mpango juu yako kuhusu lini utazaliwa, kwa muda gani utaishi hapa duniani, na lini itakuwa kikomo chako? Ukweli ni kwamba kila mmoja wetu yupo katika ulimwengu huu kwa sababu maalumu na kwa misioni maalumu ya Mungu mwenyewe. Mzaburi anatuambi,  Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado,” Zab 139:16. Ndugu yangu janja yako inatoka wapi?

 Wapendwa wana wa Mungu, ni kwa namna hii ya ajabu na makusudi ya Mungu kwetu yatupasa kuwa makini sana katika mahusiano yetu na kila mmoja wetu. Nafasi uliyokuwa nayo katika ngazi yoyote ile isiwe fimbo ya kuwachapia wengine. Nitambue nipo ulimwenguni hapa kwa sababu maalumu na wale niliokabidhiwa wapo kwa sababu maalum na makusudi ya Mungu. Hukumu niitoayo yapasa kuwa ya kweli na haki. Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale,” Rum 2:1. Kuondokana na kadhia hii yakupasa kuwa na hofu ya Mungu na kutenda yote katika kweli na haki.

Wapendwa katika Kristo, je, hatupaswi kutoa hukumu pale inapostahili? Yatupasa kutoa uamuzi wenye misingi ya upendo, kweli, na haki. Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu?” Rum 2:3. Maamuzi yetu yakijengwa katika msingi wa upendo, kweli na haki hatuwezi kuingia hatiani na hukumu ya Mungu. Mungu mara zote husimama na mtu mwenye haki. Hivyo katika kweli, na haki, hakuna upendeleo kwa Mungu,” Rum 2:11. Mungu hutuhesabia haki pale tunaposimama kusimama katika kweli. Na ukweli huu utatufanya kuwa huru. “Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:32. Katika jambo hili hakuna namna nyingine ya kuishi zaidi ya kusimama katika kweli.

Katika Injili ya leo Yesu anawakemea Mafarisayo na wana sheria kwa kutokuishi katika kweli na haki. Yesu anawafananisha Mafarisayo na wataka sifa bila kuwa na sifa, wajikwezao bila thaminisho la kweli, na mwisho wajipambao kwa uzuri na wema ingali wameoza kabisa ndani yao. Haya ndiyo makaburi yanayovutia machoni mwa watu ili hali ndani yake ni majanga na fedheha.  Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo,” Lk 11:44. Ndugu yangu, katika maisha yako jaribu mara zote kuwa kile ulicho. Hatua ya kwanza ni kuwa binadamu na kuikubali hali hiyo ya kibinadamu. Mungu hawezi kukupandisha ngazi nyingine kama haupo tayari kukubali ubinadamu wako aliyo kuumba kwa sura na mfano wake. Yesu alipowapa Mafarisayo ukweli juu ya maisha yao, wanasheria walimjia juu na kutaka kujua kama wao nao wapo salama. Yesu akawajibu, akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu,” Lk 11:46. Wana-sheria yawapasa kusimama katika kweli na haki siku zote. Leo katika jamii yetu, watu hawa wanadhamana kubwa sana katika mizania ya kweli na haki. Rushwa na ufisadi vimekuwa mitengo hatarishi sana katika utumishi katika sekta zote serikalini. Haki ya mtu haiwezi nunuliwa kwa gharama yoyote ile. Uwepo wa mtu na haki yake ambayo inayochezewa, hali hiyo imeweka na Mungu mwenyewe kwa chapa ya uumbaji wake wa peke wa mtu huyo. Hivyo ni Mungu mwenyewe anayestahili kulipwa haki hiyo.

Tumsifu Yesu Kristo!


Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8

No hay comentarios:

Publicar un comentario