domingo, 11 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 28 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 28 YA MWAKA-B
12/10/2015
Somo: Rum 1:1-7
Zab: 97:1-4
Injili: Lk 11:29-32
Nukuu:
ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake,” Rum 1:5

ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo,” Rum 1:6

Na makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona,” Lk 11:29

Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona,” Lk 11:32

TAFAKARI: “Maisha bila Mungu ni sawa safari bila kuijua njia.”

Wapendwa wana wa Mungu, ulimwengu wetu wa leo pamoja na maendeleo yake, binadamu amefikia hatua ya kufikiri na kuishi bila Mungu. Watu walio wengi leo sio kwamba hawataki kuamini kuwa Mungu yupo bali hawataki kusikia kabisa kuhusu Mungu. Leo walio wengi uweka umuhimu wao katika kazi zao, namna ya kupata pesa, namna ya kupata umaarufu, na mwisho wa siku namna ya kuyafurahia maisha. Tupo kwenye ulimwengu wa vitu na kuviabudu vitu hivyo ndiyo imekuwa  sanamu ya kila siku.

Maisha ya mwanadamu bila Mungu hayana maana yoyote. Uwepo wako hapa duniani ni kwa sababu Mungu alipenda uwe hivyo na alikuwa na mpango nawe hata kabla ya kutungwa mimba kwako. Hivyo hakuna mtu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe. Kwa maana, “mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,” Efe 2:20. Yesu Kristo ndiyo msingi wa yale yote tuyafanyayo kwa sababu kwa kupitia Yeye yote tuyaonayo kwa macho yetu yalifanyika. “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Hapa ndipo tunapouona Umungu wa Yesu na uwezo wake juu ya vitu vyote.

Hivyo katika Injili ya leo Yesu anawakaripia wale wasioamini uwepo wake na kubakia tu katika Ishara. Ujumbe anaotupa Yesu leo ni kwamba Yeye ni zaidi ya Ishara zile tuzionazo. Ishara utusaidia tu kuelewa na kuamini mambo yale yaliyopita ufahamu wetu. Ila kwa ishara hizo kama zilivyo haziwezi kulingana na Kristo ambaye katika mambo yote yaliweza kuwa kupitia yeye mwenyewe. Hivyo msingi wa imani yetu haupo kwenye Ishara. Yesu anawaambia makusanyiko ya watu na sisi pia katika ulimwengu wetu leo  kwamba, “Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona,” Lk 11:29. Ishara ya Yona ilikuwa kwamba baada ya kukaidi kwenda Ninawi alimezwa na samaki na kukaa ndani ya tumbo la samaki kwa siku tatu.  Kwa Ishara hii, Yesu aliwafunulia kusanyiko lile Ishara ya ufufuko wake uliotokea siku ya tatu baada ya mateso, kusulubiwa msalabani na kufa. Hii ndiyo Ishara kubwa kupita zote na kielelezo cha uzima wa milele.

Wapendwa wana wa Mungu, tusipoyaona maisha yetu katika mtazamo huu wa umilele, maisha na fahari yake yote hapa duniani hayana maana yoyote. Ninawi walikengeuka na kumwasi Mungu, ila walitubu na kupata msamaha wa Mungu kupitia Nabii Yona. Hawa walioamini na kumsadiki Mungu pasipo shaka ndio watakao kuwa mahakimu wetu siku ya kiama. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona,” Lk 11:32. Miongoni mwetu hata leo wapo watu ambao kwa maisha yao na wongofu wao Mungu anasema nasi kupitia wao. Hawa pia siku ya mwisho watakuwa mahakimu wetu. Mara nyingi tumekuwa vinara wa kuwanyanyapaa kwa mabadiliko yao ya kiroho kwa kuzidi kuwafananisha na maisha yao ya zamani. Hili ni kosa kubwa sana kiimani. Hakuna mwenye hati miliki ya maisha ya umilele. Sote tunaitaji upendo na huruma ya Mungu katika kuhesabiwa haki na kuwa warithi wa maisha hayo ya umilele.

Je, wa mwamini Yesu Kristo? Mtume Paulo anatuambia wazi kwamba, ni katika Yesu Kristo, ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake,” Rum 1:5. Katika jambo hili la msingi, Yesu Kristo ndiye njia ya safari yetu ya maisha ya umilele na hakuna mbadala wake. Kwa kuuishi ukweli huu, na kuufanya wengine wauishi kwa kujitoa kwetu pasipo kujibakiza ndiko kunakotufanya sisi kuwa wateule wa Kristo. Hivyo kwa kupitia hawa tuliojitoa kwao bila kujibakiza ili wamjue Mungu, wampende, wamtumikie na mwisho warudi kwake kwenye uzima wa milele, “katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo,” Rum 1:6. Usifikiri hata mara moja unapoteza muda wako kwa kuwalisha neno watu wa Mungu. Usisikitike hata mara moja unapotumia muda wako kwa ajili ya wokovu wa watu. Kuna furaha kubwa sana kwa Mungu ikiwa kwa kupitia kwako mtu mmoja alipata wokovu na kwenda Mbinguni kwenye maisha ya umilele. Ndugu yangu uliyesafari nami katika tafakari hii, maisha bila Kristo Yesu ni sawa na safari bila kuijua njia.

Tumsifu Yesu Kristo!


“Maana, ijapokuwa naihubiri njili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri njili!” 1Kor 9:16

No hay comentarios:

Publicar un comentario