viernes, 23 de octubre de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 29 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 29 YA MWAKA-B
23/10/2015
Somo: Rum 7:18-25a
Zab: 119:66, 68, 76, 77, 93, 94
Injili: Lk 12:54-59
Nukuu:
Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo,” Rum 7:19 

Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu,” Rum 7:20

Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu,” Rum 7:22-23

Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?” Lk 12:56

Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani,” Lk 12:58

TAFAKARI: “Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli kwamba kwa asili ya binadamu kama alivyoumbwa na sura na mfano wake Mungu, si asili yake kutenda uovu. Kwa nini basi lile jema alipendalo halifanyi, na lile baya asilolipenda hulifanya? Kadiri ya mafundisho ya Mt. Augustino anasema hivi; “Hata baada ya maanguko ya mwanadamu Mungu hakumuondolea mwanadamu ule uhuru wake. Angefanya hivyo basi Mungu asingekuwa na haki ya kumuhukumu mwanadamu kwa sababu mwanadamu huyu angekuwa hana utashi wake mwenyewe na hivyo kosa au dhambi isingekuwepo wake. Hata hivyo Mungu kwa upendo wake mkuu alimwachia mwanadamu uhuru wake, na kwa njia hiyo mwanadamu huweza kuziacha njia zake mbaya na kumrudia Mungu.”

Tukirudi kwa Mtume Paulo, anamwona mtu katika hali hii: Mwili, Nafsi, na Roho. Mtu huyu husukumwa na kutenda kadiri na mwitikio wa nafsi yake. Kwenye nafsi ya mtu ndipo penye dhamiri yake. Nafsi ni kama mnara wa kuongoza ndege. Nnara huu ukiegemea mwili basi matendo ya mwili tunayajua kama tusomavyo, Gal 5:19.21. Na nafsi ikiegemea Roho, tunaona matunda ya roho kama tusomavyo, Gal 5:22-23. Hata hivyo, kama asemavyo Mt. Augustino, mwanadamu bado ananafasi ya kufanya vizuri hasa ataamua na kutumia uhuru uliopo ndani mwake wa kuchagua jema na kuacha baya. Hivyo ni kwa mantiki hii Paulo anasema, Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo,” Rum 7:19. Je, hapa wa kulaumiwa ni nani? Je, tumalaumu Mungu aliyetupa uhuru huu, au sisi wenyewe kwa kutokutumia uhuru wetu vyema?

Sheria ya Mungu katika utu wa ndani, ni UHURU aliyopewa mwanadamu umsaidia katika mambo mazuri kumwelekea Yeye na ufalme wake. Kufurahia uhuru huu katika ubaya ndilo anguko la mwanadamu. Sheria ya utu huu wa ndani, yaani uhuru ulionao unapoifanya nafsi yako kuegemea mwili, ndipo mtu anapodondoka kwenye dhambi iliyo katika viungo vyake. Hii ni sawa na nafsi kupigwa mwereka na uhuru huu ambao ndiyo sheria ya ndani ya utu wako. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu,” Rum 7:22-23. Kujinasua katika mtego huu ni kutambua na kuyafanya matendo ya Roho ambayo ndani kwayo yamejaa uhai na uzima, Gal 5:22-23.

Unapotambua hali hiyo na usifanye chochote ndicho anachosema leo Yesu katika Injili. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?” Lk 12:56. Ni kuujua ukweli kama ulivyo  nawe ukabaki katika ubishi na ung’ang’anizi usio na uzima ndani yake. Watesi wa Yesu nyakati zake, hasa Waandishi, Mafarisayo na Wanasheria, waliujua ukweli lakini waliupindisha kwa makusudi kukidhi haja zao na maslahi yao.

Yesu anawashauri na kutushauri sisi leo kwamba, kama tunaufahamu ukweli basi tuufuate na kuufanya tungali hai kwani hakimu wetu Mungu yupo anasafiri nasi kuelekea kwenye kiti hukumu. Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani,” Lk 12:58. Kumbe kabla ya kutupwa gerezani, yaani kwenye mateso yasiyo na mwisho, Mama Kanisa anatushirikisha huruma ya Mungu kwa kupitia sakramenti ya upatanisho. Sote tunahitaji toba na kupatanishwa na Mungu kila tunapodondoka katika dhambi.

Tumsifu Yesu Kristo!


“Basi zaeni mtunda yapasayo toba,” Mt 3:8

No hay comentarios:

Publicar un comentario