viernes, 30 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 30 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 30 YA MWAKA-B
31/10/2015
Somo: Rum 11:1-2a, 11-12, 25-29
Zab: 94:12-13a, 14-15, 17-18
Injili: Lk 14:7-11
Nukuu:          
Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali,” Rum 11:2

Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu,” Rum 11:11b

Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili,” Rum 11:25 

Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.” Rum 11:27 

Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake,” Rum 11:29

Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe,” Lk 14:8

akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma,” Lk 14:9 

Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe,” Lk 14:10

Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11 

TAFAKARI: “Pungua ili Mungu awe na nafsi juu ya maisha yako.”

Wapendwa wana wa Mungu, ulimwengu na vyote vilivyomo vyaufunua Utukufu na Furaha ya Mungu. Hivyo uwepo wako kama binadamu ni Utukufu wa Mungu na Furaha yake. Kwa namna nyingine kujikweza kwetu na kutokuenenda kama binadamu ni chukizo kwa Mungu aliyetuumba. Huku ni kuasi na kujitenga na Mungu. Kuukubali ubinadamu wako ni sawa na kupungua ili Mungu awe na nafasi juu ya maisha yako. Mwenye hofu ya Mungu hukiri kwamba, “kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu,” Zab 90:2. Kuumbwa kwetu kama tulivyo ni mpango wa Mungu na ndiyo maana, Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali,” Rum 11:2.

Lakini jambo la ajabu na kushangaza ni kwamba, binadamu huyu hujisaha sana na kufanya atakayo na kusahau kuwa Mungu ndiye kila kitu kwake. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?” Isa 43:13. Ulevi wa sifa na madaraka umekuwa moja ya vyanzo vya uasi wa mwanadamu juu ya Ukuu wa Mungu. Ulevi huu wa sifa na madaraka uharibu yote mazuri aliyoyafanya Mungu juu ya mwanadamu na mwisho wa siku yote hujeuka na kuwa ubatili.  Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua,” Zab 39:6. Huku ndiko kujiamini kwa kipumbavu ilhali hatujui hata hatma ya maisha yetu kwa sekunde moja ijayo.

Ndugu yangu, kumcha Bwana ni kuishi katika umilele alioukusudia ndani ya maisha yako. Hizo ndizo fadhili za Bwana kwa kila anayemcha. Ndugu yangu, fadhili za Bwana zina wamchao tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana,” Zab 103:17. Ni kwa upendeleo wake Mungu aliamua kuanzisha uhusiano wake na mtu na mwisho kama Taifa, yaaani, Israeli, ili kukamilisha kile alichokusudia kwa wanadamu wote yaani kutupatia uzima wa milele. Ila kwa kujikweza na kuasi kwa watu hawa mara kwa mara Mungu alijiweka pembeni ili wajifunze na kumrudia kwa unyenyekevu. Hivyo kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu,” Rum 11:11b. Waisraeli walipewa upendeleo lakini walijisahau bila kujua ukweli huu kwamba, karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake,” Rum 11:29. Majanga yote utupata tunaposhindwa kufahamu mipaka yetu na ubinadamu wetu.

Leo katika somo la Injili Yesu anatupa angalizo hasa tunapoalikwa kwenye tafrija mbalimbali. Tukizama ndani zaidi tunaona kwamba uhai tulionao na maisha tunayoyaishi ni sawa na kualikwa kwenye furaha ya Mungu na utukufu wake. Basi ni vyema mimi na wewe kutambua duniani hapa tunapita tu, na tupo kwa maandalizi ya maisha ya umilele. Yesu anatuwasa hivi kuhusu ukweli huu; Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma,” Lk 14:8-9. Kama sote tumealikwa harusini ni wazi tumepewa mastahili yaliyo sawa na yule aliyetualika. Basi yatupasa kujua kuwa sote ni waalikwa na siyo ‘mgeni rasmi.’ Kwa utaratibu wa kawaida mbele palipoandaliwa si mastahili yangu. Kumbe ni vyema na busara kutafuta nafasi nyingine. Ili kuwa sehemu salama zaidi, Yesu anatuasa hivi; Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe,” Lk 14:10. Huku ndiko kwa maneno mengine kupungua ili Mungu awe na nafasi juu ya maisha yako.

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii utakubaliana nami kwamba kati yetu kwa nafasi tulizokuwa nazo na madaraka tuliyonayo yaliyopitiliza hututia upofu na kutufanya kuwa ndiyo fimbo ya kuchapia wengine. Jeuri hii ndugu yangu tunaipata wapi wakati Maandiko Matakatifu yanatuambia, Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara,” Zab 90:10. Jinyenyekeshe basi na kuwa kile Mungu alichokusudia katika maisha yako.

Tusifu Yesu Kristo!


Bwana huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri,” Zab 147:6

No hay comentarios:

Publicar un comentario