lunes, 12 de octubre de 2015

JUMANNE WIKI YA 28 YA MWAKA-B
13/10/2015
Somo: Rum 1:16-25
Zab: 18:2-5
Injili: Lk 11:37-41
Nukuu:
Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia,” Rum 1:16

Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao,” Rum 1:24

Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu,” Rum 11:39

Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu,” Rum 11:41

TAFAKARI: “Injili ni uweza wa Mungu uletao wokovu. Na hii ndiyo habari njema kwetu”

Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli kwamba binadamu leo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika fani ya habari ikiwa ni wepesi wa kupata habari hizo na hata kuzitengeneza, na kuzisambaza. Pamoja na mafanikio haya, mwanadamu hajawa na amani ya kutosha na usalama wake katika ulimwengu huu wa leo wa sanyansi na maendeleo yake. Wepesi wa kupata habari na kusambaa kwake kumekuwa ndiyo sababu kubwa ya kumwongezea hofu. Kwa maana nyingine tumefanikiwa katika mawasiliano kiiujumla na sio kwa kile tunachowasiliana (ujumbe). Ujumbe wa mawasiliano yetu bado haujawa habari njema kwetu. Neno la Mungu ni habari njema kama lilivyo, uzima, na wokovu wetu. Hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu na kama mbatizwa kuliishi neno la Mungu na kutolionea haya. Kwa maana nyingine kila mbatizwa apaswa kuwa habari njema kwa wengine. Mtume Paulo anatuambia, Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia,” Rum 1:16. Neno hili ni uzima na wokovu kwa kila mmoja wetu tunapolishika na kuliishi.

Leo ni wachache sana kati yetu tunaochukua hata muda kidogo kulisoma neno la Mungu. Hatulipendi neno hili kwa sababu huzisuta nafsi zetu. Ulimwengu tunaoishi kila na kila tunapopita unatupa ujumbe huu, “maisha bila Mungu yanawezekana. Hivyo weka umuhimu katika maisha yako na hasa utazame mwili wako.” Tunapolipiga kisogo neno la Mungu basi maisha yetu ya kiroho huwa hatarini. Mwili uinuliwa kupita kiasi na mwisho wa siku tunakosa yote. Maisha ya mtindo huu hayatupi amani yoyote zaidi ya hofu na mashaka muda wote. Hivyo, kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao,” Rum 1:24. Tuelewe kwamba miili yetu ni mitakatifu kwa sababu ndilo hekalu la Roho Mtakatifu. “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe,” 1Kor 6:19. Kama mwili ni nyumba ya Roho na Nafsi, nyumba hii inapokuwa chafu huathiri pia Nafsi na Roho, hasa pale nafsi inapoegemea katika mwili. “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabibu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana,” Rum 12:1. Wito huu ni wa kila mmoja wetu kadiri ya wito wake.

Tatizo kubwa la kutokufikia malengo mazuri ya kuishi maisha ya kiroho kadiri ya mpango wa Mungu ni pale tunapoweka umuhimu wa vitu pasipo kuwa na umuhimu. Mfumo wa maisha unaobeba falsafa hii utuzeesha kabla ya wakati na kupotea muda bure. Katika Injili ya leo Yesu analiona hilo kwa Mafarisayo na analikemea kwa nguvu zake zote. “Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu,” Rum 11:39. Huku ni sawa na kufunga bandeji kwanye paji la uso kusikokuwa na kidonda ukaacha kufunga kidonda kinachotoa usaa mguuni. Kwa upande mwingine hili ni tatizo la kutokujipokea kama ulivyo na kuanzia hapo ulipo ndipo uweze kusonga mbele kuliko kuzuri zaidi. Kuyagusa maisha yako ya ndani na usiyopenda kuyazungumza ndipo kuliko na ufunguo wa maisha yako. Tunapenda sana kuangalia tamthilia za watu mbalimbali maarufu ulimwenguni na mwisho wa siku tunasahau kuwa tamthilia nzuri na ya pekee ni kuhusu maisha yako. Yatazame maisha yako ya ndani utagundua unafiki wako mbele ya Mungu na kwako mwenyewe. Eneo hili ni muhimu sana kuligusa kwani ndiyo wewe mwenyewe. Wokovu wa mtu huanzia hapa kama hatua ya ndani na ya mabadiliko kiroho.

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, yale yote tuyatoayo nje na kuyafanya huakisi maisha yetu ya ndani. Ni kweli unaweza kuficha hali na ukweli wako wa ndani na kutenda kwa kuwapendezesha watu au kutenda kwa kadiri ya mazingira fulani. Ukweli ni kwaba huwezi kuificha hali hii kwa muda wako wote.  Zawadi yako kubwa kwa Mungu ni kuyatoa yale yaliyo ndani mwako kwake kwani ndani humo kuna chapa yake. Kumbuka umeumbwa kwa sura na mfano wake. Chapa hii ya Mungu ndani kwako hufifishwa na dhambi zako. Unapoishi katika hali ya neema na utakaso, taswira hii ya Mungu ndani yako hung’ara na kufanywa upya siku kwa siku. Hivyo, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu,” Rum. Wapendwa wana wa Mungu, hivyo vya ndani ndivyo vimpendezavyo Mungu kwa sababu vina chapa yake.

Tumsifu Yesu Kristo!


“Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu,” 2Tim 2:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario