JUMANNE WIKI YA 29 YA MWAKA-B
20/10/2015
Somo: Rum 5:12, 15b,
17-19, 20b-21
Zab: 40: 7-8a, 8b-9,
10, 17
Injili: Lk 12:35-38
Nukuu:
“kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi
walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu
mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi,” Rum 5:15b
“Basi tena, kama kwa
kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu
wote walihesabiwa haki yenye uzima,” Rum 5:18
“Na
dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi; ili
kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya
haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu,” 5:20b-21
“Viuno vyenu na viwe
vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka,” Lk 12:35
“nanyi iweni kama watu
wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha,
wamfungulie mara,” Lk 12:36
“Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo
atawakuta wanakesha,” Lk 12:37a
Wapendwa wana wa Mungu, masomo yetu ya leo
yanatuelekeza kutafakari kuhusu muda wetu wa kuishi hapa duniani na mahusiano
yetu na Kristo. Ni kweli kwamba kifo bado ni tishio na hakizoeleki. Pamoja na
ukweli huo, kifo hakiwezi kuepukika kama mimi na wewe tu hai leo. Ndugu yangu
ipo siku tutakakufa iwe tunapenda au hatupendi. Leo sina lengo la kukutisha
kuhusu kifo, ila ni vyema kuuzungumza ukweli huu ambao mara nyingi hatupendi
kuusikia. Kunatofauti kubwa sana kati ya yule anayemwamini Kristo na asiyemwamini
juu ya ukweli kuhusu Kifo. Ndani na katika Kristo kifo hakina nguvu tena.
Katika Injili ya leo, pamoja na ukweli huu juu ya kifo, Yesu anatuwasa kwamba, “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa
zenu ziwe zinawaka,” Lk 12:35. Kuvifunga viuno ni kuwa
tayari katika maana ya kujiandaa vyema kwa lolote lile ukilenga lililo salama
zaidi. Ni kuishi maisha yenye kumpendeza Mungu kwa gharama zote. Jambo la pili
katika maana hiyo ya kuvifunga viuno ni kwamba taa zetu ziwe zinawaka,
ikimaanisha kuishi maisha yasiyo na hatia. Ni kuishi maisha ya kuuchuchumilia
ukamilifu ingawa udhaifu upo. Kila siku upewayo na Mungu iwe nafasi ya kuongoka
kwako. Ukweli huu unatupelekea kuyaona maisha hapa duniani ni JUKUMU LA MUDA
MFUPI. Je,
unamtazamo gani kuhusu maisha yako?
Ndugu unayesafiri nami katika tafakari
hii, ni ukweli usiofichika kwamba maisha hapa duniani ni jukumu la muda mfupi.
Je, unabisha? Maandiko Matakatifu hufundisha na kutukumbusha maisha yetu
duniani yalivyo mafupi na yasiyodumu. Maisha yanaelezwa kama ukungu, mkimbiaji,
pumzi, na mvuke. "Kwani sisi tu wa
jana tu, wala hatujui neno, kwa kuwa siku zetu duniani ni kivuli tu." Ayu
8:9
Ndugu, ili kutimiza
vizuri maisha yako hupaswi kusahau ukweli wa aina mbili: Kwanza,
yakilinganishwa na umilele, maisha ni mafupi sana. Hivyo, “nanyi
iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili
atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara,” Lk 12:36. Pili, dunia ni
makazi ya muda tu. Hatuwezi kukaa hapa kwa muda mrefu, hivyo usijishikamanishe
sana nayo. Yesu leo anatuambia, “Heri
watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha,” Lk 12:37a. Tumwombe Mungu atusaidie kuyaona
maisha ya duniani kama anavyoyaona yeye mwenyewe. Mfalme Daudi aliomba,
"Bwana, nijulishe mwisho wangu, na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani;
nijue jinsi nilivyo dhaifu," Zab 39:4
Ndugu yangu hapana shaka wa mfahamu
vizuri "inzi!" Mdudu huyu kadiri ya utafiki wa kisayansi huishi siku
saba tu. Ni wiki moja kati ya wiki 52 katika mwaka mmoja. Tazama fujo na papara
za inzi. Hutua kila mahali kwa siku hizo saba; kwenye vyakula (vilivyo chacha
na visivyo chacha), kwenye vinjwaji, kwenye vidonda, kwenye vinyesi, nk. Tazama
anavyoongea kwa ishara akiwa amenyanyua miguu yake ya nyuma na kusema,
"yaliyopita yeshapita." Na anapoinua miguu ya mbele husema hivi,
"yajayo na yaje, ponda mali, furahia yote, haya ndiyo maisha."
Ndugu, tulio wengi leo
maisha yetu hayana tofauti na haya ya inzi. Hutaka kufanya yote na kujaribu
yote katika maisha. Hakuna muda wa maandalizi wala tafakari kuhusu umilele wetu
kama zawadi ya pekee tuliyopewa sisi wanadamu. Maisha yetu leo yana maana sana “kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule
mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema
yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi,” Rum 5:15b.
Yesu Kristo katurudishia hadhi ya kuwa tena wana wa Mungu na warithi wa ufalme
wake wa mbinguni.
Jambo la ajabu ona tunavyoishi na jirani
zetu! Unaweka wigo "fence" kiasi kwamba unamzuiya hata jirani yako
kufungua mlango. Ona! tusivyo wajali wengine afya zao! Tunaelekeza maji taka
kwenye makazi yao bila huruma. Eti kwa vile unapesa, na unajulikana hadi
usalama wa Taifa. Eti kwa vile wewe ni kiongozi wa ngazi za juu kwenye utawala
dhalimu. Eti kwa vile wewe ni mfanya biashara maarufu nchini. Je, hili ndilo
kusudi la Mungu kwa maisha yako hapa duniani?
Ndugu yangu, usisahau
kuwa maisha ya hapa duniani ni sawa na kuwa ugenini. Haya si makazi yako ya
kudumu, au hatma yako ya mwisho. Unapita tu!
Unatembea tu duniani. Mfalme Daudi anatukumbusha, "Mimi ni mgeni
katika nchi, usinifiche maagizo yako," Zab 119:19, na Mtume Petro anasema, "na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye
kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika
wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni." 1Pet 1:17. Waamini wa kweli
wanafahamu wazi kwamba kuna mambo mengi ya maisha kuliko hii miaka michache
tunayoishi hapa duniani. Uhakika huu tunapewa na Kristo mwenyewe baada ya
kukishida kifo kwa sadaka yake pale msalabani. Sote tumehesabiwa haki kwa kifo
cha Kristo. “Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa
adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye
uzima,” Rum 5:18
Ndugu, kitambulisho
chako kiko katika umilele, na nchi yako ni mbinguni kwa sadaka ya Bwana wetu
Yesu Kristo aliyekubali kuutoa uhai wake ili mimi na wewe tuwe huru kutoka
utumwa wa dhambi. “Na dhambi ilipozidi, neema
ilikuwa nyingi zaidi; ili kwamba,
kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema
itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu,” 5:20b-21. Yote haya
yawezekana kwako na kwangu kwa neema tu ya Mungu. Unapofahamu ukweli
huu, utaacha kuwa na wasiwasi wa "kupata kila kitu" hapa duniani.
Mungu yupo wazi kabisa kuhusu habari za kuishi kwa ajili ya "hapa" na
"sasa" tu huku ukijifananisha na watu wa dunia hii katika kipaumbele na
mtindo wa maisha.
Tunapochezacheza na majaribu ya dunia
hii, Mungu anaita hali hiyo uzinzi wa kiroho.
"Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki ya dunia ni kuwa adui
wa Mungu?" Yak 4:4. Karipio hili kwa maana nyingine la tuambia kwamba
'twajidanganya mbele za Mungu iwapo tunachotaka ni mambo yetu, kuchezacheza na
ulimwengu kwa kila nafasi tunayopata mwisho wetu ni kuwa maadui wa Mungu na
njia yake.' Rejea mfano wa inzi hapo juu. "Basi tu wajumbe kwa ajili ya
Kristo..." 2Kor 5:20. Cha kusikitisha, wakristo wengi tumemsaliti mfalme
wetu na ufalme wake. Katika hali ya upumbavu tumeamua kwamba kwa sababu
tunaisha hapa duniani, basi hapa ndiko nyumbani kwetu. "Wapenzi, nawasihi
kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipinganazo na roho."
1Pet 2:11.
Mungu pia anatuonya tusijishikamanishe
sana na vitu vinavyotuzunguka kwa kuwa si vya kudumu. "Na wale wautumiao
ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu
yanapita." 1Kor 7:31. Ni wazi yatupasa kufanya kazi na kujipatia mahitaji
yetu ya kila siku. Ila yote hayo tuyapatayo hatupaswi hata mara moja
kujilinganisha nayo. Utu wetu na watu wengine ni zaidi ya mali hizo. “Nanyi
mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu;
mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa
damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya
Kristo,” 1Pet 1:18-19
Ndugu, ni ukweli usiotia shaka kwamba
kwa mivuto ya hali ya juu, na vyombo vya mawasiliano vyenye kutia upofu, na
mambo mengi ya anasa yaliyopo siku hizi, ni rahisi kusahau kwamba maisha si
kufanya raha tu. Ndugu sikuonei gele bali nakukumbusha tu!
Ni pale tu tunapokumbuka kuwa maisha ni
majaribu, dhamana, na jukumu la muda
mfupi ndipo mvuto wa mambo ya anasa utakapokosa nguvu maishani mwetu. Hili
likifikiwa twaweza kujiandaa kwa jambo jingine ambalo ni bora zaidi. "Kwa
maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.
"2Kor 4:18b.
Ukweli ni kwamba dunia si makazi yetu ya
kudumu huelezea kwa nini, kama wafuasi wa Kristo, tunapatwa na magumu, huzuni,
na kukataliwa (Yoh 15: 18-19; 16:20; 16:33). Ukweli huu pia hueleza kwa nini
baadhi ya ahadi za Mungu huonekana kutotimizwa, baadhi ya sala hazijajibiwa, na
baadhi ya mazingira kuonekana kutokuwa na haki. Huu si mwisho wa mambo.
Ili kutufanya tusijifungamanishe na
ulimwengu sana, Mungu huruhusu tusikie hali fulani ya kutokuridhisha na
kutosheka katika maisha-hitaji ambalo "haliwezi" kutoshelezwa kamwe
hapa duniani. Hatuna furaha kabisa hapa kwa sababu hatutakiwi! Dunia si makazi
yetu ya milele, tumeumbwa kwa ajili ya kitu bora zaidi.
Ndugu yangu, samaki hawezi kuwa na
furaha kuishi nchi kavu, kwa sababu ameumbwa kwa ajili ya kuishi majini. Tai
kadhalika asingefurahi kama asingeruhusiwa kupaa angani. Hatuwezi kamwe kujisikia
kutosheka kabisa hapa duniani, kwa sababu tumeumbwa kwa mambo mengine zaidi.
Utakuwa na vipindi vya furaha hapa, lakini hakuna cha kufanana na kile Mungu
amepanga kwa ajili yako.
Kwa kutambua kwamba maisha ni jukumu la
muda mfupi tu ni lazima kubadili kabisa mambo unayoyaona ya muhimu maishani
mwako. Mambo ya milele, yasiyo ya muda mfupi, yapasa yawe vigezo vya maamuzi
yako. Kama C. S. Lewis anavyosema, "Kila kisicho cha milele hakifai
milele.” Naye Mtume Paulo anatuambia, "Tusiviangalie vinavyoonekana, bali
visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni
vya milele," 2Kor 4:18.
Ndugu, ni kosa kubwa kudhani kuwa mpango
wa Mungu kwa ajili ya maisha yako ni mafanikio ya mali au mafanikio ya siku
hizi, katika ulimwengu unavyoyaona. Maisha tele hayana uhusiano na mali tele,
na uaminifu kwa Mungu hautuhakikishii kuwa na mafanikio ya kazi au huduma,
usitazamie taji zisizodumu (1Pet 2:11). Pia, "usiogope mtu atakapopata
utajiri, na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua
chochote; utukufu wake hautashuka ukimfuata," Zab 49:16-17.
Paulo Mtume baada ya kuongoka kwake
alikuwa mwaminifu lakini alijikuta gerezani. Yohane Mbatizaji alikuwa mwaminifu
lakini alikatwa kichwa. Mamilioni ya watu waaminifu wameuawa, wamepoteza kila
walichokuwa nacho, au maisha yao yamekoma wakiwa hawana kitu. Lakini mwisho wa
maisha haya si mwisho, bali mwanzo wa maisha mapya ya umilele. Kifo kwa njia ya
haki ndani na katika Kristo ni kuzaliwa katika maisha ya umilele. Hapa kifo
huwa njia, au daraja la kuvuka kwenda kwenye umilele.
Ndugu niliyesafiri nawe katika tafakari
hii, naomba nisikuchoshe. Katika macho
ya Mungu, mashujaa wa imani sio wale waliopata mali, wenye mafanikio na nguvu
katika maisha haya, bali ni wale wanaoyaona maisha kama jukumu la muda mfupi na
kutumia muda huo kwa uaminifu, wakitumaini kupokea thawabu yao katika umilele.
"Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona
tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu
ya nchi. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo
Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao, maana amewatengenezea mji," Ebr 11:13,
16. Asante kwa kusafiri nami. Tafakari na chukua hatua.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Maana miaka elfu machoni pako ni
kama siku ya jana ikiisha kupita, na kama kesha la usiku,” Zab 90:4
“Basi,
kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote
yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36
No hay comentarios:
Publicar un comentario